Kundi la Wagner: Linafanya shughuli zake nchi gani na ipi hatima yake nje ya Urusi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukraine, Mali, Sudan, Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya, ushawishi wa Kundi la Wagner unaenea zaidi ya mipaka ya Urusi, ambapo athari za uasi wake dhidi ya Kremlin ni vigumu kutabiri. Hadi hivi karibuni Kundi la Wagner limekuwa la manufaa sana kwa maslahi ya Moscow.
Kundi la mamluki linaloongozwa na Yevgeny Prigozhin limetumika kama jeshi la kivuli la Urusi, likifanya kazi nyingi chafu popote penye maslahi ya Kremlin, pale ambapo haikutaka kutuma askari wake ili kuepuka athari za kisheria au kidiplomasia.
Wagner, kampuni ambayo ni zaidi ya jeshi la kibinafsi, imepata ushawishi wa kisiasa na lango la kutumia rasilimali nyingi za nchi hizo, ambazo zinaruhusu kundi hilo lijifadhili lenyewe.
Nchini Ukraine, ambako limekuwa na jukumu kubwa tangu kutekwa kwa Crimea mwaka 2014 hadi kutekwa kwa Bakhmut mwezi uliopita, Moscow imefungua milango kwa maelfu ya mamluki wa Wagner wanaopigana kwenye mstari wa mbele kujiunga na safu ya jeshi la kawaida.
“Katika nyingi ya nchi hizo, Kundi la Wagner linafanya kazi kwa kwa ajili ya pesa pekee. Na jeshi la Urusi halina nia wala rasilimali za kujihusisha na migogoro hiyo au kujaribu kuzuia Wagner huko”, anasema Profesa Rasmus Nilsson, wa chuo cha Kikuu cha London, wa kitendo cha masomo ya Ulaya Mashariki.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria lilikuwa ndio eneo la kwanza la Kundi la Wagner nje ya Ulaya. Syria pia ni moja ya maeneo machache ambapo wanajeshi wa Magharibi wamepambana na mamluki wa Wagner.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alianza kumsaidia Bashar al Assad mwaka 2015, baada ya jeshi la Syria kuzidiwa mashambulizi ya waasi na vikosi vya Dola la Kiislamu. Mwezi mmoja baadaye, askari wa jeshi la Urusi waliongezewa nguvu na mamluki wa Prigozhin, ambao mwishowe walikuwa zaidi ya wanaume 5,000.
Mnamo mwaka wa 2018, jeshi la Al Assad, likisaidiwa na mamluki wa Urusi, lilishambulia kituo cha kijeshi cha Merika ambacho walikuwa wakipigana na vikosi vya Islamic State. Marekani ilijibu kwa mashambulizi ambayo yanaaminika kuwaua wapiganaji kati ya 200 na 300, wakiwemo wanachama wengi wa Wagner.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mamluki wengi wa Wagner wanaaminika kuondoka Syria na na kujiunga na mapigano nchini Ukraine, ingawa kampuni zinazohusishwa na Wagner zimeshinda kandarasi zenye faida katika maeneo ambayo yaliwahi kudhibitiwa na Dola la Kiislamu. Na wachache wanasemekana wapo Venezuela.
Mnamo 2019, shirika la Reuters liliripoti kwamba mamluki wa Wagner walikwenda Caracas ili kuimarisha usalama wa Rais Nicolás Maduro wakati wa maandamano dhidi ya serikali yalitokea mwanzoni mwa mwaka huo.
Kundi la Wagner pia limeshutumiwa kwa uchimbaji haramu wa madini nchini Venezuela, suala ambalo lilijadiliwa katika bunge la Uingereza mwaka 2022. Ilipoulizwa na bunge, serikali ya Uingereza ilisema inafuatilia kwa ukaribu taarifa kuhusu uwepo wa Mamluki wa Kirusi katika nchi ya Amerika ya Kusini na juu ya shughuli za makampuni ya kimamluki katika eneo la Arco Minero, ambapo uchimbaji haramu wa dhahabu unafanywa.
Hata hivyo, kufuatia uasi wa Wagner Jumamosi iliyopita, serikali ya Maduro iliharakisha kulaani tishio la kigaidi la kundi hilo na kumuunga mkono kikamilifu Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Chanzo cha picha, Getty Images
Uwepo wa Wagner Afrika
Kikundi cha mamluki kinachoongozwa na Yevgeny Prigozhin kina uwepo mkubwa barani Afrika, ambapo wanatoa huduma za usalama, ushauri wa kisiasa au kampeni za kupotosha. Kuanzia Libya kaskazini hadi Afŕika Kusini, shughuli za Wagner zimekuwa zikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Huko Libya, mamluki wa Wagner walijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza mnamo 2019, ambapo walimuunga mkono Jenerali muasi Khalifa Haftar katika mashambulizi yake dhidi ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa huko Tripoli.
Kundi hilo, hata hivyo, linaaminika kuwepo nchini humo tangu 2014, wakati Libya ilipogawanyika pande mbili, na serikali zinazopingana mashariki na magharibi mwa nchi hiyo. Wagner wakati mmoja ilikuwa na wanajeshi 2,000 nchini Libya, ingawa haijulikani ni wanajeshi wangapi bado wapo.
Nchini Sudan, pia eneo la mapigano makali kati ya majenerali wawili hasimu, Wagner ina takribani wapiganaji 500, kulingana na vyombo vya habari vya ndani kama vile The Sudan Tribune. Mamluki wa Urusi waliingia mikononi mwa Omar al Bashir, ambaye alitia saini safu ya makubaliano na Moscow mnamo 2017.
Moja wapo ni makubaliano ya ujenzi wa kituo cha jeshi la majini katika eneo la Port Sudan. Pia makubaliano ya uchimbaji wa dhahabu na kampuni ya M Invest, ambayo, kulingana na Merikani, ni kampuni tanzu ya Kundi la Wagner.
Ingawa Sudan haijakiri uwepo wa kwa mamluki hao nchini humo, picha mbalimbali zilizochapishwa kwenye mtandao wa Telegram zinaonesha kundi hilo. Ingawa picha hizo hazikuweza kuthibitishwa na BBC. Zinaonesha wanajeshi wa Wagner wakiwafunza wanajeshi wa Sudan au kusaidia vikosi vya usalama kuvunja maandamano.
Nchini Mali, wanajeshi wa Kundi la Wagner wamekuwa wakifanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja, ingawa mamlaka ya nchi hiyo haijathibitisha rasmi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdulaye Diop, ameweka wazi kwamba hawana haja ya kujitetea: "Urusi iko hapa kwa ombi la Mali na inajibu ipasavyo mahitaji yetu ya kimkakati," alisema mwaka jana.
Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Mali, ulikuwa hadi hivi karibuni mshirika wa kimkakati wa Mali, ikiwa ni pamoja na kupeleka maelfu ya wanajeshi wa Ufaransa kusaidia wanajeshi wa Mali kupambana na waasi wa Kiislamu ambao walikuwa wamechukua udhibiti wa eneo la kaskazini.
Lakini ushirikiano huu haukuzaa matunda, chuki dhidi ya Ufaransa iliongezeka nchini humo na Paris ililazimika kuondoa wanajeshi wake mnamo 2022, na nafasi yake imechukuliwa na mamluki wa Wagner.
Hali kama hiyo imejitokeza nchini Burkina Faso, ambapo serikali inakanusha uwepo wa wapiganaji wa Wagner. Kulingana na Ouagadougou, ushirikiano na Moscow unahusisha tu mafunzo ya kijeshi kwa silaha ambazo zimenunuliwa kutoka Urusi.
Hata hivyo, ujasusi wa Marekani ulieleza mwanzoni mwa mwaka huu kwamba kundi la Wagner lilikuwa kwenye mazungumzo na serikali ya Burkinabe ili kupeleka wanajeshi.
Wanajeshi wa Wagner wanaelezwa pia kuwepo Chad, kulingana na vyanzo mbalimbali vya Afrika, Ulaya na Marekani. Chad inatawala nafasi ya kimkakati katikati mwa Sahel, ikiwa na mipaka iliyo wazi na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya na Sudan, ambapo mamluki wake wanafanya kazi.
Wagner aliripotiwa kutoa msaada wa vifaa na uendeshaji kwa waasi wa ndani ambao wanatafuta kuvuruga na pengine kupindua serikali ya mpito inayoongozwa na Mahamat Idriss Déby.
Pia wapo Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako Ufaransa iliondoa wanajeshi wake mwaka 2017 baada ya miaka mingi ya uingiliaji kati na kushindwa kusaidia Bangui katika eneo la maendeleo, utulivu, usalama na maendeleo ya kiuchumi.
Kundi la Wagner tangu wakati huo limechukua nafasi ya Ufaransa, ambapo limesaidia kuunganisha serikali ya Faustin-Archange Touadéra na kuzuia kusonga mbele kwa vikundi vya waasi vilivyoanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo 2013.
Kundi la Wagner ndio mwakilishi muhimu zaidi wa Urusi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, hutoa usalama kwa serikali, kuwezesha ushawishi wa kisiasa na kidiplomasia wa Urusi na kupata rasilimali kubwa ya madini," anaelezea Paul Stronski, mtafiti mkuu katika Mfuko wa Carnegie.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatima ya Prigozhin
Sehemu kubwa ya huduma zinazotolewa na Kundi la Wagner katika nchi hizi zitaendelea kuhitajika. Shughuli zake mara nyingi zimeambatana na shutuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, na ripoti ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa ilionya kuhusu uhalifu wa kivita unaoweza kufanywa na mamluki wa Prigozhin nchini Mali.
Kufuatia uasi wa hivi karibuni, Rais wa Belarus Alexander Lukashenko alifanikisha makubaliano kati ya Progozhin na Kremlin kumruhusu kiongozi wa Wagner kwenda uhamishoni Belarus.
"Lukashenko atakuwa na hamu kubwa ya kumweka salama ili kuweka ishara njema na Warusi," anasema Rasmus Nilsson.
Swali la muhimu sasa, anasema profesa Nilsson, ni kipi kifuatacho kwa Yevgeny Prigozhin: "Je, atanyamaza huko Belarusi au, kama wengine wanavyosema, atakwenda Afrika kuwa mbabe wa vita huko?”
Kuhusu wanajeshi wake, Nilsson anaamini baadhi yao waliotumwa Ukraine na Urusi wataishia kujiunga na jeshi la Urusi.
“Kuna watakaoamua kwenda katika tawi moja la Wagner barani Afrika, kwa mfano, au kundi lingine. Kuna mashirika mengi duniani ambayo yanatafuta mamluki,” anahitimisha profesa Nilsson.












