Je, unajua watu huvutiwa na wapenzi kutokana na harufu ya mwili?

    • Author, Novelia Wiley
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Leo hii hebu tafakari kuhusu hili.

Je unaweza kujua umri wa mtu uliyekaa karibu naye kwa kunusa harufu ya mwili wake?

Mtu huyo anaweza kuwa hajajipuliza marashi lakini unaweza kujua umri wake kutokana na harufu ya mwili wake.

Sijaona nadharia hii mitandaoni. Lakini nilijifahamisha kutokana na utafiti niliousoma uliothibitisha jinsi ya kugundua umri wa mtu kutokana na harufu yake ya mwili.

Harufu ya mwili hutofautiana kwa kila binadamu. Lakini hubadilika kadri tunavyoendelea kuishi. Mabadiliko hayo hayaakisi tu mazingira tunayoishi bali pia mwelekeo wetu wa kijamii na kimageuzi.

'Wazazi watajua harufu hiyo'

Wakati wa utotoni, harufu ya mtoto huwa hafifu kutokana na tezi za jasho zisizo na shughuli nyingi na viumbe hai vidogo kwenye ngozi.

Hata hivyo, wazazi wengine wanaweza kugundua harufu ya watoto wao zaidi kuliko watoto wa wenzao. Harufu hii huunda uhusiano mzuri wa kihisia na wa kawaida kati ya wazazi na watoto.

Pia husaidia kupunguza msongo wa mawazo kwa wazazi huku ikijenga hisia za furaha na upendo kwa mtoto. Harufu maalumu inayotokana na watoto wanaokuwa ni ya kuvutia sana.

Hata hivyo akina mama wanaosumbuliwa na unyogovu baada ya kujifungua wakati mwingine hawawezi kunusa harufu ya mwili ya watoto wao.

Kunukia kwa mtoto

Wakati wa kubaleghe, harufu ya mwili hubadilika kila wakati. Mabadiliko hayo yanasababishwa na uzalishaji wa homoni za kijinsia ambazo husisimua tezi za jasho na tezi za mafuta kwenye ngozi. Tezi nyingi za jasho huzalisha maji na chumvi.

Wakati tezi za Apokrini huzalisha protini na mvuke unaohusiana na mafuta. Tezi hizi huzalisha harufu mbalimbali ambazo ni za kipekee kwa kila mtu.

Lipidi na sebum, kemikali ya mafuta inayolainisha nywele, ngozi na ngozi ya kichwa hutolewa kutoka kwa tezi hizi. Hata hivyo, ikichanganyika na bakteria, harufu ya miili yetu hunuka vibaya.

Sawia na jasho la vijana pamoja na harufu za miili yao hubadilika na kutoa harufu mbaya. Wanapobaleghe na kuingia utu uzimani, harufu yao ya mwili inapungua, na hivyo kupunguza uwezo wa wazazi kutambua watoto wao kwa harufu.

Utajuaje harufu yako?

Utoaji wa mafuta katika tezi hizo huongezeka wakati wa kubaleghe.

Ingawa nguvu zake hupungua tunapozeeka, kila mtu tayari ana harufu maalumu ya mwili. Hii inategemea mambo mengi kama vile lishe, msongo wa mawazo, homoni au pia viumbe hai vya ngozi.

Uwezo wa mtu kunusa ni mzuri sana katika kubaini habari kujihusu, hasa ukiwa gizani au mazingira yaliyo na kelele, au wakati ambapo ni vigumu kuona au kusikia kwa urahisi.

Harufu ya mwili husaidia katika kuchagua wapenzi, kutambua jamaa, au kutofautisha jinsia.

Ni kipi hutokea unapozeeka?

Tunapozeeka, ngozi zetu hupoteza unyumbufu na kolajeni. Hii hupunguza shughuli za tezi za jasho na mafuta. Kutokana na upungufu huo inakuwa vigumu kwa wazee kudumisha joto la mwili.

Kuhusu tezi za sebasi, utoaji wao hupungua kadri tunavyozeeka. Muundo wao pia hubadilika. Hii husababisha kupungua kwa viwango vya vitamini E au Squalene ambavyo huzuia uzalishaji zaidi wa oksijeni.

Hii husababisha harufu kwa wazee, ambayo Wajapani huita 'kerisho'.

Hivyo, baada ya umri wa miaka 40, kazi ya baadhi ya asidi za mafuta kwenye ngozi kama vile Omega 7 na asidi ya Palmioleic hubadilika. Hilo hubadilisha harufu ya mwili wa binadamu.

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid