Hivi ndivyo walivyokuwa wakiishi wanaanga Suni na Butch katika anga za mbali kwa miezi tisa

erf

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Wafanyakazi waliokuwa kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu walituma salamu za Krismasi mwaka jana
    • Author, Tim Dodd
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kupiga kura, kufurahia chakula cha jioni cha Krismasi na kufanya mazoezi katika anga za juu - hayo ni baadhi tu ya mambo ambayo yamewafanya Butch Wilmore na Suni Williams kuwa na shughuli nyingi wakati wa kukaa kwao kwa muda mrefu kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS).

Maisha yalikuwaje kwa wanaanga hao wa Nasa waliokaa maili 250 (400km) juu ya sayari yetu ya dunia? Bila shaka kulikuwa na mambo mengi huko angani ya kuwaweka bize kwa miezi yote tisa. Wamereja salama juma lililopita lakini Maisha yalikuwaje huko anga za mbali kwa mida wote huo?

Suni, 59, na Butch, 62, wamekuwa wakitoa msaada kwa misheni zinazoendelea katika kituo hicho kwa kufanya matengenezo na majaribio, na kufanya matembezi ya angani.

Suni alitoka nje ya kituo hicho katikati ya mwezi wa Januari na mwanaanga mwenzake Nick Hague ili kufanya ukarabati wa chombo hicho. Baadaye mwezi huo, yeye na Butch walitoka nje ya chombo pamoja.

Tafakuri juu ya sayari ya dunia

Butch na Suni wamekubaliana na hali yao huko. Walisema katika mkutano na waandishi wa habari mwezi Septemba kwamba wamefunzwa "kutarajia yasiyotarajiwa."

Kwa hakika wamepata fursa za kutafakari kuhusu maisha ya nyumbani - na kwa kutazama mawio na machweo ya jua.

Kwa vile kituo cha anga za juu huzunguka mara 16 kuipita dunia kila baada ya saa 24 wakati wa kulizunguka jua, maanake kinasafiri na kuona jua likichomoza na kuzama mara 16, na walio ndani huona jua likizama na kuchomoza kila baada ya dakika 45.

Kuishi katika mazingira hayo yanayokupa picha ya kipekee kuhusu dunia, kunakupa nafasi ya kuwa na tafakuri, jambo ambalo Suni amekiri.

"Inafungua mlango wa kukufanya ufikirie tofauti kidogo. Ni sayari moja tuliyo nayo na tunapaswa kuitunza," alisema.

"Kuna watu wengi sana duniani wanaotutumia ujumbe na hilo linakufanya ujisikie uko nyumbani na kila mtu."

Kupiga kura kutoka angani

Butch na Suni na Wamarekani wengine wawili waliokuwa kwenye chombo hicho pamoja nao, Don Pettit na Nick Hague, kila mmoja alipata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi wa Marekani mwaka jana.

"Ni jukumu muhimu sana ambalo tunalo kama raia," Suni alisema kwa waandishi wa habari.

Butch alisema Nasa ilifanya "rahisi sana" kwao kujumuishwa katika uchaguzi.

Ili kuwezesha upigaji kura wao, Kituo cha Kufuatilia Misheni huko Houston kilituma karatasi za kura kupitia barua pepe kwa njia fiche kwenda ISS.

Kisha wanaanga walizijaza na kuzituma kwa satelaiti kwenda kwenye kituo cha ardhini huko New Mexico.

Kutoka hapo, simu za mezani zilitumika kuzituma kura hizo kwenda Kituo cha Udhibiti wa Misheni cha Houston, nao walizituma kwa njia ya kielektroniki kwenda kwa makarani wa kaunti za wanaanga ili kufunguliwa.

Kufanya mazoezi angani

ESDC

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Suni Williams anafanya mazoezi ya kukimbia kwenye kituo cha ISS mwaka 2012

Butch na Suni hufanya mazoezi kwa saa mbili au zaidi kila siku ili kukabiliana na upotevu wa uzito wa mifupa kutokana na kuishi angani.

"Viungo vyako haviumi, na hilo ni jambo nzuri," anasema Butch.

Kuna mashine tatu tofauti za mazoezi ili kusaidia kukabiliana na athari za kuishi katika anga za juu ambako hakuna graviti.

Kifaa cha kisasa cha mazoezi (ARED) kinatumika kufanya mazoezi ya kupiga mchura, kuinua vitu vizito, na vifaa vya kuimarisha misuli ya mgongo. Kwa mashine ya mazoezi ya kukimbia, ni lazima wajifunge kamba ili kujizuia wasielee.

Wakati wa Krismasi

Wakati wa Krismasi, wanaanga kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za juu walichapisha ujumbe wa sherehe wa kuwatakia marafiki na familia zao duniani Krismasi njema.

Timu hiyo ilivalia kofia za Santa, na kupeana maikrofoni ili kuzungumza huku mkebe wa pipi ukielea kuzunguka vichwa vyao. Ilikuwa ni nafasi kwa wafanyakazi hao kufurahia.

Mojawapo ya kazi ya mwisho ya Butch na Suni kwenye timu ya ISS, ilikuwa ni kuwafanya wanaokuja kuchukua nafasi zao wajisikie wako nyumbani.

Tarehe 16 Machi, chombo cha SpaceX kilichobeba wafanyakazi wapya kiliwasili kwenye ISS. Lilikuwa tukio muhimu sana kwa Butch na Suni, kwani lilifungua njia kwao kurudi nyumbani.