Hezbollah inamchaguaje kiongozi wake mpya baada ya kuuawa kwa Nasrallah?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Na Ithar Shalaby

BBC BBC Arabic

Kwa miaka 32 iliyopita, Hezbollah haijamjua kiongozi na katibu mkuu isipokuwa Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa Ijumaa iliyopita katika mashambulizi ya Israel yaliyolenga makao makuu ya chama hicho kusini mwa mji mkuu wa Lebanon Beirut.

Tangu 1992, Nasrallah amekuwa sura kuu ya chama, akishikilia wadhifa wa katibu mkuu wa tatu baada ya kuuawa kwa mtangulizi wake, Abbas al-Musawi.

Sasa kwa kuwa nafasi hii ni wazi, kazi ya kumchagua mrithi wa Nasrallah inaweza kuwa moja ya vipaumbele muhimu vya Hezbollah kwa wakati huu.

Ni utaratibu gani wa kumchagua Katibu Mkuu wa Hezbollah?

Kwa mujibu wa kanuni za ndani za chama, Katibu Mkuu mpya huchaguliwa baada ya kuchaguliwa na wajumbe wa kile kinachojulikana kama "Baraza la Shura," baraza lenye wajumbe saba, ambao kila mmoja anawajibika kwa jukumu maalum kwa chama.

Mwandishi wa masuala ya kisiasa Qassem Qasir analielezea kama "Baraza la Uamuzi la Shura." Qasir ameiambia BBC kwamba baraza la Shura ndilo linalochukua uongozi mkuu wa chama, na kwa kawaida huchaguliwa wakati wa mkutano mkuu, ambao unaundwa na makada na viongozi wa Hezbollah, na kwa muda mrefu hufanyika kila baada ya miaka mitatu.

Qasir anasema kuwa mkutano huo wa baraza hilo haujafanyika kwa miaka mingi kutokana na hali ya vita nchini Syria na Lebanon, na Nasrallah amechukua nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho.

Chini ya mwamvuli wa Baraza la Shura, chama hicho kina mabaraza makuu matano: Baraza Kuu, Baraza la Mahakama, Baraza la Bunge, Baraza la Siasa, na baraza la Jihad ambalo linahusika na shughuli za kijeshi za chama.

Wajumbe wa sasa wa Baraza la Shura ni wakuu wa mabaraza haya makuu.

Mbali na Katibu mkuu Hassan Nasrallah na mkuu wa baraza la Shura, ni pamoja na: Naim Qassem, naibu katibu mkuu wa chama; Mohammad Yazbek, mkuu wa baraza la mahakama; Ibrahim Amin al-Sayyed, mkuu wa baraza la siasa; Hashem Safi al-Din, mkuu wa halmashauri kuu na mgombea wa kwanza kuchukua nafasi ya Nasrallah; Hussein Khalil, msaidizi wa kisiasa wa Katibu Mkuu; na Mohammad Raad, mkuu wa baraza la bunge na mkuu wa Uaminifu kwa kambi ya upinzani, ambayo ni tawi la kisiasa la Hezbollah katika bunge la Lebanon.

Unaweza pia kusoma:

Qasir anatarajia kwamba Hezbollah haitafanya uchaguzi katika kipindi kijacho kumchagua Katibu mkuu mpya wa chama, na kwamba majukumu hayo yatapewa Naibu katibu mkuu wa chama hicho, Naim Qassem, hadi hali ya sasa ya vita itakapomalizika.

Sifa za katibu mkuu wa Hezbollah

Hezbollah iliundwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 kama kikundi cha kisiasa cha Kishia kilichoongozwa na viongozi wa dini ambao waliamini katika kujitolea kwao kwa kanuni ya "Uchungaji wa sheria ya Kiislam au Jurist," nadharia iliyoanzishwa na kiongozi mkuu wa Iran Ruhollah Khomeini kufuatia mapinduzi ya Kiislamu ya 1979. Kwa hiyo, moja ya sifa maarufu zinazohitajika kwa mtu ambaye angechukua urais wa halmashauri kuu ya Hezbollah ni kwamba lazima awe ni kiongozi wa dini.

Hii imethibitishwa na Ali Shukr, mtafiti katika mahusiano ya kimataifa katika kituo cha habari cha Kiarabu mjini Beirut, ambaye aliiambia BBC: "Wajumbe wote wa Baraza la Shura wana uwezo wa kuongoza chama, na kwa hivyo katibu mkuu lazima awe kiongozi wa kidini ambaye amekuwa na uzoefu wa kufanya kazi katika chama kwa kipindi cha muda na ambaye ana uwezo wa kutosha wa kimwili na kiakili wa kusimamia na kuongoza."

"Hali ya sasa nchini Lebanon inahitaji kuchagua mtu ambaye ana uwezo wa kusimamia mgogoro kwa busara, mwenye maono, na kwa usimamizi wa hali ya juu, na wakati huo huo kwa uamuzi," aliongeza Wissam Nassif, msomi na mtafiti katika mahusiano ya kimataifa. Nassif, ambaye amekuwa akifuatilia shughuli za Hezbollah kwa miaka mingi, ameiambia BBC.

"Kumchagua katibu mkuu mpya wa chama sio uamuzi rahisi kwasababu inahitaji kuchagua kiongozi ambaye ana uwepo tofauti na kiwango cha juu cha hekima." Nassif anaamini kuwa katibu mkuu mpya wa chama hicho anaweza kuchaguliwa katika kipindi kijacho, lakini suala hilo litategemea na hali ya ndani ya Baraza la Shura.

Alisema, "Mtu mpya anaweza kuchaguliwa bila kumtangaza wakati huu kwa hofu ya kulengwa na Israeli."

"Baraka za Iran" na uteuzi wa kiongozi mpya wa Hezbollah

Hezbollah, ambayo inatajwa kama kundi la kigaidi katika nchi kadhaa za Magharibi, wakati ikichukuliwa kama "kundi halali la upinzani" nchini Lebanon, inapata msaada mkubwa na ufadhili kutoka Iran. Kwa hivyo, waangalizi wanaamini kuwa uteuzi wa kiongozi mpya wa Hezbollah utafanyika kwa "baraka za Iran."

Kwa mujibu wa Ali Shukr, mtafiti katika mahusiano ya kimataifa, "wajumbe wa Baraza la Shura hawawezi kupata idhini ya Iran kwa maana halisi ya neno, bali ni pongezi na baraka," ikizingatiwa kuwa wajumbe wote wa baraza hilo tayari wamepokea idhini ya Iran kwa kujiunga na uongozi wa chama.

Hata hivyo, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Faisal Abdul Sater, ambaye yuko karibu na Hezbollah, hakubaliani na mtazamo huu, akiiambia BBC: "Uteuzi wa katibu mkuu mpya wa Hezbollah ni suala la ndani ya chama na hauna uhusiano wowote na Iran kwa njia yoyote," akibainisha kuwa wajumbe wa Baraza la Shura hapo awali walimchagua katibu kkuu Hassan Nasrallah baada ya kuuawa kwa Abbas al-Musawi, ambaye pia alichaguliwa na wajumbe wa baraza hilo.

Kwa hiyo anaashiria kwamba wanachama wa chama "watatumia tena utaratibu huo huo wa kumchagua katibu mkuu mpya, hata kama wakati wa sasa hauko sawa," lakini hatarajii itachukua muda mrefu kutekeleza hilo.

Mwaka 1992, katibu mkuu wa pili wa chama hicho, Abbas al-Moussawi, aliuawa, pamoja na mkewe na mtoto wake, baada ya helikopta za Israel kushambulia msafara wake wakati alipokuwa akirejea kutoka mji wa Jebchit, ambako alikuwa akishiriki katika maadhimisho ya miaka minane ya mauaji ya kiongozi Ragheb Harb, ambaye alichukuliwa kama sura ya upinzani kusini mwa Lebanon na karibu na Subhi al-Tufayli, akiwa ni katibu mkuu wa kwanza wa Hezbollah baada ya kuanzishwa kwake mwaka 1989.

Siku moja baada ya kuuawa kwa al-Moussawi, Baraza la Shura kwa kauli moja lilimchagua Hassan Nasrallah, wakati huo akiwa kijana wa miaka 32, kubaki madarakani hadi alipouawa na vikosi vya Israeli mnamo Septemba 27.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla