Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kiongozi wa muda mrefu wa Hezbollah Hassan Nasrallah ameuawa baada ya Israel kushambulia Beirut

Hezbollah imeapa kuendelea kupigana baada ya kuthibitisha kifo cha Nasrallah - saa kadhaa kabla, jeshi la Israel lilisema lilimuua katika shambulio katika mji mkuu wa Lebanon.

Muhtasari

  • 'Hatupigani vita na watu wa Lebanon – tunapigana na Hezbollah' - msemaji wa IDF
  • Ndege za Iran zaambiwa zisiingie kwenye anga ya Lebanon - ripoti
  • Hezbollah imeahidi kupigana vita baada ya kuthibitisha kifo cha Nasrallah
  • Hezbollah yathibitisha kiongozi wake Hassan Nasrallah ameuawa
  • Khamenei: Vikosi katika kanda vinaunga mkono na kusimama na Hezbollah
  • 'Ni wakati hatari Mashariki ya Kati' - Hugo Bachega
  • Mkuu wa masuala ya kigeni EU: 'Hakuna anayeweza kumzuia Netanyahu'
  • Israel yasema ilimuua kamanda wa makombora wa Hezbollah
  • Kiongozi wa Hezbollah alengwa katika mashambulizi ya anga ya Israel

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tumekamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo. Kwaheri.

  2. Hamas inasimama katika 'mshikamano' na Hezbollah baada ya kifo cha Nasrallah

    Tunasikia sasa taarifa kutoka kundi la wanamgambo wa Palestina, Hamas ambao pamoja na Hezbollah yenye makao yake Lebanon wanaungwa mkono na Iran kijeshi na kifedha.

    Kundi hilo lenye makao yake makuu huko Gaza, linasema kuwa linaomboleza kifo cha kiongozi wa Hezbollah na kwamba linasimama katika "mshikamano na ndugu wa Hezbollah na upinzani wa Kiislamu nchini Lebanon".

    Wakati mzozo wa Israel na Hezbollah umekuwa ukiendelea kwa miongo kadhaa, vita vya sasa kati yao vilianza baada ya watu wenye silaha wa Hamas kuanzisha mashambulizi kutoka Gaza tarehe Oktoba 7, 2023 na kuwaua takriban watu 1,200.

    Mapigano kati ya Hezbollah na Israel yalianza kuongezeka Oktoba 8, 2023 - siku moja baada ya shambulio hilo ambalo halijawahi kutokea awali.

    Hezbollah ilishambulia maeneo kadhaa ya kijeshi ya Israel kwa mshikamano na Wapalestina na kusema kuwa itaendelea kupambana na Israel hadi usitishaji mapigano Gaza utakapotekelezwa.

  3. 'Hatupigani vita na watu wa Lebanon – tunapigana na Hezbollah' - msemaji wa IDF

    Msemaji wa Jeshi la Israel (IDF) Daniel Hagari amezungumzia kifo cha Hassan Nasrallah mara tu baada ya kifo hicho kuthibitishwa na Hezbollah na IDF.

    Hagari alimuelezea Nasrallah kuwa "miongoni mwa maadui wakubwa kabisa wa Israel"

    Alisema Nasrallah aliuawa katika shambulio "sahihi" lililotekelezwa na jeshi la anga la Israeli siku ya Ijumaa huko Beirut.

    Jeshi la Israel kwa sasa linashambulia miundombinu ya Hezbollah nchini Lebanon, Hagari anasema.

    Aliongeza kuwa kuwa jeshi lipo katika "tahadhari ya kiwango cha juu kabisa wakati wote"

    "Hatupigani vita haviko na watu wa Lebanon, tunapigana vita na Hezbollah", alisema

    Aliongeza kuwa mikusanyiko katikati mwa Israeli imepunguzwa hadi watu wasiozidi 1,000

  4. Ndege za Iran zaambiwa zisiingie kwenye anga ya Lebanon - ripoti

    Wizara ya uchukuzi ya Lebanon imeambia ndege ya Iran isiingie kwenye anga yake baada ya Israel kuonya udhibiti wa usafiri wa anga huko Beirut kwamba itatumia "nguvu" ikiwa ndege hiyo itatua, kulingana na shirika la habari la Reuters.

    Chanzo cha wizara hiyo kilisema haijabainika ni nini kilikuwa kwenye ndege hiyo.

    "Kipaumbele ni maisha ya watu," chanzo hicho kiliongeza.

    Onyo hili linawadia baada ya jeshi la Israel kusema kuwa limemuua Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hezbollah.

    Kundi hilo limepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa Iran, kifedha na kijeshi, kwa miaka mingi na linashirikiana na Hamas.

    EU yaonya mashirika ya ndege kuepuka anga ya Lebanon na Israel

    Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya unayaonya mashirika ya ndege kuepuka anga ya Lebanon na Israel kwa kipindi cha mwezi mmoja.

    Shirika la Usalama wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA) limetoa pendekezo rasmi "kutofanya kazi ndani ya anga za Lebanon na Israel katika viwango vyote vya ndege," kwa muda wa hadi tarehe 31 Oktoba.

    "EASA itaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo, kwa nia ya kutathmini kama kuna ongezeko au kupungua kwa hatari kwa waendeshaji ndege wa EU kutokana na mabadiliko ya tishio," EASA ilisema.

  5. Hezbollah imeahidi kupigana vita baada ya kuthibitisha kifo cha Nasrallah

    Kundi la Hezbollah limetoa taarifa ndefu katika mtandao wa Telegram baada ya kuthibitisha kuwa kiongozi wake - Hassan Nasrallah "ameuawa".

    "Mtukufu, Mkuu wa Upinzani, mja mwadilifu, amefariki dunia na kurejea kwa Mola wake," inasema taarifa hiyo.

    Kundi hilo lilionekana kuthibitisha kwamba alifariki kutokana na mashambulizi ya anga huko Beirut, likisema kifo chake kimesababishwa na "uvamizi wa kihaini wa Wazayuni kwenye kitongoji cha kusini".

    Kundi hilo pia liliendelea "kuahidi" kupigana vita dhidi ya Israel na kuendelea kuunga mkono "Gaza na Palestina, na kuilinda Lebanon na watu wake thabiti na wenye heshima".

    Mapigano kati ya Hezbollah na Israel yaliongezeka tarehe 8 Oktoba 2023 - siku moja baada ya shambulio lisilokuwa na kifani dhidi ya Israel na wapiganaji wa Hamas ambao walianzisha vita huko Gaza.

    Hezbollah imesema itaacha kushambulia Israel pale tu vita vya Gaza vitakapokoma

    Soma zaidi:

  6. Habari za hivi punde, Hezbollah yathibitisha kiongozi wake Hassan Nasrallah ameuawa

  7. Khamenei: Vikosi katika kanda vinaunga mkono na kusimama na Hezbollah

    Kiongozi Mkuu wa Iran amezungumza kwa mara ya kwanza tangu Israel iliposema kuwa imemuua kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah.

    Hezbollah, kikundi chenye makao yake nchini Lebanon kimepata uungwaji mkono wa nguvu kutoka kwa Iran, kifedha na kijeshi, kwa miaka mingi.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi, Ayatollah Khamenei hakumtaja Nasrallah hata kidogo.

    Alianza kwa kulaani kwanza mauaji ya "watu wasio na ulinzi wa Lebanon", akisema kwamba "ilithibitisha hatua na sera za kizembe za viongozi" wa Israel.

    "Wahalifu wa Israel lazima wajue kwamba wao ni wadogo sana kuweza kusababisha uharibifu wowote mkubwa kwenye ngome za Hezbollah nchini Lebanon," Khamenei alisema na kuongeza: "Vikosi vyote vya upinzani katika eneo hilo vinaunga mkono na kusimama pamoja na Hezbollah."

    Pia aliwataka Waislamu wote kusimama pamoja na watu wa Lebanon na Hezbollah na kuwaunga mkono katika "kukabiliana na utawala wa kidhalimu".

    Soma zaidi:

  8. 'Ni wakati hatari Mashariki ya Kati' - Hugo Bachega

    Hugo Bachega

    Mwandishi wa Mashariki ya Kati, mjini Beirut

    Taarifa kutoka kwa jeshi la Israel, kwamba kiongozi mwenye nguvu na wa muda mrefu wa Hezbollah Hassan Nasrallah aliuawa katika shambulio la anga huko Beirut, raia wa eneo hili wanaendelea kulipokea - na bado hakuna taarifa rasmi kutoka kwa Hezbollah.

    Hezbollah, ambayo inachukuliwa kuwa shirika la kigaidi na Uingereza, Marekani na wengine, ni zaidi ya wanamgambo. Pia ni chama cha kisiasa, chenye uwakilishi katika bunge la Lebanon, na sehemu ya serikali. Ina msingi mkubwa na ni sehemu ya jamii ya Lebanon.

    Hatujui Hezbollah itajibu vipi. Tumeona kwamba Hezbollah bado haijatuma makombora yake ya hali ya juu zaidi, ikiwa ni pamoja na makombora ya kuongozwa kwa usahihi ambayo yanaweza kushambulia ndani kabisa ya Israel.

    Dalili zimekuwa zikionyesha kuwa kundi hilo halikutaka makabiliano makubwa na Israel ambayo yanaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu yake na mauaji ya viongozi wake wakuu.

    Hivi ndivyo ilivyotokea, kwa hivyo nadhani kuna swali kubwa ambalo halijajibiwa.

    Pia kumekuwa na wasiwasi kwamba aina yoyote ya mzozo mkubwa kati ya Israel na Hezbollah unaweza kulazimisha makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran katika kanda nzima kujiunga na Hezbollah katika vita hivi.

    Ni wakati hatari sana Mashariki ya Kati na matokeo yasiyotabirika.

    Soma zaidi:

  9. Mkuu wa masuala ya kigeni wa EU: 'Hakuna anayeweza kumzuia Netanyahu'

    Mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya anasema hakuna mamlaka yoyote, ikiwemo Marekani, inayoweza "kumzuia" Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

    Josep Borrell aliwaambia waandishi wa habari mjini New York kwamba "tunachofanya ni kuweka shinikizo zote za kidiplomasia ili kusitishwa kwa mapigano, lakini hakuna anayeonekana kuwa na uwezo wa kumzuia Netanyahu, si Gaza wala katika Ukingo wa Magharibi".

    Borrell alisema Netanyahu aliweka wazi kwamba Waisraeli "hawatakome hadi Hezbollah iangamizwe".

    "Ikiwa tafsiri ya kusambaratishwa ni sawa na Hamas, basi vita vitaendelea kwa kipindi kirefu," alisema, akinukuliwa na shirika la habari la AFP.

    Aliunga mkono wito wa Marekani na Ufaransa wa kusitisha mapigano kwa siku 21.

    Israel yazuia makombora yaliyorushwa nchini Israel kutoka Lebanon - IDF

    Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema liligundua roketi 10 zilizorushwa kutoka Lebanon mapema Jumamosi, baada ya ving'ora kuanza kulia katika eneo la juu la Galilaya nchini Israel.

    Baadhi ya roketi hizo zilinaswa, ilisema taarifa hiyo, bila kutaja uharibifu wowote au waliojeruhiwa.

    "IDF inaendelea kushambulia, kuharibu na kusambaratisha uwezo wa kijeshi wa Hezbollah na miundombinu nchini Lebanon," ilisema katika taarifa.

    Soma zaidi:

  10. Israel yasema ilimuua kamanda wa makombora wa Hezbollah

    Jeshi la Israel limesema kuwa lilimuua kamanda wa kitengo cha makombora cha Hezbollah kusini mwa Lebanon, aliyetajwa kwa jina la Muhammad Ali Ismail, na naibu wake, Hussein Ahmad Ismail, katika shambulio la anga.

    Ali Ismail alikuwa nyuma ya mashambulizi "mengi" dhidi ya Israel, ilisema, "ikiwa ni pamoja na kurusha makombora kuelekea eneo la Israel na lile lililorushwa uso kwa uso kuelekea eneo la kati la Israel siku ya Jumatano".

    Hakuna maelezo zaidi ya shambulizi hilo yaliyotolewa.

    Picha zinaonyesha mashambulizi makali ya Beirut

    Tazama baadhi ya picha za milipuko mikubwa huko Beirut, huku mashambulizi ya anga ya Israel yakiendelea.

    Watu waliokimbia makazi yao kutoka Dahieh na kusini mwa Lebanon sasa wako kwenye mitaa ya katikati mwa jiji:

    Soma zaidi:

  11. Kiongozi wa Hezbollah alengwa katika mashambulizi ya anga ya Israel

    Karibu tukujuze kuhusu kile kinachoendelea katika taarifa zenye uhusiano na mashambulizi ya Israel hasa kilichotokea usiku kucha.

    Israel imemlenga kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah katika mfululizo wa mashambulizi makubwa ya anga huko Beirut siku ya Ijumaa, afisa wa Marekani aliambia mshirika wa BBC, CBS News.

    Hata hivyo, afisa wa Israel alisema ni mapema mno kusema kama Nasrallah ameshambuliwa.

    Afisa huyo wa Marekani pia alisema Washington "haina dalili" zozote zinazoonyesha hatima ya Nasrallah.

    Shambulio la anga limeshambulia majengo kadhaa huko Dahieh, ngome ya Hezbollah kusini mwa mji huo.

    Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) alisema shambulizi "sahihi kabisa" limefanywa kwenye makao makuu ya Hezbollah.

    Katika sasisho lake la hivi punde, wizara ya afya ya Lebanon ilisema takriban watu sita wameuawa katika shambulizi la Ijumaa na 91 kujeruhiwa.

    Mashambulizi hayo ya anga yametokea baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutoa hotuba kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, ambapo aliapa kuendelea kuishambulia Hezbollah, licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano kwa muda.

    Ofisi yake siku ya Ijumaa ilisema anakatisha ziara yake ya New York na kurejea Israel.

    Mapema asubuhi ya leo, jeshi la Israel lilisema vikosi vyake vinashambulia maeneo ya Hezbollah huko Beirut, muda mfupi baada ya IDF kuwataka wakaazi katika vitongoji kadhaa vya kusini kuhama mara moja.

    Picha za usiku kucha zilionyesha moshi mwingi ukitanda kwenye anga ya Beirut, huku watu waliokimbia makazi wakitafuta hifadhi katika eneo la uwanja wa Martyr la mji mkuu.

    Soma zaidi:

  12. Bila shaka hujambo msomaji wetu, karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 28/9/2024