Ni kina nani wanaoongoza upinzani Iran?

Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwanaharakati wa haki za binadamu, gwiji wa soka na mwanamfalme. Mume mwenye huzuni, mwanaharakati wa wanawake na mwigizaji wa Hollywood. Kundi hili la watu tofauti limebeba matumaini na ndoto za Wairani wengi ndani na nje ya nchi.

Waandamanaji wanataka waungane na kuunda muungano ambapo makasisi wangeondolewa mamlakani. Maandamano hayo yalichochewa na kifo cha Mahsa Amini akiwa chini ya ulinzi wa polisi mwezi Septemba. Alizuiliwa kwa madai ya kutovaa hijabu yake 'vizuri'.

Takriban watu 500 wameuawa katika maandamano ya mitaani na karibu 20,000 wako jela. Lakini licha ya maombi mengi, upinzani haujaungana. Walakini, wataalam wengine wa kisiasa wanaona kutokuwepo kwa muundo wa umoja ni nguvu kuwa kwa sasa.

"Kwa sababu hii ni vuguvugu la ugatuzi, la kisasa, serikali haiwezi kuizima kwa kuua au kukamata uongozi," anasema Mohammad Barzanjeh, mchambuzi wa kisiasa anayeishi London, Kanada. "Lakini wakati vuguvugu likiendelea, itahitaji uongozi wa kisiasa kufafanua mkakati huo, wakati kauli mbiu zitahitaji kutetea jambo fulani badala ya kupinga jambo fulani." Anaongeza kuwa 'Mwanamke, Maisha, Uhuru' ndiyo kauli mbiu pekee chanya ya kupinga inayotumika hadi sasa.

Kuswekwa ndani nchini Iran

Kiongozi wa mwisho wa upinzani kupinga kuanzishwa kwa makasisi ndani ya Iran alikuwa Mir Hossein Mousavi, mgombea urais katika uchaguzi wa 2009. Amekuwa chini ya kizuizi cha nyumbani tangu wakati huo na sasa ni dhaifu sana.

Iran

Chanzo cha picha, Majid Saeedi

Maelezo ya picha, Waziri mkuu wa zamani na mgombea urais ambaye alijaribu kubadilisha utawala akiwa ndani ya utawala

Harakati iliyitwa 'Green Movement' ilitokana na uchaguzi huu ambapo mamilioni waliingia barabarani kuandamana kwa amani kupinga kile wanachosema kuwa kura iliyoibiwa ili kumchagua tena kiongozi wao mwenye msimamo mkali, Rais Mahmoud Ahmadinejad.

Kwa miaka mingi, wengi wa wanamageuzi wanaokosoa mfumo huo wamefungwa jela au kutengwa. Na wengi wao wamepoteza uaminifu miongoni mwa idadi ya vijana waliokatishwa tamaa baada ya miongo kadhaa ya kuvunjwa kwa ahadi na uchumi unaoyumba.

Wafungwa mashuhuri wa kisiasa Narges Mohammadi na Nasrin Sotoudeh wana nafasi nzuri ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa waandamanaji lakini huenda wasiweze kupata uungwaji mkono wa kutosha kwa nafasi ya uongozi.

Nargis

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Narges Mohammadi anazuiliwa katika gereza maarufu la Evin nchini Iran

Wote wawili wanatambulika duniani kote kwa kazi yao ya kutetea haki za binadamu ndani ya Iran. Narges Mohammadi amekuwa akiteswa na mamlaka kwa kupinga hukumu ya kifo. Wakati huo huo, wakili wa haki za binadamu Nasrin Sotoudeh anapinga uvaaji wa hijabu wa lazima. Amekuwa chini ya kifungo na amezuiwa kufanya kujishughulisha na masual ya sheria au kuondoka nje ya nchi.

Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nasrin Sotoudeh, anayeonekana hapa katikati, ni mwanasheria wa haki za binadamu ambaye amekuwa mwiba kwa utawala wa Iran.

Kutokana na ukandamizaji ambao watu ndani ya Iran wanastahimili, wengi wanawashutumu wanasiasa walio uhamishoni kwa kuwahimiza watu kuhatarisha maisha yao wakipigana na utawala wa kikatili huku wao wenyewe wakiishi kwa usalama nje ya nchi.

Viongozi wa upinzani ng'ambo hadi sasa wamejizuia kutoa wito kwa Wairani ndani ya nchi kujitokeza barabarani lakini huwasifu baadaye. Na ingawa vuguvugu la sasa la maandamano limeenea, halijaona mamilioni ya watu wakiingia mitaani kama mwaka wa 2009.

"Ili kuleta mabadiliko, maandamano ya mitaani yanahitaji kufikia umati mkubwa na hii haiwezi kutokea kama watu nje ya 'Generation Z' wanatarajiwa kutoa changamoto kwa vikosi vya usalama," anasema Barzanjeh.

Wahamiaji wanaoishi nje ya nchi

Reza Pahlavi amekuwa mtu wa mara kwa mara katika mazingira ya upinzani nchini Iran ambapo anawakilisha ile hali ya kutamani enzi ya kabla ya mapinduzi. Akiwa mtoto wa mfalme, aliapa kupitia katiba iliyofutwa baada ya kifo cha baba yake kwamba angesimia vazi hilo.

Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Reza Pahlavi

Alipata umaarufu baada ya baadhi ya waandamanaji vijana katika maandamano ya 2018 kushuhudiwa wakiimba jina lake na kutaka arejeshwe Iran. Lakini kusita kwa Reza Pahlavi kuchukua jukumu kubwa zaidi na ikiwemo kugombea kumewakatisha tamaa wafuasi wake wengi.

Kwa kadiri Baraza la Kitaifa la Upinzani, linalojulikana zaidi kama MEK, linavyohusika, rais wa baadaye wa Iran alichaguliwa muda mrefu uliopita. Jina lake ni Maryam Rajavi. Yeye ni mwenza wa zamani aliyegeuka mke wa aliyekuwa kiongozi wa MEK, Massoud Rajavi.

Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maryam Rajavi anaongoza moja ya taasisi tata ya upinzani nchini Iran

Rajavi anaongoza shirika ambalo linachukuliwa kuwa na msingi bora na wenye nidhamu wa wafuasi. Wanajulikana na wakosoaji kama 'ibada' lakini wana pesa za kutosha kulipia wanasiasa mashuhuri wa Magharibi kutoa hotuba na kumpamba Rajavi kwenye mikusanyiko.

MEK inasisitiza kuwa ina wahudumu wa chinichini ndani ya Iran. Lakini watu wengi bado wanachukizwa na kitendo cha shirika hilo kuasi Iraq wakati wa vita vyake na Iran katika miaka ya 1980.

Hadi hivi majuzi, MEK ilikuwa kwenye orodha ya Idara ya Jimbo la Marekani ya mashirika ya kigaidi.

Kiongozi anayetarajiwa wa upinzani aliye na simulizi rahisi zaidi ni Mwanasoka Bora wa Mwaka wa 2004 wa Asia, Ali Karimi. Yeye ni mtu maarufu ambaye amevutia mioyo ya watu kwa uungaji mkono wake thabiti wa maandamano.

Iran

Chanzo cha picha, Gallo Images

Maelezo ya picha, Mwanasoka anayeunga mkono maandamano ya mtaani Iran

Karimi sasa anaishi Dubai na huwasiliana na watu zaidi kupitia ukurasa wake wa Instagram na akaunti ya Twitter. Wengi wa wafuasi wake wangependa kumuona akichukua nafasi ya uongozi lakini wakosoaji wanaamini kwamba hana haiba na utaalamu wa kisiasa unaohitajika kuongoza vuguvugu hilo pana.

Matukio yasiyofikirika yalimfanya Hamed Esmaeilion kufahamika zaidi kwenye umma. Kutunguliwa kwa ndege ya abiria ya Ukraine (PS752) na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) mnamo Januari 2020 ni moja ya matukio ya kusikitisha zaidi katika historia ya hivi karibuni ya Iran.

Daktari wa meno alipoteza mke na binti yake kwenye ndege hiyo, na amebadilika kutoka kwa baba na mume wenye huzuni, na kuwa mtu wa upinzani mkali.

Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hamed, mwanaharakati asiyekuwa na uhusiano kisiasa

Lakini anakataa kuwania uongozi au hata kuwa mwanaharakati wa kisiasa, akisema anapendelea kujulikana kama mwanaharakati wa kijamii. Ameweza kuwashawishi makumi kwa maelfu ya Wairani wa kigeni kote ulimwenguni kuhudhuria mikutano ya kupinga serikali.

Daktari huyo wa meno ana nafasi ya kipekee miongoni mwa waandamanaji kutokana na chuki yake kubwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kutojihusisha na siasa zinazohusishwa na watu wengine wa upinzani wanaoishi nje ya nchi.

Masih Alinejad alikuwa mwandishi wa habari anayeunga mkono mageuzi nchini Iran. Baada ya kuondoka nchini humo, alianza kufanya kampeni dhidi ya hijab ya lazima, akiunga mkono video nyingi za wanawake wakinyanyaswa na polisi wa maadili.

Anaweza kupewa sifa kwa kuanzisha cheche za kwanza za upinzani uliopangwa wa kiraia ndani ya Iran.

Iran

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Masih Alinejad alikuwa mwandishi wa habari kabla ya kuwa mwanaharakati

Lakini picha inayomuonyesha akiwa amesimama karibu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo mwaka 2019, huku akitoa wito kwa utawala wa Trump kutolegeza vikwazo dhidi ya Iran wakati wa janga la coronavirus, ilizua utata.

FBI baadaye ilitibua kile wachunguzi wanasema ni njama ya serikali ya Iran ya kumteka nyara. Mwanzoni mwa maandamano ya sasa, alitoa wito kwa raia wa Irani kuvamia balozi za Irani nje ya nchi. Alinejad baadaye alifuta tweet hii na kukosoa utawala wa Biden kwa kuwa mpole sana dhidi ya Iran.

Iran

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kutoka muigizaji wa Hollywood mpaka mwanaharakati wa haki za binadamu

Lakini wakati Marekani ilipoandaa kikao maalum cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Iran, hakualikwa kuhudhuria.

Mwigizaji wa Hollywood na kipenzi cha zamani cha gazeti la udaku ambaye alisomea udaktari anapewa kipaumbele.

Nazanin Boniadi ni mwanaharakati wa haki za binadamu ambaye ametembelea nchi yake mara moja tu katika maisha yake ya utu uzima. Yeye hajajikita kisiasa sana jambo ambalo linamfanya kupendwa na Wairani wengi lakini kutambuliwa kwa jina ndani ya nchi kunaweza kuwa kikwazo chake kikubwa kwa sasa.

Hatua zinazofuata

Katika kuonyesha mshikamano ambaoo halijawahi kushuhudiwa, viongozi wote walioko uhamishoni walituma ujumbe mmoja unaofanana wa Mwaka Mpya. "Mwaka wa 2022 ulionyesha utukufu wa mshikamano wa Wairani," ulisomeka. "Mwaka 2023 utakuwa mwaka wa ushindi, uhuru na haki."

Haijulikani ikiwa viongozi wa upinzani ndani ya Iran hawakutaka kurudia kauli hiyo au hawakuweza kufanya hivyo. Ishara ya jinsi ilivyo ngumu kupima hali ya ndani ya nchi. Mashirika pekee ambayo yanaendelea kuleta watu wao mitaani ni makundi ya kisiasa ya Kikurdi.

"Tofauti na upinzani wa kitaifa ulio uhamishoni, vikundi vya Wakurdi vimekita mizizi ndani ya Wakurdi wa Iran na vinaweza kutumika kama mfano wa vyama vya kisiasa," anasema Barzanjeh.

Labda haishangazi kwa kuwa Masih Amini alikuwa Mkurdi kwamba watu wachache wa Iran wasiojiweza wanazuia moto wa maandamano.