Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Licha ya kuikosoa Iran, Israel nayo ina nyuklia ya siri
Israel Inapolenga mpango wa nyuklia wa Iran, ina mpango wake wa nyuklia unaoendelea kwa mujibu wa gazeti New York Times.
Muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa taifa la Israel mwaka 1948, taifa hilo limekuwa na nia ya kujenga mpango wa nyuklia ili kujihakikishia uwepo wake.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel akizungumza kwenye meza yenye nembo ya Umoja wa Mataifa. Anaonekana kubeba ramani mbili, moja imeandikwa "Laana" na nyingine imeandikwa "Baraka."
Wataalamu wanaamini kuwa Israel imekuwa ikipanua mpango wake wa siri wa nyuklia.
Vita ambavyo Israel ilianzisha dhidi ya Iran vinalenga kuzuia mpango wake wa nyuklia, ambapo sehemu kubwa ya ulimwengu inatazama kwa hofu na wataalam wanasema ukuaji wake unaweza kutengeneza silaha ya atomiki ndani ya miezi kadhaa.
Israel ina mpango wake wa siri wa silaha za nyuklia, ambao hautambuliwi hadharani lakini, baadhi ya wataalam wanaamini, pia unapanuka.
"Kwa mtazamo rasmi wa kidiplomasia, Waisraeli hawatathibitisha au kukataa" silaha zao za nyuklia, alisema Alexander K. Bollfrass, mtaalamu wa usalama wa nyuklia katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati huko London.
Badala yake, Israel imesema haitakuwa nchi ya kwanza "kuanzisha" silaha za nyuklia Mashariki ya Kati. Maneno hayo yasiyoeleweka kimakusudi yanalingana na kile Bw. Bollfrass alichoita "utata juu ya kile ambacho ni wazi kuhusu mpango wa silaha za nyuklia."
Je, Israel ina silaha ngapi za kinyuklia?
Israel inaaminika kuwa na angalau vichwa 90 vya nyuklia vya kivita na nyenzo za kutosha kuzalisha hadi mamia zaidi, kulingana na kituo cha kudhibiti silaha na kuzuia kuenea kwa silaha na mpango wa Tishio la Nyuklia.
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, shirika linalosimamia nyuklia la Umoja wa Mataifa, limetathmini kuwa nchi 30 zina uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia lakini ni tisa pekee ndizo zinazofahamika kuwa nazo.
Israel ndiyo inayoshika nafasi ya pili kwa udogo kati ya tisa hizo, ikitanguliwa na Korea Kaskazini pekee, kulingana na kikundi cha utetezi kilichoshinda Tuzo ya Nobel, Kampeni ya Kimataifa ya Kukomesha Silaha za Nyuklia.
Israel inaweza kurusha vichwa vya kivita vya nyuklia kutoka kwa ndege za kivita, nyambizi au makombora ya ardhini, wataalam wanasema.
Israel ni moja ya nchi tano - ikijiunga na India, Pakistan, Korea Kaskazini na Sudan Kusini - ambayo haijasaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia Kuenea kwa Nyuklia.
Makubaliano hayo, ambayo yalianza kutekelezwa mwaka 1970, kwa ujumla yanazilazimisha serikali kuendeleza matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia.
(Iran imetia saini mkataba huo, ingawa Israel na mataifa yenye nguvu duniani yameishutumu Tehran kwa kukiuka kwa kurutubisha uranium kwa viwango vya juu vya kutosha kutengeneza silaha za nyuklia.)
Israel italazimika kuachana na silaha zake za nyuklia ili kutia saini mkataba huo, unaozitambua nchi tano pekee kuwa mataifa rasmi ya nyuklia: Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani - wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wote walikuwa wamelipua silaha ya nyuklia kufikia 1967, tarehe ya mwiaho kwa mkataba wa kuhitimu kuteuliwa.
Israel imekuwa na silaha za nyuklia kwa muda gani?
Viongozi wa Israel walikuwa na nia ya kujenga silaha za nyuklia ili kulinda uhai wa nchi hiyo mara tu baada ya kuanzishwa mwaka 1948 kufuatia mauaji ya Holocaust, rekodi za kihistoria zinaonyesha.
Tume ya Nishati ya Atomiki ya Israeli ilianzishwa mwaka wa 1952, na mwenyekiti wake wa kwanza, Ernst David Bergmann, anasema kwamba bomu la nyuklia litahakikisha "kwamba hatutaongozwa tena kama wana-kondoo kwenye machinjo," kulingana na Maktaba ya Kiyahud.
Israel ilianza kujenga eneo la kutengeneza silaha za nyuklia mwaka 1958, karibu na mji wa Dimona, kusini mwa Israel, watafiti wanaamini.
Ripoti ya hivi majuzi ya kijasusi ya Marekani kutoka Desemba 1960, na Kamati ya Pamoja ya Ujasusi ya Nishati ya Atomiki, ilisema kuwa mradi wa Dimona ulijumuisha mtambo wa kuchakata kwa ajili ya uzalishaji wa plutonium.
Ripoti hiyo ilihitimisha kuwa mradi huo unahusiana na silaha za nyuklia.
Je, Israel imewahi kutumia silaha zake za nyuklia katika vita?
Hapana.
Maktaba ya Kiyahudi ya Kiyahudi, ambayo inachukuliwa kuwa kati ya ensaiklopidia pana zaidi za Kiyahudi ulimwenguni, imetoa ripoti kwamba Israeli ilitayarisha mabomu yake ya nyuklia wakati wa vita vya Waarabu na Israeli vya 1967 na 1973, lakini silaha hizo hazikutumiwa.
Kumekuwa na ripoti chache katika kipindi cha miaka 50 iliyopita kwamba Israel imefanyia majaribio silaha zake za nyuklia katika maeneo ya chini ya ardhi, ikiwa ni pamoja na katika jangwa la Negev kusini mwa Israel.
Kipindi maarufu zaidi - na ambacho bado kinajadiliwa - kilikuwa mwezi Septemba 1979, wakati satelaiti ya Marekani iliyoundwa kugundua milipuko ya nyuklia iliripoti kuwaka mara mbili karibu na mahali ambapo bahari ya Atlantiki ya Kusini na Hindi hukutana.
Wanasayansi wengine waliamini kuwa mwanga huo uliwezekana kuwa ulitokana na jaribio la nyuklia, lililofanywa na Israel au Afrika Kusini, au pengine na zote mbili.
Je, Israel inatengeneza wapi silaha zake za nyuklia?
Inaaminika sana kuwa mpango wa silaha za nyuklia wa Israeli uko Dimona.
Wataalamu wanasema inaonekana kuwa wakaguzi kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki hawajawahi kufika katika eneo hilo, na kwamba hakuna makubaliano na Israel ambayo yangeruhusu shirika la Umoja wa Mataifa la kufuatilia suala hilo.
Wanasayansi wa Marekani walitembelea Dimona katika miaka ya 1960 na kuhitimisha kuwa mpango wa nyuklia huko ulikuwa wa amani, kulingana na ukaguzi unaozidi kuwa mdogo, rekodi za kihistoria zinaonyesha.
Lakini hakuna ushahidi wa umma kwamba wakaguzi wa Marekani wamerudi tangu wakati huo.
Picha za satelaiti zinaonyesha ujenzi mpya huko Dimona katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa uchache, wataalam walisema, kituo hicho kinafanyiwa uboreshaji unaohitajika.
Pia kuna imani inayoongezeka miongoni mwa baadhi ya wataalam kwamba Israel inajenga kinu kipya huko Dimona ili kuongeza uwezo wake wa nyuklia. Ripoti iliyotolewa wiki hii na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm ilisema Israel inaonekana kuboresha eneo la kinu ili kuzalisha plutonium, ambayo inaweza kutumika kwa silaha za nyuklia na baadhi ya malengo ya amani, kama vile angani.
Kwa sababu ya usiri wake, Dimona kwa muda mrefu imekuwa ishara ya kuvutia na, kwa wengine, hasira juu ya mpango wa silaha za nyuklia wa Israeli.
Katika tukio nadra la umma kwenye eneo hilo 2018, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israeli aliitumia kama uwanja wa nyuma kuwaonya maadui kwamba "wale wanaotishia kutufuta katika ramani wanajiweka katika hatari kama hiyo - na kwa hali yoyote hawatafikia lengo lao."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla