Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Chakula kilivyosababisha mauaji India chazua mjadala wa unyanyasaji wa wanawake
Mwezi uliopita, polisi nchini India walimkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 46 ambaye anadaiwa kumuua mkewe kwa sababu kifungua kinywa chake kilikuwa na chumvi nyingi.
''Nikesh Ghag, karani wa benki huko Thane, karibu na mji wa magharibi wa Mumbai, alimnyonga mke wake mwenye umri wa miaka 40 kwa hasira kwa sababu chakula kinachofahamika kama khichdi ya sabudana [tapioca lulu au sago] alichokuwa anamuandalia kilikuwa na chumvi nyingi,'' afisa wa polisi Milind Desai, aliambia BBC.
Mtoto wa wanandoa hao mwenye umri wa miaka 12, ambaye alishuhudia uhalifu huo, aliwaambia polisi kwamba baba yake alimfuata mama yake, Nirmala, chumbani akilalamikia chumvi iliyopitiliza kwenye chakula na kuanza kumpiga.
''Aliendelea kulia na kumwomba babake awache anachofanya,'' Bw Desai alisema, ''lakini mshtakiwa aliendelea kumpiga mkewe na kumnyonga kwa kamba''.
Baada ya Bw Ghag kutoka nje ya nyumba kwa nguvu, mtoto huyo aliwaita bibi yake mzaa mama na mjomba wake.
''Kufika eneo la tukio, familia yake ilikuwa imemkimbiza hospitalini, lakini wakati huo alikuwa tayari amefariki,'' Bw Desai alisema.
Baadaye mshtakiwa alijisalimisha katika kituo cha polisi, ambapo aliwaambia maafisa kuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu.
Alipelekwa jela.
Familia ya Nirmala iliambia polisi kwamba Bw Ghag amekuwa akizozana naye kuhusu ''maswala ya nyumbani'' kwa siku 15 zilizopita.
Bw Desai alisema hawajapokea malalamishi yoyote kuhusu hili kutoka kwa mwathiriwa au familia yake.
Mauaji ya mwanamke na mumewe, yaliyochochewa na ugomvi juu ya chakula, mara kwa mara yanagonga vichwa vya habari nchini India.
Chukua baadhi ya kesi za hivi majuzi:
- Mnamo Januari, mwanamume mmoja alikamatwa huko Noida, kitongoji cha mji mkuu Delhi, kwa madai ya kumuua mkewe kwa kukataa kumpatia chakula cha jioni.
- Mnamo Juni 2021, mwanamume mmoja alikamatwa huko Uttar Pradesh baada ya kudaiwa kumuua mke wake kwa kukosa kula saladi na mlo wake.
- Miezi minne baadaye, mwanamume mmoja huko Bangalore alidaiwa kumpiga mkewe hadi kufa kwa kutopika kuku wa kukaanga ipasavyo.
- Mnamo mwaka wa 2017, BBC iliripoti kisa ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 60 alimuua mkewe kwa kumpiga risasi kwa kuchelewa kumuandalia chakula chake cha jioni.
Mwanaharakati wa jinsia Madhavi Kuckreja anasema 'kifo huleta usikivu'' lakini haya yote ni matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo ''hayaonekani''.
Matukio mengi yakiripotiwa chini ya kisheria ya ''ukatili wa mume au jamaa zake'', unyanyasaji wa nyumbani mara kwa mara umekuwa uhalifu wa kikatili dhidi ya wanawake unaoripotiwa zaidi nchini India mwaka baada ya mwaka.
Mnamo mwaka 2020 - mwaka wa mwisho ambapo data ya uhalifu inapatikana - polisi walipokea malalamiko kutoka kwa wanawake 112,292 - ambayo yanakadiriwa huripotiwa kila baada ya dakika tano.
Dhulma kama hiyo sio jambo la ajabu nchini India.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, mwanamke mmoja kati ya watatu duniani kote wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia, mwingi wao unasababishwa na wapenzi wa karibu.
Na nchini India hali ni sawa na hiyo.
Wanaharakati hapa wanapaswa kupigana na utamaduni wa ukimya unaoizunguka na kwa kushangaza kukubalika kwa kiasi kikubwa kwa vurugu kama hizo.
Takwimu za hivi punde kutoka Utafiti wa Kitaifa wa Afya ya Familia (NFHS5), uchunguzi wa kina zaidi wa kaya kuhusu jamii ya Kihindi uliofanywa na serikali, zina fafanua:
Zaidi ya 40% ya wanawake na 38% ya wanaume waliwaambia wachunguzi kutoka serikalini kuwa ni sawa kwa mwanaume kumpiga mkewe ikiwa anadharau wakwe zake, ametelekeza nyumba yake au watoto wake, anatoka nje bila kumwambia, kukataa kushiriki tendo la ndoa au kikosa kupika vizuri.
Katika majimbo manne, zaidi ya 77% ya wanawake walihalalisha kupigwa kwa mke.
Katika majimbo mengi wanawake wengi kuliko wanaume walihalalisha kupigwa kwa mke na katika kila jimbo - isipokuwa tu Karnataka - wanawake wengi zaidi kuliko wanaume walidhani ni sawa kwa mwanamume kumpiga mkewe ikiwa hakupika ipasavyo.
Idadi imepungua katika utafiti wa awali miaka mitano iliyopita - wakati 52% wanawake na 42% wanaume walihalalisha kupigwa kwa mke - lakini mitazamo haijabadilika, anasema Amita Pitre, ambaye anaongoza mpango wa haki ya jinsia wa Oxfam India.
''Unyanyasaji dhidi ya wanawake - na uhalali wake - unatokana na mfumo dume. Kuna kukubalika kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa sababu nchini India, wanawake wanachukuliwa kuwa wa duni, aliiambia BBC.
''Kuna fikra za kijamii ambazo haziwezi kubadilika kuhusu jinsi mwanamke anapaswa kuishi: daima awe chini ya mwanamume, aahirishe katika kufanya maamuzi, amtumikie na apate kipato kidogo kuliko yeye, miongoni mwa mambo mengine mengi. Na kukubalika kwa kinyume chake ni kwa asilimia ndogo sana. Kwa hivyo, ikiwa mwanamke atapinga, basi ni sawa kwa mume kumwonyesha mahali pake.''
Sababu inayowafanya wanawake zaidi kuhalalisha kumpiga mke, anasema, ni kwa sababu ''mfumo dume huimarisha kanuni za kijinsia na wanawake huweka mawazo sawa, imani zao hufinyangwa na familia na jamii''.
Bi Kuckreja, ambaye alianzisha Vanangana, shirika la hisani ambalo limekuwa likifanya kazi na wanawake waliopigwa kwa robo karne huko Bundelkhand kaskazini mwa India - moja ya mikoa maskini zaidi nchini - anasema ushauri unaotolewa kwa wachumba wapya unatafsiriwa kuwa ''Unaingia kwenye nyumba yako ya ndoa, utaondoka tu kwa jeneza lako wakati wa mazishi.''
Kwa hiyo wanawake wengi, hata wale wanaopigwa mara kwa mara, wanakubali ukatili kuwa hatima yao na hawatoi taarifa.
''Ingawa kuna ripoti nyingi zaidi katika muongo uliopita, kupigwa kwa mke bado hakuripotiwa sana nchini India. Kesi kama hizo ni ngumu kuripoti na kurekodi. Watu wengi bado wanaweza kusema kwamba kinachotokea nyumbani lazima kibaki nyumbani, nimekatishwa tamaa na kwenda kwa polisi,'' Bi Kuckreja anasema.
Pia, hawana pa kwenda ikiwa wataacha nyumba yao ya ndoa, anasema.
''Wazazi mara nyingi hawawataki kwa sababu ya unyanyapaa na, mara nyingi, kwa sababu ni maskini na hawawezi kulisha midomo ya ziada. Hakuna mfumo wa kutoa msaada, nyumba chache za makazi na fidia inayotolewa kwa wanawake waliotelekezwa ni duni - mara nyingi kati ya rupia 500 hadi 1500, ambayo haitoshi kwa mwanamke kuishi, acha peke yake kulisha watoto wake.''
Pushpa Sharma, anayeongoza Vanangana, aliniambia kuhusu kesi mbili alizopokea mwezi uliopita ambapo wanawake walipigwa na kisha kuachwa na waume zao, pamoja na watoto wadogo.
''Katika matukio yote mawili, waume zao waliwatoa nje ya nyumba wakiwa wamewashika nywele zao na kuwashambulia mbele ya majirani. Walidai kuwa hawakupika vizuri, lakini hiyo ni sehemu ya malalamiko. Mlo ni kichocheo tu.
Anasema mwanamke anaweza ''kupigwa kwa kuzaa watoto wa kike na sio mrithi wa kiume, au kwa sababu ana ngozi nyeusi au sio mzuri, au hakuleta mahari ya kutosha, au mume alikuwa amelewa ama hakuandaa chakula au maji kwa haraka mume aliporudi nyumbani, au aliweka chumvi zaidi kwenye chakula, au alisahau kumuongeza mume chakula.
Mnamo mwaka 1997, Vanangana alizindua mchezo wa kuigiza wa mitaani unaoitwa Mujhe Jawab Do ili kuhamasisha watu kuhusu unyanyasaji wa nyumbani.
''Ilianza na maneno 'ohh hakuna chumvi kwenye chakula… (supu ya dengu),'' Bi Kuckreja anasema.
''Baada ya miaka 25 ya kampeni yetu, kidogo hali imebadilika. Na hiyo ni kwa sababu ya kile tunachoweka kwenye ndoa. Tunafanya kila kitu ili kuokoa ndoa - ni takatifu, lazima idumu milele. ''Wazo hilo linahitaji kubadilika.''
Ni lazima tuwawezeshe wanawake.
''Hawana haja ya kuvumilia kupigwa,'' anasema.