Kwa nini kuporomoka kwa ANC ni ishara mbaya kwa vyama vya ukombozi Afrika?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Danai Nesta Kupemba
- Nafasi, BBC
Chama kikongwe zaidi cha ukombozi barani Afrika kiko taabani na huenda kikapotea kama vyama vingine vya aina hiyo barani Afrika.
Chama cha African National Congress (ANC) - kilichoanzishwa nchini Afrika Kusini zaidi ya karne moja iliyopita - kimepoteza wingi wake wa viti bungeni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, ingawa bado kinasalia kuwa chama maarufu zaidi nchini humo.
Idadi kubwa ya wapiga kura hawakuwa tayari kukipa kura za kutosha chama cha Nelson Mandela, kilichoongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Jambo kama hilo limetokea kwa vyama vingine vilivyopigana na utawala wa kikoloni na kushika madaraka, ambavyo vimeingia kwenye kashfa za ufisadi na upendeleo miongoni mwa watu wachache wa karibu na kuwakasirisha raia wenye njaa ya mabadiliko.
End of Pia unaweza kusoma
Kifo cha vyama vya ukombozi

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Baadhi ya vyama vya ukombozi ambavyo vimesalia madarakani kusini mwa Afrika vinashutumiwa kubaki madarakani kwa kuiba kura.
"Ni jambo lisiloepukika kwamba watu wanataka mabadiliko," anasema mtafiti David Soler Crespo, ambaye ameandika kuhusu kifo cha polepole cha harakati za ukombozi.
"Haiwezekani chama kimoja kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia kwa miaka 100."
Harakati zilizofanikiwa zikitoka kutoka msituni hadi ofisini, zilijipigia debe kuwa wao pekee ndiyo wanaweza kuiongoza nchi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waliingiza mavuguvugu hayo ndani ya vinasaba vya nchi, na hivyo kuifanya iwe vigumu kutenganisha chama na serikali.
Nchini Namibia, maneno "Swapo ni taifa, na taifa ni Swapo" yaliyotumiwa wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini, bado yana nguvu.
Ukiangalia katika eneo zima, watumishi wa umma na walioteuliwa na serikali, hasa katika vikosi vya usalama na vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali mara nyingi walikuwa wapiganaji wa msituni, ambao huweka kipaumbele cha utiifu kwa chama kuliko taifa.
"Hakuna mstari wa kutenganisha kati ya serikali na chama. Si kwamba ni chama, ni mfumo pia," anasema Crespo.
Na urithi wa ukombozi umeingizwa sana katika tamaduni za eneo hilo, huku hadithi za mapambano zikielezwa kwenye meza za chakula cha jioni cha familia na vyombo vya habari vya kitaifa vikiendelea kuwakumbusha wananchi juu ya uhuru wao ulivyopatikana kwa tabu.
Nyimbo za ukombozi na sauti za wakati wa vita huimbwa katika shule, na hata kwenye michezo.
Kwa wananchi kuhama chama cha ukombozi ni tatizo kubwa la kisaikolojia. Lakini baada ya muda hilo hutokea.
"Watu hawaathiriki tena na historia wanapopiga kura," mtaalamu wa siasa ya kijamii kutoka Namibia, Ndumba Kamwanyah ameiambia BBC, akitafakari juu ya kupungua uungwaji mkono kwa Swapo, ambayo imekuwa madarakani tangu 1990.
Vyama vingi viliunga mkono itikadi za ujamaa, lakini mara nyingi hizi itikadi zimeporomoka baada ya muda na watu wamekuwa wakihoji iwapo wananchi wananufaika kwa usawa.
Mifano Hai

Chanzo cha picha, AFP
Moja ya vuguvugu la kwanza la kupigania uhuru kusini mwa Afrika kupoteza ushawishi ni Chama cha United National Independence Party (Unip) cha Zambia, ambacho kiliingia madarakani mwaka 1964 baada ya kumalizika utawala wa Uingereza.
Miaka ya 1970 na 1980 kilitawala nchi kama chama pekee kisheria, na mwanzilishi wake Kenneth Kaunda akishika usukani.
Lakini kutoridhika kwa wananchi kuliongezeka na mwaka 1990 kukawa na maandamano mabaya katika mji mkuu, Lusaka, na jaribio la mapinduzi.
Mwaka uliofuata, uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi baada ya zaidi ya miongo miwili ulishuhudia Rais Kaunda akishindwa na Frederick Chiluba. Chama cha Unip, ambacho wakati fulani kilikuwa na nguvu zote, sasa kimetoweka.
Vyama vya ukombozi nchini Angola, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe vimesalia madarakani lakini vyote vimeshuhudia kupungua uungwaji mkono katika uchaguzi mkuu.
Mwaka 2019 nchini Namibia, chama cha Swapo kilipoteza wingi wa wabunge wa thuluthi mbili.
Katika uchaguzi wa urais, Hage Geingob pia alipoteza umaarufu kwani kura zake zilishuka kutoka 87% mwaka 2014 hadi 56%.
Mwaka uliofuata, Swapo ilipata pigo la kihistoria katika chaguzi wa kikanda na serikali za mitaa.
Profesa Kamwanyah, ambaye alikipigia kampeni chama hicho kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, anasema anaheshimu yale ambayo serikali ya ukombozi ilifanikisha kuyafanya siku za nyuma, lakini anasikitishwa na hali halisi ya sasa.
"Kinachofanywa na chama hicho kwa sasa, hakiakisi maadili ya awali yaliyowafanya watu kufa kwa ajili ya nchi hii," msomi huyo wa Namibia anasema.
Namibia itafanya uchaguzi wake mkuu Novemba 2024 na kuna uvumi kwamba chama hicho kinaweza kukumbwa na hatima sawa na ANC.
"Nafikiri Swapo itashinda, lakini hawatapata wingi wa kura bungeni," anasema Prof Kamwanyah.
Ndiilokelwa Nthengwe, mwanaharakati wa Namibia mwenye umri wa miaka 26, anasema kumekuwa na mabadiliko ya kizazi.
Bi Nthengwe amekuwa mstari wa mbele katika harakati nyingi za kijamii nchini humo. Vijana wanathamini usawa wa kijinsia, anasema, pamoja na kazi na huduma bora za afya.
"Kile ambacho vijana wanataka ni mabadiliko, mabadiliko na mabadiliko zaidi."
Kutawala kwa mbinu chafu

Chanzo cha picha, AFP
Namibia, pamoja na Afrika Kusini, zinaonekana kuwa na demokrasia iliyo wazi, vyama tawala nchini Zimbabwe, Angola na Msumbiji vimeshutumiwa kwa kuzima upinzani ili kuendelea kushikilia madaraka.
Udanganyifu katika uchaguzi, kukandamiza vyama vya upinzani na vitisho kwa wapiga kura ni miongoni mwa mbinu zao wanazotuhumiwa kuzitumia.
Adriano Nuvunga, mwenyekiti wa jopo la Southern Defenders Observer Mission, amefuatilia uchaguzi nchini Msumbiji kwa miongo miwili iliyopita.
"Mara zote uchaguzi ambao nimekuwa mwangalizi tangu 1999 umekuwa na udanganyifu," anasema Nuvunga.
Anasema pia aliona vitisho kwa wapiga kura na kuvuruga kura.
Nchini Zimbabwe mwaka 2008 Amnesty International ilieleza juu ya mauaji ya kiholela, mateso na unyanyasaji dhidi ya wafuasi wa upinzani kati ya duru ya kwanza na ya pili ya kura za urais.
Kwa hakika uchaguzi mara nyingi nchini Zimbabwe umekumbwa na madai ya wizi au vitisho dhidi ya upinzani, ingawa haya mara zote hukanushwa na chama tawala, Zanu-PF.
Kufuatia uchaguzi wa 2022 nchini Angola, maelfu ya watu waliingia barabarani kuandamana dhidi ya madai ya udanganyifu katika uchaguzi.
Kadiri vyama vya ukombozi vinavyozidi kukaa madarakani ndivyo vinavyozidi kushutumiwa kwa ufisadi na upendeleo na kutotawala kwa maslahi ya wananchi.
Hayati Chris Hani, shujaa wa kupinga ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, aliliona hili mapema aliposema: “Ninachohofia ni kwamba wakombozi wanaibuka kama waendesha magari ya Mercedes Benzes na kutumia rasilimali za nchi kuishi kwenye majumba na kujikusanyia mali.”
Kupindua utawala wa kikoloni na wa wazungu wachache ilikuwa kazi ngumu, lakini utawala mpya umeleta changamoto nyingine.
Crespo anasema ikiwa vyama hivi vitarejesha maadili yaliyowaleta serikalini, kuwasikiliza vijana na kujitambua tena, wanaweza kubaki madarakani kwa muda mrefu zaidi.
Imetafsiriwa na Rashidi Abdalla na kuhaririwa na Floriana Kaijage












