Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah ni nani?
Nasrallah hajaonekana hadharani kwa miaka kadhaa sasa kutokana na hofu ya kuuawa na Israel.
Na siku ya Jumamosi, wanajeshi wa Israel walisema walimuua Nasrallah katika shambulio la Beirut.
Pia, Hezbollah imethibitisha kifo cha kiongozi Hassan Nasrallah baada ya Israel kushambulia Beirut.
Akiwa na uhusiano wa karibu na Iran, alichukua jukumu muhimu katika kuigeuza Hezbollah kuwa na nguvu ya kisiasa na kijeshi ilivyo leo - na anabakia kuheshimiwa na wafuasi wa kundi hilo.
Chini ya uongozi wa Nasrallah, Hezbollah imesaidia kutoa mafunzo kwa wapiganaji kutoka kundi la wapiganaji la Palestina la Hamas, pamoja na wanamgambo wa Iraq na Yemen, na kupata makombora na roketi kutoka Iran kwa ajili ya mapambano dhidi ya Israel.
Aliongoza mageuzi ya Hezbollah kutoka kwa wanamgambo walioasisiwa kupigana na wanajeshi wa Israel wanaoikalia Lebanon kuwa jeshi lenye nguvu kuliko jeshi la Lebanon, mbabe katika siasa za Lebanon, mtoaji mkuu wa huduma za afya, elimu na huduma za kijamii, na sehemu muhimu ya Iran katika ukanda wa mashariki ya kati.
Hassan Nasrallah alizaliwa mwaka 1960, alikulia katika kitongoji cha Bourj Hammoud mashariki mwa Beirut, ambapo baba yake Abdul Karim alikuwa akiendesha biashara mbogamboga. Alikuwa mtoto mkubwa kati ya watoto tisa.
Alijiunga na vuguvugu la Amal, ambalo wakati huo lilikuwa la wanamgambo wa Shia, baada ya Lebanon kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1975. Baada ya kukaa kwa muda mfupi katika mji mtakatifu wa Iraq wa Najaf katika seminari ya Shia, alijiunga tena na Amal huko Lebanon kabla ya yeye na wengine kujitenga na kundi hilo mwaka 1982, muda mfupi baada ya Israel kuivamia Lebanon kujibu mashambulizi ya wanamgambo wa Kipalestina.
Kundi hilo jipya, Islamic Amal, lilipata uungwaji mkono mkubwa wa kijeshi na kimashirika kutoka kwa wanamapinduzi wa Iran wenye makao yake katika Bonde la Bekaa, na likaibuka kuwa kundi mashuhuri na madhubuti zaidi kati ya wanamgambo wa Shia ambao baadaye waliunda Hezbollah.
Mwaka 1985, Hezbollah ilitangaza rasmi kuanzishwa kwake kwa kuchapisha "barua ya wazi" ambayo ilibainisha Marekani na Umoja wa Kisovieti kama maadui wakuu wa Uislamu na kutaka "kuangamizwa" kwa Israel, ambayo ilitajwa ilikuwa inakalia kwa mabavu ardhi za waislamu.
Nasrallah alipitia katika ngazi tofauti za uongozi wa Hezbollah kadiri kundi hilo lilivyokua. Alisema baada ya kutumika kama mpiganaji alikuwa mkurugenzi wake huko Baalbek, kisha eneo lote la Bekaa, na baadaye Beirut.
Alikuwa kiongozi wa Hezbollah mwaka 1992 akiwa na umri wa miaka 32, baada ya mtangulizi wake Abbas al-Musawi kuuawa katika shambulio la helikopta la Israel.
Moja ya matendo yake ya kwanza ilikuwa ni kulipiza kisasi mauaji ya Musawi. Aliamuru mashambulizi ya roketi kaskazini mwa Israel ambayo yalimuua msichana, afisa wa usalama wa Israel katika ubalozi wa Israel nchini Uturuki aliyeuawa kwa bomu lililotegwa kwenye gari na mlipuaji wa kujitoa muhanga akaupiga ubalozi wa Israel mjini Buenos Aires, Argentina na kuua watu 29.
Nasrallah pia alisimamia vita vikali dhidi ya vikosi vya Israeli vilivyomalizika kwa kuondoka kwao kusini mwa Lebanon mnamo 2000, ingawa alipata pigo la binafsi kwani mtoto wake mkubwa Hadi aliuawa katika mapigano makali na wanajeshi wa Israeli.
Kufuatia kujiondoa huko Nasrallah alitangaza kwamba Hezbollah imepata ushindi wa kwanza wa Waarabu dhidi ya Israeli. Pia aliapa kwamba Hezbollah haitapokonya silaha, akisema kwamba inazingatia kwamba "eneo lote la Lebanon lazima lirejeshwe", likiwemo eneo la Mashamba ya Shebaa.
