Kwanini Singapore inathamini wingi na ubora wa maisha?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Lindsey Galloway
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Linapokuja suala la kuishi kwa muda mrefu, maeneo machache ulimwenguni yameshuhudia ongezeko kubwa kuishi kwa muda mrefu kama vile kisiwa cha Asia kusini mashariki.
Mtoto aliyezaliwa nchini Singapore mwaka 1960 alitarajiwa kuishi hadi umri wa miaka 65, lakini mtoto anayezaliwa leo anatarajiwa kuishi zaidi ya miaka 86 kulingana na makadirio. Aidha, idadi ya wazee wa miaka 100 na zaidi nchini Singapore iliongezeka mara mbili kati ya 2010 na 2020.
Ongezeko hili kubwa la umri wa maisha limetokana kwa kiasi kikubwa na sera za serikali zilizolenga kuboresha afya ya jamii. Hata hivyo, ufanisi huu ulitosha kuitambua Singapore kama taifa ambalo lina watu wanaoishi muda mrefu wakiwa na afya na kuorodheshwa ya sita duniani mnamo Agosti 2023.
Maeneo haya yaliyo na watu wanaoishi muda mrefu yaligunduliwa na mwandishi wa habari wa jarida la National Geographic, Dan Buettner, ambaye alitaja maeneo ambako watu wanaishi maisha marefu na wenye afya, kutokana na mafungamano ya utamaduni, mtindo wa maisha, lishe, na ushirikiano wa jamii.
Singapore ilikuwa eneo la kwanza kujumuishwa katika maeneo ya watu wanaoishi kwa muda mrefu kwa karne tisa inayojulikana kama ‘blue zone 2,0 by Buettner’ na inatofautiana na Blue Zones nyingine kwa sababu kuishi sana kwa wakazi wake kumechangiwa zaidi na sera za kisasa kuliko tamaduni za jadi zinazopatikana katika jamii nyingine kama vile Ugiriki na Costa Rica.
Sio tu kuishi kwa muda mrefu tubali pia ubora wa maisha ambao wakazi wa Singapore wanathamini.
Tulizungumza na baadhi yao ili kuelewa ni sera na mbinu zipi zinachangia katika kufanya maisha yao kuwa bora na yenye furaha, na wanavyoshauri kwa wengine wanaotaka kuishi hapa kwa matumaini ya maisha marefu.
Ubora wa hali ya afya

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia wa Singapore wameshuhudia mabadiliko ya sera za serikali ambazo zinaathiri afya na ubora wa maisha.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
‘'Kuishi hapa, nimeona mabadiliko ya hali ya afya,'' amesema mkazi anayeitwa Firdaus Syazwani, ambaye hufanya ushauri wa fedha kwenye blogu inayofahamika Dollar Bureau.
"Kuongezwa kwa ushuru ya sigara na pombe zikiambatana na kupigwa marufuku kwa kuvuta sigara hadharani inaboresha afya ya mtu na pia inaleta mazingira mazuri ya umma,na kufanya iwe safi na kuridhisha.Huwezi kupata moshi wa aina nyingine!”
Alishangazwa kujua Singapore ni eneo la watu wanoishi kwa muda mrefu, ingawa alifahamu wanatumia sana sukari, chumvi na tui la nazi kwa vyakula vyao vya asilia. Lakini hayo yanabadilika japo kwa kujikokota kwasababu ya sera .
"Kutokana na upendeleo wa vyakula vya kienyeji, bodi ya kuboresha afya ina kampeini za kuhamasisha umuhimu wa vyakula vilivyo na viritubisho kwa wakaazi,”alieleza.
“Hatua kama vile kuweka alama za kuonyesha lishe kwenye bidhaa na kupunguza sukari kwenye vinywaji kumekuza ufahamu wa afya na chaguo bora za kiafya. Ingawa bado haijulikani ni kwa kiasi gani hatua hizi zitafaulu, mimi binafsi hutafuta vinywaji visivyo na sukari nione alama hizo,”alisema Firdaus.
Mfumo wa afya wa Singapore umepigiwa upatu ulimwenguni kwa ubora na pia gharama yake ya nafuu.
Mfumo unaotathmini nchi juu ya uendelezaji wa wakazi wake kustawi, unaoakisi ustawi wa kiuchumi na kijamii 2023 iliiweka nchi hiyo kama bora duniani kwa afya ya wananchi wake na upatikanaji wa huduma za afya.
Nchi hii inatoa huduma za afya za kimataifa, lakini pia ina mchanganyiko wa huduma za kibinafsi na mifuko ya akiba kusaidia kulipa gharama za matibabu ya kibinafsi.
Kipaumbele kwa maeneo ya kupumzika
Lakini si huduma za afya pekee zinazochangia maisha marefu ya wakazi.
Sera nyingine kama vile usafiri wa umma unaohamasisha kutembea na kufanya mazoezi kila siku, pamoja na juhudi za kuhakikisha nchi inakuwa safi na nzuri, huwapa wakazi hali ya usalama na utulivu.

Chanzo cha picha, Getty Images
“Mipango ya serikali inayoipa kipaumbele kuunganisha bustani, mabonde, na hifadhi za asili kwenye mandhari ya jiji imeifanya Singapore kuwa maarufu kama ‘jiji la bustani’,” alisema mshirika mkuu katika safdie architects ,Charu Kokate, ambaye pia aliongoza miradi maarufu kama Sky Habitat Residential Towers na Jewel Changi Airport.
“Baada ya kuishi Singapore kwa zaidi ya miaka 15, ninatamaushwa kila wakati na jinsi Idara ya Upangaji wa Miji ilivyoipanga miji hii kwa umakini.
Kipaumbele chao kwa uendelevu, matumizi bora ya ardhi, na kujumuisha maeneo ya kijani katika miji ni cha kipekee.”
Maeneo anayopendelea kuzuru ni bustani ya botanic Singapore.iliyoko katikati mwa jiji ,ikiwa ni bustani lililoko nchi za joto kutambuliwa kama turathi ya kitaifa na UNESCO.
"Bustani ya maua na uhifadhi wa mimea ni mahali pazuri kwa wapenda asili, familia, na watalii wanaotafuta amani na utulivu,” alisema.
Bustani za umma pia hutumika kama kitovu cha jamii, jambo ambalo watafiti wote wanaofuatilia nadharia ya kuishi kwa muda mrefu wanakubaliana kuwa ni muhimu kwa maisha marefu na yenye afya.
“Kuanzia vijana hadi wazee, utapata idadi kubwa ya watu wanaojihusisha na mazoezi ya kila mara, kwa msaada wa bustani kubwa za umma, maeneo ya mazoezi, na madarasa ya mazoezi yanayopatikana kirahisi katika jiji zima,” alisema Syazwani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa wale wanaofikiria kuhamia hapa,kukumbatia uelewa na mtindo wa Maisha ni muhimu.
Anapendekeza East Coast Park, ufukwe wa bahari ambao unatoa nafasi nyingi za kuzuru na kutembea huku ukifurahia upepo wa bahari.
Ni kipi unapaswa kujua?
Ingawa ubora wa maisha unaweza kuwa wa juu Singapore, ni gharama kubwa kuishi hapa.
Nchi hii mara nyingi inaorodheshwa ya pili kama moja ya maeneo ghali zaidi ya kuishi duniani, Mercer ikiifanya kuwa ya pili baada ya Hong Kong.
Ingawa watu wanatofautiana, na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani wanahamia hapa, serikali inalenga kuimarisha mshikamano wa kijamii, ikitekeleza sheria na kanuni.
Nchi ina sheria kali na adhabu dhidi ya kutupa taka, uvutaji sigara hadharani, dawa za kulevya, na hata kuvuka barabara kinyume cha sheria, lakini wakazi wengi wanakubaliana kuwa masharti haya husaidia kufanya nchi kuwa salama na nzuri kuishi.
“Sera za serikali zimepangwa kwa umakini kulingana na mahitaji ya wananchi, zikilenga kuboresha ubora wa maisha kwa jumla, kusaidia ustawi wa kiuchumi, na kudumisha mshikamano wa kijamii,” alisema Kokate.
“Utulivu wa kisiasa wa Singapore unachukua nafasi muhimu katika kukuza mazingira yanayochochea uwekezaji wa biashara, ukuaji wa uchumi, na mshikamano wa kijamii.”

Chanzo cha picha, Getty Images
“Jiji hili lina kitu kwa kila mtu, bila kujali umri,” alisema Kokate. “Jamii ya kitamaduni inasherehekea aina mbalimbali za tamaduni, ikiifanya kuwa na utamaduni wa kipekee ambao unaboreshwa kwa wageni na wahamiaji.”
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












