Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Unachopaswa kujua kuhusu mzozo kati ya Israel na Hezbollah
Israel na Hezbollah wanaonekana kuelekea kwenye vita vya kila upande ambavyo vinaweza kuenea katika eneo hilo kubwa, baada ya wiki moja ya kuongezeka kwa mzozo wao wa muda mrefu.
Baada ya siku kadhaa za mashambulizi ya anga dhidi ya Beirut na kusini mwa Lebanon, Israel ilitangaza kuwa jeshi lake lilikuwa limeanza "mashambulio machache, ya ndani na yaliyolenga ardhini" dhidi ya Hezbollah.
Siku ya Ijumaa, Israel ilitoa pigo kubwa dhidi ya kundi la Kiislamu la Shia kwa kumuua kiongozi wao Hassan Nasrallah katika shambulio kubwa la anga katika viunga vya kusini mwa Beirut.
Israel imefanya mashambulizi baada ya takriban mwaka mmoja wa mapigano ya mpakani yaliyosababishwa na vita huko Gaza, ikisema inataka kuhakikisha wanarejea salama wakaazi wa maeneo ya mpakani ambao wamefurushwa na mashambulizi ya Hezbollah.
Ingawa Hezbollah imedhoofishwa, haijashindwa. Kundi hilo linaendelea kurusha makombora kaskazini mwa Israel na bado linaaminika kuwa na silaha kubwa ya makombora ya masafa marefu.
Huu hapa mwongozo mfupi wa hatua zilizopigwa hivi karibuni.
Israel yaanzisha operesheni ya ardhini kusini mwa Lebanon
Katika taarifa iliyotumwa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) saa 02:00 kwa saa za ndani siku ya Jumanne asubuhi, Israel ilithibitisha kile ambacho kilitarajiwa na wengi - kwamba ilikuwa ikianzisha mashambulizi ya ardhini kuvuka mpaka na kuingia Lebanon.
IDF ilisema kwamba malengo yake "yapo katika vijiji vilivyo karibu na mpaka na yanaleta tishio la haraka kwa jamii za Israeli kaskazini mwa Israeli".
Tangazo hilo lilitanguliwa na vifaru vya Israel karibu na mpaka wa Lebanon na uhamasishaji wa askari wa akiba.
Mkuu wa Kamandi ya Kaskazini ya jeshi anapendelea kuundwa kwa eneo la amani ndani ya kusini mwa Lebanon, ili kuwaondoa wapiganaji wa Hezbollah na miundombinu mbali na mpaka, na kuruhusu Israel kuwarejesha raia 60,000 kwenye nyumba walizohama karibu mwaka mmoja uliopita.
Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti hapo awali kwamba makundi madogo ya makomando wa Israel yamekuwa yakifanya mashambulizi mafupi kuvuka mpaka.
Uvamizi wa Lebanon unafuatia mfululizo wa mashambulizi dhidi ya Hezbollah
Israel imefanya uharibifu mkubwa dhidi ya Hezbollah katika wiki za hivi karibuni, na kuua zaidi ya makamanda wakuu kumi na inaonekana kuharibu maelfu ya silaha katika mashambulio ya anga.
Pia ililaumiwa kwa mashambulizi ya pager na walkie-talkie ambayo yaliwaacha maelfu ya wanachama wa Hezbollah wakiwa vilema, vipofu au kuuawa.
Hata hivyo, Mhariri wa Kimataifa wa BBC Jeremy Bowen anasema kuuawa kwa Hassan Nasrallah ni pigo kubwa kuliko yote.
Kwa zaidi ya miaka 30, alikuwa moyo unaopiga wa Hezbollah. Kwa msaada wa ufadhili wa Iran, mafunzo na silaha, aliigeuza kundi hilo kuwa kikosi cha kijeshi ambacho mashambulizi yake yalipelekea Israel kukomesha ukaliaji wa miaka 22 kusini mwa Lebanon mwaka 2000 na ambayo ilipigana na Israel na kusimama wakati wa vita vya mwezi mzima mwaka 2006.
Kwa Israeli, mauaji ya Nasrallah ni ushindi mkubwa. Katika hotuba ya kejeli katika Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alidai kuwa Israel "inashinda" vita dhidi ya maadui wanaotaka kuiangamiza. Kufikia wakati huo, alikuwa ameidhinisha shambulio lililomuua Nasrallah.
Lebanon inasema mamia wameuawa na hadi milioni moja wamekimbia makazi yao
Wizara ya afya ya Lebanon ilisema Jumamosi kwamba mashambulizi ya Israel yameua zaidi ya watu 1,000 katika wiki mbili zilizopita, wakiwemo watoto 87 na wanawake 56.
Hakukuwa na kikomo cha mashambulizi ya Israel siku ya Jumapili, baada ya watu wengine 100 kuuawa huku Waziri Mkuu Najib Mikati akionya kwamba takriban watu milioni moja - moja ya tano ya idadi ya watu - wanaweza kuwa wamekimbia makazi yao.
Mamlaka zinatatizika kusaidia kila mtu, huku malazi na hospitali zikiwa chini ya shinikizo.
Israel inasema inashambulia maeneo ya Hezbollah, ikiwa ni pamoja na maduka ya silaha na dampo za risasi, na ilishutumu kundi hilo kwa kutumia raia kama ngao za binadamu.
Lakini mwandishi mwandamizi wa kimataifa wa BBC Orla Guerin anasema hilo linapingwa na wakaazi wa Bonde la Bekaa la kati, ngome ya Hezbollah ambayo imekuwa ikilipuliwa mara kwa mara katika wiki iliyopita.
Mkurugenzi wa matibabu wa hospitali ya eneo la Rayaq pia alimwambia kwamba majeruhi wote ambao ilikuwa imewatibu walikuwa raia.
PICHA...
Juhudi za kuzuia mzozo huo zimegonga mwamba
Rais wa Marekani Joe Biden aliunga mkono mauaji ya Hassan Nasrallah. Hata hivyo, mwandishi wa BBC wa idara ya mambo ya nje Tom Bateman anasema uamuzi wa Israel wa kuzidisha mzozo huo na Hezbollah ulipata pigo kubwa kwa mkakati wake wote wa miezi 11 iliyopita - kujaribu kusimamisha vita huko Gaza vinavyokumba eneo hilo.
Biden amesema anaongeza ulinzi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, huku Pentagon ikiwaonya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kutojaribu kutumia wakati huu kushambulia kambi za Marekani.
Licha ya majaribio ya awali ya Marekani kumdhibiti kiongozi wa Israel na kuwashawishi Hezbollah waafikie mapatano, Netanyahu ameashiria kwa nguvu kwamba atafanya anavyoona inafaa, bila kujali shinikizo kutoka kwa Washington.
Hezbollah na Iran wanafikiria jinsi ya kujibu
Katika hotuba yake siku ya Jumatatu, naibu kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassam, alielezea mashambulizi yake ya sasa ya roketi, ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya Israel kama "kima cha chini kabisa" na akasema "itaibuka washindi" baada ya mashambulizi ya ardhini ya Israel.
Kundi hilo bado lina maelfu ya wapiganaji, wengi wao wakiwa ni wapiganaji wa zamani katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchi jirani ya Syria, pamoja na makombora, mengi yao yakiwa yale ya masafa marefu, yanayoongozwa kwa usahihi ambayo yanaweza kufika Tel Aviv na miji mingine.
Mwandishi wa Usalama wa BBC Frank Gardner anasema kutakuwa na shinikizo ndani ya kundi hilo kutumia makombora hayo kabla ya kuharibiwa, na kwamba shambulio kubwa dhidi ya Israeli ambalo litaua raia linaweza kusababisha majibu mabaya.
Mauaji ya Nasrallah pia yalikuwa pigo kubwa kwa Iran, yakigonga katikati mwa mtandao wa kikanda wa wanamgambo washirika, wenye silaha kali wanaojulikana kama "Mhimili wa Upinzani" ambao ni muhimu kwa mkakati wake wa kuzuia dhidi ya Israeli.
Siku ya Jumapili, ndege za Israel zilishambulia miundombinu katika mji wa bandari wa Bahari ya shamu ya Hudaydah nchini Yemen kujibu mashambulizi ya hivi majuzi ya makombora na ndege zisizo na rubani za wapiganaji wa Houthi wanoungwa mkono na Iran.
Iran inaweza kuwaomba Wahouthi na makundi mengine kuongeza mashambulizi yao dhidi ya kambi za Israel na Marekani katika eneo hilo.
Lakini jibu lolote itakalochagua, litasababisha vita vya kikanda ambavyo vinaweza kuivutia Marekani na ambavyo haiwezi kuvishinda.
imetafsiriwa na Seif Abdalla