'Nilikwenda Saudi Arabia kushinda mataji, sio pesa' - Edouard Mendy

    • Author, Nizaar Kinsella & Babacar Faye
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Kipa wa Senegal, Edouard Mendy anaamini kwamba ukosoaji dhidi yake na wanasoka wengine kwamba walikimbilia Saudi Arabia kwa sababu ya pesa sio sahihi.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alihamia Al-Ahli kutoka Chelsea mwaka 2023 kwa uhamisho wa pauni milioni 16 ($21.4 milioni) na mwezi Mei, mshindi huyo wa Kombe la Mataifa ya Afrika aliisaidia klabu yake ya Saudia kushinda Ligi ya Mabingwa Asia, na kuwa mmoja wa wachezaji wa kwanza kushinda taji hilo na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini, kama wengine wengi, Mendy amekosolewa kwa kuchezea pesa badala ya heshima katika Ligi mpya na tajiri ya Saudia.

Alipoulizwa kuhusu ukosoaji huo katika mahojiano na BBC, Mendy amesema: "Kama nilivyosema hapo awali, mradi wa Al-Ahli ulipokuja, ulinifanya nijisikie nina jukumu muhimu. Miaka miwili baadaye, tulishinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu. Kwa hivyo, hilo linahalalisha chaguo langu. Na ninatumai miaka ijayo litahalalishika zaidi."

Aliongeza: "Baadhi ya watu wanakimbilia kwenye hitimisho na kusema, sababu pekee ni pesa. Nimekuwa nikisema tangu mwanzo, nilipoondoka Chelsea, nilijua najiunga na timu nyingine ambayo ningeweza kushinda kila kitu, ushindi ambao haukuwezekana tena Chelsea."

Tangu wakati huo The Blues wameshinda Ligi ya Conference Ulaya, mashindano ya vilabu vya daraja la tatu barani Ulaya, chini ya usimamizi mpya wa Todd Boehly na Clearlake Capital.

Lakini ushindi huo unakuja baada ya miaka miwili bila taji, miaka ambayo iliwakatisha tamaa baadhi ya mashabiki baada ya mafanikio yaliyopatikana chini ya Roman Abramovich katika miaka 19 iliyopita.

Mendy pia alisherehekea kile alichoelezea kama "ushindi wa kihistoria" na Senegal dhidi ya Uingereza kwenye Uwanja wa Jiji la Nottingham Forest, na siku chache kabla alikuwa Dakar na kupata ushindi mwingine tofauti.

Pia unaweza kusoma

Nje ya Soka

Yeye ndiye mlezi wa Shule ya Yakaar, huko Keur Massar, ambayo inalenga kuwezesha ufadhili wa vifaa vya kujifunzia vya kidijitali kwa watoto wa eneo hilo ambao ni masikini.

Kama inavyojulikana, Mendy alikulia Ufaransa, akiwa na umri wa miaka 22, hakuwa na kazi, akipambana kupata klabu, wakati wanafamilia wake wakiishi katika viunga vya Dakar.

Hii ndiyo sababu neno 'Yakaar,' ambalo linamaanisha 'tumaini', lilichaguliwa, neno ambalo Mendy amekuwa akilibeba katika maisha yake yote.

“Kwa kweli, tumaini ndio neno linalofafanua kazi yangu vizuri zaidi,” anasema.

Mendy pia aliulizwa ikiwa kuwa golikipa kutoka Afrika ni jukumu zito.

"Bila shaka. Nilipokuwa Uingereza, hakukuwa na makipa wengi Waafrika kwenye vilabu vikubwa.”

"Iwe katika kiwango cha kitaifa au kimataifa. Ni sawa kwa makipa wengine wa Afrika kama André Onana (Manchester United) au Yassine Bounou (Al-Hilal)."

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah