Hizi ndizo saa za mwisho za Papa zilivyokuwa

Muda wa kusoma: Dakika 5

Adhuhuri ya Jumatatu, kengele za kanisa kote Italia zilianza kulia. Papa Francis alipoteza maisha.

Haikupita hata saa 24 tangu ajitokeze kwa kushtukiza kwenye roshani inayotazama St Peter's Square, akiwabariki watu 35,000 waliokusanyika kusherehekea Pasaka huko Vatican.

Papa alikuwa akipumua peke yake, bila mirija ya oksijeni, licha ya kuambiwa na madaktari wake kutumia miezi miwili kupata nafuu baada ya siku 38 hospitalini akiwa na homa ya mapafu mara mbili.

Zaidi ya wiki mbili zilizopita Papa Francis alikuwa amefanya kile ambacho alikuwa akifanya siku zote, alipokea wageni na alikutana na watu kutoka kila nyanja ya maisha.

Alipotokea Jumapili ya Pasaka, umati wa watu uliokuwa chini ulilipuka kwa shangwe ; kisha umati ukanyamaza.

"Wapendwa, ninawatakia Pasaka njema," alisema, sauti yake ikiwa nzito akitia juhudi.

Yalipaswa kuwa maneno yake ya mwisho hadharani.

Unaweza kusoma

"Nadhani watu wanaweza kuhisi kitu- kana kwamba wangeweza kusema ilikuwa mara ya mwisho kumwona," alisema Mauro, mkazi wa Roma ambaye alikuwa katika Uwanja wa St Peter's kwa ajili ya Misa ya Pasaka na sasa alikuwa amerejea kutoa heshima zake.

"Kwa kawaida kila mtu hupiga kelele 'Uishi muda mrefu Papa!'... wakati huu palikuwa kimya kuliko kawaida, labda kulikuwa na heshima zaidi kwa mateso aliyokuwa akiyapitia."

"Alitubariki lakini sauti yake ilikuwa ikikwaruza," mwanaume mmoja anayeitwa Alberto aliiambia BBC. "Nadhani alikuwa anatupa kwaheri yake ya mwisho."

Madaktari waliomtibu Francis katika hospitali ya Gemelli ya Roma walikuwa wameagiza utaratibu wa kupumzika kabisa, lakini haikuwa ikiwezekana kwamba Papa ambaye alitumia muda mwingi wa upapa kukutana na watu angeendelea hivyo.

Francis alikuwa tayari ameweka wazi kuwa anataka kurejea Vatikani kwa wakati kwa ajili ya Pasaka, mara tu wataalamu wanaomhudumia walipoeleza kuwa masuala yake ya kiafya hayangetatuliwa haraka.

Kwa Wakristo, Pasaka ni muhimu zaidi kuliko Krismasi kwani inaashiria kanuni ya msingi ya imani yao, ufufuo wa Kristo, siku tatu baada ya kupigwa misumari msalabani.

Kabla ya kuruhusiwa tarehe 23 Machi, Francis alipungia mkono umati wa watu kutoka hospitalini pia, na kisha akarejea kwenye makazi yake katika nyumba ya wageni ya Casa Santa Marta aliyokuwa amejenga.

Timu yake ya matibabu ilisema alichohitaji ni oksijeni tu, na kupona huko kulikuwa bora kuliko hospitali ilivyo na maambukizi.

Pasaka ilikuwa imesalia wiki tatu tu na, ilipokaribia, ratiba ya Papa ilizidi kuwa na shughuli nyingi.

Alikutana na Mfalme Charles na Malkia Camilla kwenye ukumbi wa Casa San Marta na kisha akaonekana kwenye roshani ya Vatican kwa Jumapili ya mitende siku nne baadaye tarehe 13 Aprili, akichanganyika na umati wa watu 20,000 katika St Peter's Square, kinyume na ushauri wa madaktari.

Lakini kwa Papa, Pasaka ilikuwa wakati muhimu kuliko nyakati zote.

Alhamisi iliyopita, kama alivyokuwa amefanya mara nyingi hapo awali na kama alivyokuwa akifanya katika nchi yake ya asili ya Argentina kabla ya kuwa Papa, alitembelea jela ya Regina Coeli huko Roma ambako alitumia nusu saa kukutana na wafungwa na alipokelewa kwa makofi na wafanyakazi na walinzi alipokuwa akiwasili kwa kiti cha magurudumu.

Katika miaka iliyotangulia alikuwa ameosha miguu ya wafungwa, akionesha yale ambayo Yesu inasemekana kuwa alifanya pamoja na wanafunzi wake usiku uliotangulia kifo chake.

"Mwaka huu siwezi kufanya hivyo, lakini ninaweza na nataka bado kuwa karibu na ninyi," alisema kwa sauti dhaifu kwa makumi ya wafungwa waliokuja kumuona, na ambao walimshangilia alipokuwa akizunguka jela.

"Tuna bahati sana. Walio nje hawapati kumuona na sisi tunaona," mtu mmoja aliviambia vyombo vya habari vya Italia.

Alipokuwa akitoka gerezani, Francis aliulizwa na mwandishi wa habari jinsi atakavyofurahia Pasaka mwaka huu.

"Kwa njia yoyote naweza," alijibu.

Na, Jumapili, alitimiza ahadi yake.

Alifanya mkutano mfupi na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance kabla ya kufika mbele ya umati wa watu katika uwanja wa St Peter's huku umati wa watu waliokuwa chini wakipiga kelele kwa furaha.

Alitoa baraka yake ya mwisho - anwani ya Urbi et Orbi kwa Kilatini, ikimaanisha "kwa jiji na kwa ulimwengu". Kisha, Askofu Mkuu Diego Ravelli alisoma hotuba iliyoandikwa na Papa Francis alipokuwa ameketi kimya kando yake.

Kisha, kwa mshangao wa kila mtu, alishuka hadi St Peter's Square, ambako alisukumwa na gari la papa lililokuwa wazi juu - Mercedes-Benz ndogo nyeupe inayotumiwa na mapapa kukutana na umati.

Kamera ilimfuata huku akiinua mkono wake kuwabariki waumini waliokuwa kwenye uwanja wa jua, na watoto wachache waliletwa karibu naye. Ilikuwa mara ya mwisho dunia kumuona akiwa hai.

Kutazama baraka za Francis siku ya Jumapili, Alberto kutoka Roma alihisi hatadumu zaidi, ingawa kifo cha Papa bado kilikuja kama mshtuko.

"Sikujisikia furaha kumuona, niliweza kusema alikuwa anaumwa," alisema. "Lakini ilikuwa ni heshima kumuona mara ya mwisho."

Francis alikufa mapema Jumatatu katika nyumba yake pendwa ya Casa Santa Marta - makazi ya vyumba 100 vya kawaida, vinavyoendeshwa na watawa na wazi kwa mahujaji na wageni.

Zaidi ya saa mbili baadaye, kadinali chamberlain, au camerlengo, alisimama katika Casa Santa Marta na kutangaza habari hiyo hadharani.

Vatican ilisema Jumatatu jioni alikufa kwa kiharusi na kwa moyo kushindwa kufanya kazi.

Katika siku zijazo, makadinali kutoka kote ulimwenguni watakaa Casa Santa Marta wanapokusanyika Roma kwa mkutano ambao utamchagua mrithi wa Francis.

Nje, katika mwanga mkali wa jua katika Uwanja wa St Peter's, watu walichanganyika na mapadre chini ya basilica ya kuvutia.

Kundi la watawa waliovalia kijivu na nyeupe walimkazia macho mwanaume ambaye, akiwa na vipokea sauti vya masikioni, alikuwa akicheza kuzunguka uwanja. "Hakuna heshima," walisema.

Skrini zile zile kubwa zilizotangaza baraka za Papa kwa Pasaka sasa zilionesha picha ya Francis akitabasamu na notisi kwamba rozari maalum ilikuwa ikifanyika kwa ajili yake saa 12 baada ya kifo chake.

Iliwaruhusu Wakatoliki walio karibu na walio mbali kumwombea Papa wao na kumshukuru kwa kusherehekea Pasaka ya mwisho pamoja nao.