Vita vya Ukraine: Urusi yatekeleza shambulizi na kuua watu 22 Ukraine

Nyumba ya makazi pia iliharibiwa katika shambulio la Chaplyne

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Nyumba ya makazi pia iliharibiwa katika shambulio la Chaplyne

Shambulizi la roketi la Urusi kwenye kituo cha treni cha Ukraine limeua watu 22, Ukraine inasema, katika siku ya kuadhimisha miezi sita tangu uvamizi wa Moscow kuanza.

Inasema waathiriwa watano wa shambulio hilo katika mji wa mashariki wa Chaplyne waliteketea hadi kufa wakiwa ndani ya gari.

Mvulana mwenye umri wa miaka 11 pia aliuawa.

Rais Volodymyr Zelensky alitangaza shambulizi hilo katikati ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Alisema takriban watu 50 walijeruhiwa.

Urusi hadi sasa haijatoa maoni yoyote.

Imekanusha mara kwa mara kulenga miundombinu ya kiraia.

Bw Zelensky alisema alifahamu kuhusu shambulizi la Chaplyne, katika eneo la Dnipropetrovsk, alipokuwa akijiandaa kuzungumza na Baraza la Usalama, na kuongeza: ‘’Hivi ndivyo Urusi ilivyojiandaa kwa mkutano wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa’’.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

“Mabehewa manne ya abiria yanateketea kwa moto sasa hivi...idadi ya vifo inaweza kuongezeka,” alisema.

Mnamo Aprili, shambulizi la kwenye kituo kingine cha gari moshi liliua zaidi ya watu 50.

Ukraine imetumia Jumatano kuadhimisha siku yake ya kila mwaka ya uhuru na Bw Zelensky alikuwa awali amesema Urusi inaweza kufanya kitu ‘’kinyama’’ kuvuruga sherehe hizo.

Hapo awali alishutumu vikosi vya Moscow kwa kugeuza kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kuwa ‘eneo la vita’ ambalo lilihatarisha mtambo huo na watu wa Uropa na kuiweka ulimwengu ‘ukingoni mwa janga la mionzi’.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliambia mkutano huo huo kwamba ‘vita visivyo na maana’ vinaweza kusukuma mamilioni ya watu katika umaskini uliokithiri, nchini Ukraine na kwingineko.

Ulimwenguni kote, kulikuwa na mikusanyiko ya wafuasi mitaani kuashiria uhuru wa Ukraine.

Viongozi wa dunia pia walikusanyika kuunga mkono taifa hilo lililozorota kuadhimisha hafla hiyo.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alionekana mjini Kyiv katika safari ambayo haikutangazwa ili kuonyesha uungaji mkono wa nchi yake, na kutangaza £54m ($63.5m) kama msaada mpya wa kijeshi - kiasi ambacho kilipunguzwa na tangazo la Rais wa Marekani Joe Biden la nyongeza ya $3bn (£2.5bn).

Ujumbe wa usaidizi ulifika kutoka kote ulimwenguni: kutoka Australia, Ujerumani, Finland, Poland, Uturuki na zaidi.

Akiwa Vatican, Papa Francis alitoa wito wa ‘hatua madhubuti’’ kukomesha vita na kuepusha hatari ya maafa ya nyuklia katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia - kikubwa zaidi barani Ulaya.

Lakini katika mitaa ya Kyiv, kulikuwa na utulivu.

Soma zaidi:
Rais Zelensky alisema Urusi imehatarisha kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, na watu wa Ulaya

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais Zelensky alisema Urusi imehatarisha kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, na watu wa Ulaya

Ukraine ilikuwa imepiga marufuku mikusanyiko na matukio makubwa kutokana na hofu kwamba Urusi inaweza kulenga mikusanyiko kama hiyo ya raia.

Ilifuata onyo kutoka kwa Marekani kwa raia wake yeyote kuondoka kabla ya maadhimisho.

Baadhi yao walikusanyika kwenye Mtaa wa Khreshchatyk ili kutazama safu ya mizinga ya Urusi iliyokamatwa na magari ya kivita yaliyowekwa kwenye maonyesho badala ya gwaride la kawaida la Ukraine.

Kati ya hotuba zake za kisiasa, Rais Zelensky na mkewe pia walihudhuria sherehe ya kumbukumbu ya wanajeshi na raia walioanguka vitani, wakiweka maua ya manjano na bluu kwenye Ukuta wa Kumbukumbu ya Watetezi Waliouawa Kyiv.

Mapema wiki hii, maafisa wa Ukraine walitoa taarifa za kwanza kuhusu visababishi vya kijeshi katika muda fulani - wakisema kuwa karibu wanajeshi 9,000 waliuawa katika mzozo huo wa miezi sita, ingawa idadi hiyo haiwezi kuthibitishwa kivyake.

Licha ya hasara, kiongozi huyo wa Ukraine alianza siku kwa hotuba ya kitaifa ya dharau, na kuapa kutwaa tena Ukrainia yote, ‘’bila makubaliano yoyote au maafikiano’’.

‘’Hatujui maneno haya - yaliharibiwa na makombora mnamo 24 Februari,’’ alisema.

Wakati huo huo, huko Urusi, siku ya kuadhimisha nusu mwaka tangu kuanza kwa uvamizi huo ilipita kimya kimya.

Tukio moja muhimu nchini Urusi Jumatano lilikuwa kukamatwa kwa Yevgeny Roizman - mmoja wa wanasiasa wa mwisho waliobaki wa upinzani nchini humo.

Meya huyo wa zamani wa Yekaterinburg alikamatwa kwa tuhuma za ‘’kulidharau jeshi la Urusi’’, ambalo tangu uvamizi wa Ukraine uanze linaweza kubeba kifungo cha hadi miaka mitano.

Alipokuwa akitolewa, alisema alikuwa anakamatwa kwa kusema kwa sauti neno moja, ‘’uvamizi wa Ukraine’’.

Maelfu ya watu wamefikishwa mahakamani kutokana na mashtaka kama hayo, huku wengi wao wakipatikana na hatia, wanasema wanasheria wa haki za binadamu.

Kundi moja la kutetea haki za binadamu, OVD-Info, linasema zaidi ya watu 16,000 wamezuiliwa kwa kupinga uvamizi huo - makosa ambayo ni pamoja na maandamano ya mitaani, mitandao ya kijamii, au kurejelea tu ‘’operesheni maalum ya kijeshi’’ ya Urusi kama vita au uvamizi.