Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, kuishi na watu usiowajua kunaweza kuleta furaha zaidi?
- Author, Matilda Welin
- Nafasi, BBC
Wakati gharama za makazi na kukodisha zikiendelea kuwa juu, na huku Shirika la Afya Ulimwenguni likitangaza upweke kuwa ni suala linalotia mashaka kwa afya za watu duniani kote, maisha ya kuishi pamoja yameanza kuzingatiwa.
Rosie Kellett, 30, ni mwandishi wa mapishi aliyeko London. Mwaka 2020, alihitaji mahali papya pa kuishi baada ya penzi kuvunjika. Kwenye mitandao ya kijamii aliona ghala ambalo ni jengo la zamani la kiwanda – likiwa tupu.
Kwa sasa Kellett anaishi na watu wengine sita wakiwa na umri mwisho wa 20 na mapema 30. Kila wiki, kila mmoja wao huweka pauni 25 kwenye akaunti ya benki ya pamoja ili kulipia gharama ya vifaa vya nyumbani na chakula, mifuko ya taka, bidhaa za usafi na chakula cha jioni cha kila mtu.
Usiku ufikapo, mtu mmoja anapika. Katika kundi lao la mtandao wa kijamii watu huthibitisha ikiwa watahudhuria chakula cha jioni, kama wawekewe chakula watachelewa au watarudi nyumbani na mgeni.
Kuna kazi za nyumbani - na mikutano ya nyumbani. "Tunajaribu kuwa na mazungumzo mara kwa mara iwezekanavyo ili ikiwa mtu yeyote hajafurahishwa na jambo, au ikiwa kuna chochote mtu anataka kujadili."
Jambo bora zaidi juu ya kuishi kijumuiya, anasema, ni kwamba kila wakati kuna mtu karibu. Unahisi kama familia.
"Kuna changamoto, pia," Kellett anasema. Lazima afanye bidii kuhakikisha anapata wakati wake pekee. "Kuna bafu mbili na vyoo viwili, ambavyo wote tunatumia bila shida, lakini kuna mashine moja ya kuosha nguo na haitoshi kabisa," anasema.
Creal Zearing, 36, anaishi na mume wake na bintiye mwenye umri wa miaka mitatu katika nyumba ya jumuiya huko Madison, Wisconsin nchini Marekani.
Takriban watu 100 wanaishi hapo, kuanzia familia zilizo na watoto hadi wazee walio peke yako. Kuna matukio ya kijamii kama sherehe na karamu kila mwezi.
‘Kuna mkutano wa wanajumuiya kila baada ya wiki mbili, na vikao vya bodi na kamati, pia. Mimi nafanya kazi lakini kuna kundi la watu ambao wamestaafu. Kila mkazi anatarajiwa kuchangia saa nne za kazi kwa wiki,’’ anasema Zearing.
"Ninachothamini sana ni kwamba tuna jamii kubwa," anasema Zearing. "Kama mama mpya nimeweza kuwategemea wazazi wengine kwa ushauri."
Pia anapenda ikiwa anaporudi nyumbani kutoka kazini akiwa amechoka, humpeleka binti yake nje ya nyumba ili kucheza na watoto wengine.
‘Sio kila kitu kiko sawa. Mumewe amepingwa mara kadhaa, baada ya kupendekeza njia mpya za kufanya mambo, na kukutana na upinzani.’’
Kuna faida kuishi kijumuiya?
Wanachama wa kituo kimoja huko Suffolk waliiambia BBC 2023 kwamba uwepo wao ulikuwa unasaidia kuwalinda kutokana na shida ya gharama ya maisha.
Katika makazi ya pamoja, watu wana nyumba zao zinazojitosheleza na jumuiya inajisimamia yenyewe.
Kinachofanya jumuiya hizi kuwa tofauti na aina nyingine za jumuiya ni kwamba kuna kiwango cha kusanyo la mapato. Mapato yako yanaingia kwenye kapu moja na kisha mnatumia vitu pamoja."
Watu zaidi wanaweza kugeukia maisha ya haya kwa sababu soko la kupata nyumba linazidi kuwa gumu.
Utafiti unaonyesha watu wanaoishi katika jumuiya hizi wana maisha bora na ni watu wenye furaha zaidi katika jamii.
Changamoto zipo
Anasema Penny Clark, mtaalamu wa kusaidia upatikanaji wa nyumba za jumuiya, "kazi unayofanya katika nyumba hizo inaweza kuwa kubwa - wakati mwingine inageuka kuwa ngumu sana, na watu huondoka wakiwa wamekasirika."
Pia ni vigumu kuunda jumuiya mpya ya makazi ya pamoja. Ni vigumu kupata ardhi, kuna hatari za kifedha, na benki zinasitasita kukopesha pesa.
"Tuko katika dunia ambayo ina mawazo fulani kuhusu maisha bora ni nini, na nyumba nzuri ni ipi. Na maisha ya jumuiya hayalingani na mawazo hayo," Clark anasema.
"Katika jamii tuna mtazamo kwamba faragha ni nzuri, na kumiliki vitu vyako ni jambo zuri. Na kuishi maisha ya pamoja sio matarajio ya wengi. Wazo la nyumba nzuri ni nyumba kubwa ambayo unamiliki peke yako."
Watu wanaoishi kwenye nyumba za jumuiya, huulizwa maswali mara kwa mara kutoka kwa watu wanaotaka kuhamia.
Huko London, baada ya Rosie Kellett kuweka video mbili Instagram kuhusu jinsi anavyoishi, watu wengi waliwasiliana naye wakiuliza kama wanaweza kuhamia.
"Nilijisikia vibaya kwa sababu tulikuwa hatuchuki watu wapya," anasema. "Kwa kweli kuna hamu ya kuwa na nyumba nyingi kama hizi, lakini lazima uiandae mwenyewe."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah