Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini watu wasio na wenza 'waseja' hunukia tofauti
- Author, William Park
- Nafasi, Mwandishi wa makala maalum
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kuna hazina kubwa ya taarifa za kisaikolojia na kibaolojia iliyofichwa katika harufu ya miili yetu, lakini kwa sababu fulani tunaichagua kuipuuza.
Mfalme Louis XIV wa Ufaransa alikuwa na shauku kubwa ya manukato.
Maua yaliyokatwa yalipambwa katika kila chumba cha jumba la Versailles, fanicha na chemchemi zilinyunyiziwa manukato, na wageni walimwagiwa manukato kabla ya kuingia ikulu. Iwe ni kwa sababu usafi wake binafsi haukuwa wa viwango tunavyotarajia leo, au kwa sababu alipenda harufu nzuri, Louis alielewa kuwa harufu ina umuhimu mkubwa.
Harufu ya miili yetu inaweza kufichua mambo kuhusu afya zetu, kama uwepo wa magonjwa (kwa mfano, kipindupindu hutoa harufu tamu na kisukari kikali hutoa harufu kama tufaha lililooza).
"Inaweza pia kufichua taarifa kuhusu lishe yetu," anasema Mehmet Mahmut, mwanasaikolojia wa harufu katika Chuo Kikuu cha Macquarie, Australia. "Kuna tafiti chache zenye matokeo yanayokinzana, lakini kundi langu liligundua kuwa kadiri mtu anavyokula nyama zaidi, ndivyo harufu ya mwili wake inavyokuwa ya kupendeza zaidi."
Kwa upande wa mahusiano, harufu pia ina mchango wake. Tafiti zinaonyesha kuwa wanaume huvutiwa zaidi na harufu ya wanawake wakati wa kipindi cha rutuba katika mzunguko wa hedhi, na isiyovutia sana wakati wa hedhi. Hali hii huenda iliwasaidia mababu zetu wa kale kutambua wenza bora wa kuzaa. Vilevile, viwango vya juu vya homoni ya testosteroni kwa wanaume vinaweza kuboresha harufu yao.
Lakini jambo la kuvutia zaidi ni hili: sehemu kubwa ya harufu yetu ya kipekee huamuliwa na vinasaba vyetu.
Harufu ya kila mtu ni ya kipekee kiasi kwamba watu wanaweza kutofautisha fulana zenye jasho za mapacha wanaofanana kabisa.
Hii inaonyesha kuwa jeni zetu zina mchango mkubwa katika namna tunavyonukia
Harufu ya mwili ni ya kipekee kiasi kwamba watu wanaweza kutofautisha fulana zenye jasho za mapacha wanaofanana kabisa miongoni mwa fulana za watu wengine.
Kwa kweli, harufu ya mapacha wanaofanana ni karibu sawa kiasi kwamba wakati mwingine washiriki wa majaribio walichanganya fulana mbili za mtu mmoja wakidhani ni za mapacha wawili.
"Hili ni muhimu kwa sababu linaonyesha kuwa vinasaba vinaathiri jinsi tunavyonukia," anasema Agnieszka Sorokowska, mwanasaikolojia na mtaalamu wa harufu ya binadamu katika Chuo Kikuu cha Wroclaw, Poland. "Hivyo, tunaweza kutambua aina za msimbojeni za watu wengine kwa kuwanusa."
Hata hivyo, katika maisha halisi, mambo si rahisi hivyo. Hata tunavyochagua manukato tunayotumia tunaweza kuakisi mapendeleo yetu ya kijeni.
Sorokowska na wenzake wameonyesha kuwa inawezekana kukadiria baadhi ya sifa za utu wa mtu kulingana na aina ya manukato anayopendelea.
Lakini je, taarifa hii yote iliyomo katika harufu ya mwili wetu ina manufaa gani?
Katika utafiti mmoja, wanawake walipewa fulana zilizovaliwa na wanaume wasiowafahamu na kuombwa kuzipanga kulingana na harufu ilivyokuwa ya kupendeza. Mpangilio wao uliendana na tofauti katika kitu kinachoitwa Human Leukocyte Antigen (HLA).
HLA ni kundi la protini zinazosaidia mfumo wa kinga kutambua seli za mwili na zile za kigeni zinazoweza kusababisha magonjwa. Jeni zinazohusika na HLA (zinazojulikana pia kama MHC) zina mchango muhimu katika uwezo wa mwili kupambana na maambukizi.
Kwa mtazamo wa kijeni, ni faida kupata mtoto na mwenza mwenye wasifu wa HLA tofauti na wako. "Ukiwa na mwenza mwenye tofauti za kijeni katika harufu ya mwili na mfumo wa kinga, watoto wenu watakuwa na kinga bora dhidi ya magonjwa," anasema Sorokowska.
Wanawake katika utafiti huo waliweka juu zaidi fulana za wanaume waliokuwa na HLA tofauti zaidi na yao, na chini zaidi wale waliokuwa na HLA inayofanana. Hivyo, bila kujua, walikuwa wakipendelea wanaume wenye mchanganyiko bora wa kijeni kwa mfumo wa kinga na yote haya yalitokea kwa kiwango cha fahamu fiche.
Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa katika maisha halisi, watu hawaoi au kuolewa kwa kuzingatia harufu pekee. Utafiti wa karibu wanandoa 3,700 uligundua kuwa uwezekano wa mtu kuishia na mwenza mwenye HLA tofauti haukuwa mkubwa kuliko wa bahati nasibu.
Je, huchagua wenza kwasababu ya harufu zao?
Ingawa HLA haiathiri moja kwa moja uchaguzi wa mwenza, inaweza kuathiri ustawi wa ngono katika ndoa. Wanandoa wenye tofauti kubwa ya HLA waliripoti kuridhika zaidi kimapenzi na hamu kubwa ya kupata watoto. Athari hii ilionekana zaidi kwa wanawake.
Kwa wanabiolojia wa mageuzi, msisitizo juu ya uchaguzi wa mwanamke una mantiki. Kiasili, mwanamke ndiye anayebeba na kulea mtoto kwa gharama kubwa zaidi, hivyo huwa makini zaidi katika kuchagua mwenza mwenye ubora mzuri wa kijeni. Ndiyo maana katika viumbe wengi wa asili, madume huonyesha rangi ang'avu, hucheza, huimba au kutoa zawadi ili kuthibitisha ubora wao.
Umaarufu wa wazo la kuchagua mwenza kwa harufu ulipelekea hata kuibuka kwa matukio ya "uchumba wa fulana" na huduma za kutuma harufu kwa posta. Hata hivyo, ushahidi wa kisayansi haujaonyesha wazi kuwa tunafanya maamuzi bora ya kimapenzi kwa kuzingatia harufu.
Mara nyingi, taarifa tunazopata kwa harufu huchanganywa au kupotoshwa na hisia nyingine kama kuona. Kwa mfano, watu wanaweza kukadiria kwa usahihi kiwango cha wasiwasi (neuroticism) wa mtu kwa kunusa harufu yake tu. Lakini wanapoonyeshwa picha ya mtu huyo pamoja na harufu yake, usahihi hupungua.
Anasema kwamba BO ni sahihi zaidi kwa kuhukumu neuroticism, lakini nyuso ni rahisi, na mara nyingi sisi hufanya kile ambacho ni rahisi zaidi.
Utafiti mwingine uligundua kuwa wanawake walio katika ndoa hawakuweka fulana za waume zao katika nafasi ya kwanza kwa harufu ya kupendeza zaidi. Hii inaonyesha kuwa hawakuwachagua waume zao kwa kuzingatia harufu pekee.
Aidha, harufu ya wanaume ambao hawajaoa ilionekana kuwa kali zaidi kuliko ya wanaume waliooa. Hii huenda ikahusiana na viwango vya testosteroni, ambavyo hupungua kadiri mwanaume anavyozeeka au anapoweka kipaumbele kwa familia.
"Iwapo lengo lako pekee ni kupata mwenza mwenye vinasaba bora, basi labda unapaswa kuzingatia harufu yake," anasema Sorokowska. "Lakini kwa watu wengi, hilo si jambo muhimu zaidi."
Mahmut anakubaliana naye: "Umuhimu wa harufu umepungua kwa kiasi fulani. Tumetumia maelfu ya miaka kuficha harufu yetu halisi kwa kutumia manukato na vipodozi."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid