Waridi wa BBC: 'Mume wangu alinikata mkono kisa wivu'

    • Author, Munira Hussein
    • Nafasi, BBC News

Simulizi ya mwanamke huyu ilianza kama hadithi nzuri ya mapenzi. Alikutana na mwanaume ambaye alikuja kuwa mume wake baadae, na wakabarikiwa Watoto wawili. Lakini mambo yalianza kubadilika taratibu.

Bi Veronica Kidemi, mkazi wa Arusha Tanzania anatupa simulizi yake ambayo ilisababisha kupoteza kiungo muhimu, mkono wake wa kulia ambao ulikatwa na mume wake wa ndoa.

Iilikua ndoa yenye upendo wa hali ya juu baina ya wawili hawa lakini Bi Veronica anasema mwenzake alianza kubadilika na kuwa ni mtu mwenye wivu sana na hakupenda yeye afanye kazi.

Veronica ni mwalimu kwa taaluma, ameajiriwa katika moja ya shule ya upili nchini Tanzania.

‘’Tulianza ndoa ilikua nzuri, lakini baadaye akawa mtu wa manyanyaso, akaanza kuwa ananipiga hovyo, kesi kubwa ni kunipangia muda wa kwenda kazini na kurudi, alikua ananituhumu kwanini najitolea kazini, hataki kujua chochote kuhusu kazini kwangu’’ anasimulia Veronica

Mambo yalianza kubadilika vipi?

Bi Veronika anaeleza kuwa wakati wameoana na mume wake, ndoa ilikua nzuri lakini baadae ndio mambo yakabadilika, Mume wake hakua na kazi na yeye ndio alikua akifanya kazi na kusaidia familia, kipato alichokua akipokea alikua akimkabidhi mume wake ili waweze kuendesha familia yao.

Lakini baadae mume wake alipata kazi katika shirika moja la Umma nchini Tanzania, baada ya kupata kazi ndio mambo yalianza kubadilika.

Veronica anasema kuwa alianza kudharau kazi yake na hakutaka kujua chochote kinachohusu kazi hiyo.

Veronica anasema pia visa vingi vya ugomvi vilitokana na wivu na pia mume wake huyo hakutaka afanye kazi muda mwingi.

Kulikua na ugomvi wa mara kwa mara baina ya wawili hawa hadi kufikia mwanamke huyu kuripoti kwa família na kanisa lililowafungisha ndoa hiyo.

‘’Nilipata tabu sana kazini kwangu, kesi zikawa nyingi hadi vikao vinawekwa kujadili ndoa yetu, nilikua najisikia vibaya sana, alikua akidhani nikienda kazini basi naenda kufanya mambo mengine na sio kufanya kazi.’’

Kukatwa mkono

Veronica anasema siku ya tukio hilo, alikua kazini kwake kama kawaida na wakati huo alikua anafanya kazi maalum aliyopangiwa baada ya kuzindulia kwa sera ya kuhakikisha wanamaliza tatizo la watoto kufeli shuleni.

na alipigiwa simu na mume wake na akamuonya kuwa kwakua anafanya kazi hizo shuleni, basi asirudi nyumbani na asimkute kabisa.

‘’Tulikua hatuna maelewano, na alinipigia simu, majira ya saa sita mchana, tulikua katika operesheni ya tokomeza zero shuleni, mume wangu akaniambia kwa simu kuwa niondoke na asinikute, kisa ilikua hatuna maelewano kutokana na mimi kujitolea kazini, kwakuniambia hivyo nikaomba ruhusa ya dharura ili nikachukue kitambulisho changu nyumbani niondoke ili anisikute,Kumbe alifanya mtengo, nlivyokaribia nyumbani akanivamia’’

Veronica anaongeza kuwa mume wake alimvamia na kuanza kumshambulia maeneo mbalimbali ya mwili kwa kutumia panga.

‘’Alinivamia na kunikata mapanga kichwani ikabidi nijifunike na mikono, huu mkono wa kushuto ukaumia sana, lakini mkono wa kulia alinikata mara moja tu ukadondoka chini, nikapiga kelele, watu barabarani wakatokea ndio kuniokoa’’

Usuluhishi wa família na kanisa

Wakati unatokea ugomvi wa mara kwa mara baina ya Veronica na mume wake, família yake ilikua ikisuluhisha na kumsihi Veronica kuendelea na ndoa yake. Upande wa kanisa pia ulikua ukimsihi Veronica asiondoke nyumbani kwake.

‘’Niliondoka tulivyogombana lakini kanisa walikuja kuniomba nirudi, wakanisihi nirudi ili tulee watoto, alibadilika kwa muda mfupi, lakini baadae akaanza kuwa kisirani, anasikiliza maneno ya kuambiwa, hakua anafuatilia mambo kwa undani’’

Veronica anasema kuwa asingeshawishiwa kurudi katika ndoa hiyo basi huenda asingepoteza kiungo chochote.

‘’Nilienda kutoa ripoti kanisani jumatano baada ya kuwa anagombana na mkuu wangu wa kazi, nikamfata mtumishi wa kanisani nikamwambia, lakini kakwua mume wangu alikua mbali, wakasema watawasiliana nae, lakini akawawahi, jumatano nimetoa taarifa, ijumaa akanifanyia hilo tukio. Nahisi kama ningekataa baada ya kanisa kunifata kurudi basi nisingepoteza kiungo chochote’’

Alijifunza kuandika na mkono wa kushoto

Kabla ya tukio hili Bi. Veronica alikua akitegemea sana mkono wake wa kulia katika kuandika na kuandaa machapisho ya kufundishia wanafunzi akiwa shuleni.

Lakini kama mama wa watoto wawili pia, alikua akitegemea sana kiungo hicho muhimu kufanya shughuli zake za nyumbani kama kufua na kuwashughulikia watoto.

Ili kuweza kuendelea na majukumu yake ya kila siku ilimbidi mwanamke huyu aanze kujifunza kutumia mkono wake wa kushoto.

Na kwa msaada wa kompyuta sasa anaweza kuandaa machapisho ya wanafunzi wake kwa kutumia kifaa hicho.

‘’Nilidhani atabadilika’’

Veronica anasema kuwa alifanya makosa makubwa kudhani kuwa mume wake angebadilika siku moja na kuwa mume mwema.

‘’Nashauri mtu yoyote akiona kuna manyanyaso, asivumilie, mimi nilivumilia sana, nikajua huyu mtu kuna siku atakuja kubadilika, kumbe hapana kinachokuja ni kibaya zaidi, yani mtu akikupiga hata kofi moja , hayo si mapenzi na akianza na moja ujue atendelea’’ anasema Veronica.

Mwanamke huyu anatoa wito pia kwa serikali, kuhakikisha kuwa mamlaka husika ziwe zinasikiliza malalamiko ya wanawake ambao wanapitia unyanyasaji.

Ameongeza pia kwa upande mwingine kanisa linapaswa likemee kwa kiasi kikubwa matukio kama haya hususani hali ikiwa inahatarisha usalama wa mwanamke.

‘’Kanisa ni kweli wanashikilia vitu vya imani, na kweli unaapa kuwa nitakua katika shida na raha, lakini unavumulia nini? Kama mimi nilikua navumilia nini , nilitakiwa nife, kuna nini pale navumilia?

Kesi na hukumu kwa aliyekua mume wake

Baada ya tukio hilo, kesi iliendeshwa na mahakama nchini Tanzania kwa miaka kadhaa, na mapema mwezi huu hukumu ya miaka minne jela ilitolewa kwa aliyekua mumewe pamoja na kulipa fidia ya shilingi milioni 15.