'Siwezi kulala': Mauaji ya mwanariadha yanaashiria nini kuhusu usalama wa wanawake nchini Kenya

Muda wa kusoma: Dakika 6

Mauaji ya mwanariadha Rebecca Cheptegei na mpenzi wake wa zamani yamezidisha wito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya mauaji ya wanawake nchini Kenya.

Raia huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 33 alifariki siku chache baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mpenzi wake wa zamani nyumbani kwake katika kaunti ya Trans Nzoia magharibi mwa Kenya.

Lakini ifahamike kwamba hili sio tukio la pekee. Kenya ina moja ya viwango vya juu zaidi vya ukatili dhidi ya wanawake barani Afrika.

Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa mwezi Januari pekee zaidi ya wanawake 10 nchini humo walikuwa wahanga wa mauaji ya wanawake, ambayo yameelezwa na Umoja wa Mataifa kama mauaji ya wanawake kwa sababu ya jinsia zao.

Jane, sio jina lake halisi, anaiambia BBC kwamba amekuwa mafichoni kwa kipindi kirefu tu cha mwaka.

Anasema hawezi kurejea kazini kutokana na majeraha yaliyobadilisha maisha yake aliyoyapata baada ya mpenzi wake wa zamani kuchomwa kisu kikatili.

“Nia yake ilikuwa kuniua. Alinichoma kisu na kuniacha nikiwa nimefariki dunia. Ikiwa si majirani, ningekuwa nimefariki,” Jane anakumbuka.

Anasema alivumilia miongo kadhaa ya unyanyasaji mbaya zaidi kabla ya kuondoka. Kilichomfanya kutoweza kuvumilia tena ni wakati alipoanza uchokozi wake kwa watoto, anasema.

"Kuishi naye ilikuwa kama kuwa kuzimu. Sijui nimewezaje kuvumilia kwa miaka hiyo yote,” Jane anaongeza.

Mume wake aliyeachana naye anaendelea kumnyanyasa.

“Naishi kwa hofu. Anasema anataka kunimaliza. Siwezi kulala usiku. Kwa sasa naendelea kupata tiba kusaidia afya yangu ya akili. Mimi sio mhalifu lakini naishi kama niko jela.”

Pia unaweza kusoma:

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka wa 2018 ilidokeza kuwa asilimia 38 ya wanawake nchini Kenya wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 walifanyiwa ukatili na wapenzi wao wa karibu.

Makundi ambayo yanatoa msaada kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia yanasema kumekuwa na ongezeko la mwaka hadi mwaka la idadi ya visa hivyo.

"Kwa wastani, tunapokea hadi simu 50 na wakati mwingine watu hadi 20 hututembelea kwa siku," Njeri Migwi aliambia BBC.

Yeye ni kiongozi wa shirika linalofahamika kama ‘Usikimye’ – neno la Kiswahili linalomaanisha "usinyamaze".

Mnamo 2021, Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta alitangaza unyanyasaji wa kijinsia kuwa "tatizo la kitaifa".

Mwaka mmoja baadaye, ripoti ya serikali iligundua kuwa 41% ya wanawake walioolewa walifanyiwa ukatili wa kimwili.

Utafiti uliofanywa na Africa Data Hub uligundua kuwa kati ya 2016 na 2023, kulikuwa na visa zaidi ya 500 vya kuuawa kwa wanawake nchini Kenya.

"Katika asilimia 75 ya visa hivyo, mauaji yalifanywa na mtu ambaye alimfahamu mwanamke aliyeuawa - mpenzi wa karibu, jamaa au rafiki," ripoti inasema.

Mwanariadha wa mbio za masafa marefu Joan Chelimo anasema mauaji ya Cheptegei yamemwacha akiwa na mfadhaiko.

"Siwezi kulala, nikifikiria kwamba mtu alichomwa tu akiwa hai," anaongeza.

Mpenzi wa zamani wa Cheptegei pia alifariki kutokana na majeraha ya moto aliyoyapata akiwa anamshambulia Cheptegei.

Bi Chelimo ni mwanzilishi mwenza wa shirika la Tirop Angels lililoanzishwa baada ya kuuawa kwa mwanariadha mwingine, Agnes Tirop.

Anasema kwamba Cheptegei aliripoti dhuluma aliyokumbana nayo kwa polisi, lakini "hakuna kilichotokea".

"Kwa hivyo wahusika hawachukuliwi hatua kuwajibishwa," Bi Chelimo anaongeza.

Polisi wamekanusha madai kuwa Cheptegei aliripoti kuwa maisha yake yako hatarini.

Sunita Caminha, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa Wanawake kuhusu kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana katika Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika, anasema kuwa wanawake na wasichana wa asili tofauti wamekuwa waathirika wa mauaji ya wanawake katika ulimwengu ulioghubikwa na ubaguzi mkubwa wa kijinsia na ukosefu wa usawa.

Katika ripoti ya hivi punde ya Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, Afrika inachangia sehemu kubwa zaidi, huku wanawake 20,000 wakiuawa.

Kenya imepitisha sheria kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia, lakini wakosoaji wanasema ni hatua chache madhubuti zilizopo kukabiliana na tatizo hilo.

Judy Gitau, mkuŕugenzi wa kanda ya Afŕika wa kikundi cha kampeni cha Equality Now, anasema kwamba "kwa bahati mbaya, seŕikali mara nyingi huhisi kwamba pindi tu kunapokuwa na sheŕia, kila kitu kiko sawa – bila kuelewa kuwa sheŕia hazitekelezeki zenyewe na hazijitekelezi”.

Jane anasema kwamba kwa miaka mingi ripoti zake za unyanyasaji zilitupiliwa mbali.

"Mara nyingi, polisi wanasema huu ni ugomvi wa nyumbani. Kwanza, polisi mmoja mwanamke niliyezungumza naye alisema: 'Hatuwezi kumkamata hadi afanye jambo fulani.' Nikamuuliza: 'Unataka aniue?'

“Siku iliyofuata ndipo aliponichoma kisu,” Jane akumbuka.

Mwaka 2004, kitengo cha polisi chenye kuhusiska na masuala ya jinsia ya polisi kilianzishwa nchini Kenya ili kurahisisha wanawake kuripoti kesi za unyanyasaji wa kijinsia, na uchunguzi kuharakishwa.

Hata hivyo, ni nusu tu ya vituo vya polisi vilivyo nazo. Polisi wanasema hii ni kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali.

Huko Trans Nzoia, ambako Cheptegei aliishi, kuna vituo vitano vya polisi, lakini hakuna hata kimoja chenye kushughulikia masuala ya jinsia – kimoja pekee kiko katika makao makuu ya kaunti, anasema Kennedy Apindi, mkuu wa uchunguzi wa uhalifu katika kaunti hiyo.

"Kwa hivyo kuripoti kesi hizi ni shida. Huripotiwa kuchelewa, au haziripotiwi hadi usikie habari zao kwenye vyombo vya habari ndipo polisi wanaanza kulishughulikia,” anaongeza.

Cheptegei alikuwa mwanariadha wa tatu wa kike kufariki dunia nchini Kenya akidaiwa kuwa mikononi mwa mpenzi wake wa karibu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Mnamo 2021, wiki tano tu baada ya Agnes Tirop kuvunja rekodi ya dunia ya kukimbia kilomita 10 nchini Ujerumani, alipatikana ameuawa nyumbani kwake.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa na majeraha mengi ya kisu shingoni na tumboni.

Mpenzi wake Ibrahim Rotich alikamatwa na polisi umbali wa kilomita 640 (maili 400) huko Changamwe, pwani ya Kenya.

Miaka mitatu baada ya kuuawa, kesi bado iko mahakamani, huku Bw Rotich akiwa nje kwa bondi. Amekana shtaka la mauaji. Kesi zingine pia hudumu kwa miaka mingi.

Bi Gitau, ambaye yuko katika kamati ya mahakama iliyoundwa kuchunguza muda wa kesi za unyanyasaji wa kijinsia, anasema ucheleweshaji huo haukubaliki.

"Lazima kesi za [ukatili na unyanyasaji wa kijinsia] zipewe kipaumbele," Gitau anasema.

Miezi sita tu baada ya kuuawa kwa Tirop, mwanariadha mzaliwa wa Kenya wa Bahrain Damaris Muthee Mutua alipatikana amefariki dunia nyumbani kwake huko Iten, kuliko na wanariadha wengi katika Bonde la Ufa nchini Kenya.

Uchunguzi wa maiti ulibaini kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa amenyongwa.

Hakuna mtu ambaye amehukumiwa kwa mauaji yake.

Polisi walisema walikuwa wakimtafuta mpenzi wake kuhusiana na kifo hicho.

Sawa na Cheptegei, wanariadha wote wanadaiwa kuripoti ugomvi kuhusu pesa na mali na wapenzi wao kabla ya kukutana na mauti yao.

Bi Gitau anatoa wito wa kupewa nyumba salama zaidi kwa walionusurika.

"Kutoka ndani ya moyo wangu, mitazamo yetu, kanuni ambazo tunashikilia kama nchi, bado zinawaona wanawake kwa mtazamo fulani," anasema.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Asha Juma