Kulikuwa na utulivu wa kiasi hadi mwaka 2006, wakati wanamgambo wa Hezbollah walipoanzisha mashambulizi ya kuvuka mpaka ambapo wanajeshi nane wa Israel waliuawa na wengine wawili kutekwa nyara, na kusababisha Israel kuanizsha mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Ndege za kivita za Israeli zilirusha mabomu katika ngome muhimu za Hezbollah katika eneo la Kusini na vitongoji vya kusini mwa jiji la Beirut, huku Hezbollah ikirusha takribani roketi 4,000 kwenda Israel. Zaidi ya Walebanon 1,125, wengi wao raia, waliuawa katika mzozo wa siku 34, pia walikufa wanajeshi 119 wa Israeli na raia 45.
Makazi na ofisi ya Nasrallah yalilengwa na ndege za kivita za Israel, lakini alinusurika bila kupata hata jeraha.
Mwaka 2009, Nasrallah alitangaza ilani mpya ya kisiasa ambayo ililenga kubainisha “dira ya kisiasa” ya Hezbollah. Iliachana na kujihusisha na jamhuri ya Kiisilamu iliyokuwemo kwenye waraka wa mwaka 1985, lakini iliendelea na msimamo mkali dhidi ya Israel na Marekani na ilisisitiza kwamba Hezbollah ilihitaji kubakia kuwa na silaha licha ya azimio la Umoja wa Mataifa kulipiga marufuku kusini mwa Lebanon.
"Watu hubadilika . Dunia nzima imebadilia katika kipindi cha miaka 24 iliyopita. Lebanon imebadilika. Misimamo ya dunia imebadilika," Nasrallah alisema.
Miaka minne baadaye, Nasrallah alitangaza kuwa Hezbollah ilikuwa ikiingia katika “awamu mpya kabisa” ya uwepo wake kwa kutuma wapiganaji wake nchini Syria ili kumsaidia Rais wa nchi hiyo, Bashar al-Assad, anayeungwa mkono na Iran. “Ni mapambano yetu na tutashiriki kikamilifu”, alisema.
Kiongozi wa madhehebu ya Sunni nchini Lebanon aliishutumu Hezbollah kwa kuiingiza nchi hiyo katika vita vya Syria na kusababisha kuongezeka kwa hali ya wasiswasi.
Mwaka 2019, mdororo mkubwa wa kiuchumi nchini Lebanon ulisababisha maandamano makubwa dhidi ya tabaka la uongozi wa kisiasa lililoshutumiwa kwa rushwa, uongozi mbaya, na kutokujali. Mwanzoni Nasrallah alielezea umuhimu wa miito ya kutaka mabadiliko, lakini msimamo wake ulibadilika baada ya maandamano kuanza, akitaka kufumuliwa kabisa kwa mfumo wa kisiasa.
Oktiba 8, 2023 -siku moja baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel ambalo halikuwahi kutokea awali, na kuanzisha vita huko Gaza – mapigano kati ya Hezbollah na Israel yakazidi.
Hezbollah iliishambulia Israeli, katika kuwaunga mkono Wapalestina.
Katika hotuba yake ya Novemba, Nasrallah alisema shambulio la Hamas lilikuwa ni “asilimia 100 ya Wapalestina kwa misingi ya uamuzi na utekelezaji” lakini mashambulizi kati ya kundi lake na Israel yalikuwa “muhimu mno na yenye maana”.
Kundi hilo lilifyatua zaidi ya roketi 8,000 Kaskazini mwa Israel katika Milima ya Golan inayokaliwa na Israel. Hezbollah pia ilirusha makombora ya kushambulia vifaru magari ya kivita na kushabulia kambi za kijeshi kwa milipuko na ndege zisizo na rubani.
Jeshi la Israel (IDF) lilijibu mapigo kwa mashambulio ya anga na vifaru dhidi ya ngome za Hezbollah nchini Lebanon.
Katika hotuba zake za karibuni zaidi, Nasrallah aliishutumu Israel kwa kulipiua maelfu ya vifaa vya mawasiliano, maarufu pagers na radio za upepo zilizokuwa zikitumiwa na wanachama wa Hezbollah, na kuwaua watu 39 na kuwajeruhi wengine kwa maelfu, na kusema Israel ilikuwa “imevuka mistari yote myekundu”. Alikiri kuwa kundi lake lilikuwa limepata pigo kubwa zaidi ambalo halikuwahi kutokea awali.
Muda mfupi baadaye Israel ilizidisha mashambulio ya kuilenga Hezbollah, kwa kurusha mabomu yaliyowaua takribani watu 800.
Imetafsiriwa na Florian Kaijage