Kipi kinawasukuma watu kujiuwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati fulani maisha yanaweza kututupa katika hali ngumu ya dhiki na kukata tamaa, kufadhaika, chuki, mawazo na huzuni. Hayo yanaweza kuwafanya watu wengi kutaka kujitoa uhai.
Kujiua ni suala zito ambalo huja akilini mwa mtu kama suluhisho. Ingawa ni vigumu kuelewa sababu ya mtu kujaribu kujiua, watu wanaojaribu kujiua ndio wanajua kinachoendelea vichwani mwao.
Shirika la Nigeria Health Watch, linasema watu wa rika zote hupata mawazo ya kujiua. Lakini mawazo ya aina hiyo yapo zaidi miongoni mwa watu wenye magonjwa ya akili. Vilevile watu wanaokabiliwa na migogoro, maafa, vurugu na unyanyasaji, au hasara na kutengwa.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), zaidi ya watu 700,000 hufa kwa kujiua kila mwaka. Kijiua ni sababu ya nne ya vifo kati ya vijana wa miaka 15 hadi 29.
Shirika hilo linaeleza asilimia 77 ya vifo duniani hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati. Kutumia dawa za kuua wadudu, kujinyonga na kujipiga risasi ni miongoni mwa njia zinazotumika zaidi kujiua duniani kote.
Hannatu mwenye miaka 33 aliambia BBC jinsi familia yake ilivyokuwa chanzo cha yeye kufikia kutaka kujiua. Miaka minne iliyopita, Hannatu alijikuta katika hali ambayo baba yake, alikuwa akisisitiza aolewe na mtu ambaye hakumtaka.
"Baba alikuja na wazo niolewe na binamu yake, akanieleza kuwa lazima niolewe. Nikasema sitaki, mama naye akaniunga mkono. Baba akaniambia nichague kati ya yeye au mama yangu."
“Nilikuwa nikihangaika na mawazo na siku moja majira ya saa 8:30. nilienda kupanda kisima. Kisima hicho kinateleza sana kwani hata tukiteka maji tunaonywa tusipande juu ya kisima, lakini nilipanda juu japo nilijua naweza kutumbukia.’’
Hannatu anasema akiwa katika hali hiyo, ndipo mawazo na hofu juu ya Mungu vikamjia. Mara moja akakumbuka fatwa inayosema kila Mwislamu anayejiua ni mwana wa motoni.
“Niliamini nikijiua nitaingia motoni, kwa sababu katika Uislamu inaelezwa mtu akijiua kwa kukusudia ataingia motoni, hilo ndilo lilinifanya nishuke."
Sababu za kufikiria kujiuwa

Chanzo cha picha, PA Media
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Daktari wa upasuaji wa mishipa ya fahamu, Nafisa Hayatuddeen ameiambia BBC kwamba asilimia 80 ya majaribio ya kujitoa uhai yanaweza kuzuiwa.
Daktari Hayatuddeen anasema utafiti nchini Nigeria, unaonyesha watu 9 kati ya 100,000 wana mawazo ya kujiua. Anaongeza kuwa ndugu na familia za mtu mwenye mawazo ya kujiuwa humchukia na ndiyo maana hawajitokezi na kusema.
Daktari anasema kuna mambo tofauti ambayo yanaweza kumfanya mtu ajaribu kujiua lakini madaktari hutazama mambo matatu.
“Kwanza tunaangalia mambo ya kibaiolojia, kwa sababu tunajua kuna watu ambao kwa mfano upande wa wazazi wao au babu zao kuna mtu alijiua. Unaweza kurithi wazo hili."
"Pili, sababu za kisaikolojia ambazo huathiri maadili, mawazo ya mtu au jinsi mtu anavyoyatazama maisha au anavyojitazama mwenyewe."
“Kuna watu jambo dogo wanaliweka moyoni, au linapotokea jambo wanalichukulia kuwa ni tatizo kubwa na kulifanya kuwa tatizo kubwa kana kwamba haoni chochote zaidi ya hilo."
“Mtazamo wa tatu ni sababu za kijami, ni mambo yanayotokea katika maisha ya mtu au yale yanayotokea karibu naye na yanaathiri maisha yake.’’
"Kwa mfano, hali ya umaskini, ukosefu wa ajira, ukosefu wa chakula, mateso, maumivu na mengine mengi, matatizo haya yote ya kila siku yanaweza kusababisha watu kufikiria kujiua."
Dkt. Hayatuddeen anasema kuna mawazo au hesabu ambazo mtu huzifanya kichwani kabla ya kuamua kujiuwa. Wazo la kwanza ni huhisi maisha yake hayana raha. Anahisi maisha yake yako katika taabu na huzuni, na kisha ataanza kukata tamaa.
Kutokana na hali hiyo, mtu huyo ataanza kumwomba Mungu achukue uhai wake au anaanza kufikiria atafanya nini ili kujiua. Anasema asilimia 80 ya wale wanaojaribu kujiuwa wanachochewa na msongo wa mawazo.
Ushauri kwa wanaofikiria kujiua

Chanzo cha picha, Getty Images
Dkt. Hayatuddeen anasema kuna msaada ambao mtu anaweza kuupata ikiwa anahisi anataka kujiua.
Zipo dawa ambazo mtu anaweza kutumia au ushauri kutoka kwa mtaalamu wa magonjwa ya akili ili apone.
Dkt. Hayatuddeen anaendelea kusema, ni muhimu sana kwa jamii kuelewa kuwa kuna aina tofauti za mfadhaiko au msongo wa mawazo unaoweza kutokea na kumfanya mtu ajaribu kujiua.
Anasisitiza jamii inapaswa kuondoa unyanyapaa na kuwakatisha tamaa watu wanaotaka kujiua, na kuongeza kuwa ugonjwa wa akili unaweza kumpata mtu yeyote, hivyo ikitokea tunapaswa kuwa wawazi na kujua matibabu yapo.












