Francis: Papa kutoka Amerika ya Kusini ambaye alilibadilisha Kanisa Katoliki

Muda wa kusoma: Dakika 7

Mwaka 2013 Francis alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika na kutoka Ulimwengu wa Kusini. Alimrithi Benedict XVI, ambaye alifariki mwaka 2022. Benedict XVI alikuwa Papa wa kwanza kustaafu kwa hiari baada ya takribani miaka 600.

Papa Francis jina lake kamili ni Jorge Mario Bergoglio, alikuwa Kardinali wa Argentina, na alikuwa na umri wa miaka sabini alipokuwa Papa mwaka 2013.

Bergoglio aliwavutia wahafidhina juu ya mtazamo wake kwa masuala ya mahusiano, huku akiwavutia wanamageuzi kwa msimamo wake wa kiliberali juu ya haki za kijamii.

Lakini ndani ya urasimu wa Vatikani baadhi ya majaribio ya Francis ya kuleta mageuzi yalikumbana na upinzani, lakini alibaki kuwa maarufu miongoni mwa wanamapokeo.

Historia ya Papa Francis

Kuanzia wakati wa kuchaguliwa kwake, Francis alionyesha kuwa atafanya mambo tofauti. Aliwapokea makadinali wake kwa njia isiyo rasmi ya kusimama - badala ya kuketi kwenye kiti cha enzi cha upapa.

Tarehe 13 Machi 2013, Papa Francis alijitokeza kwenye roshani inayoangalia bustani ya St Peter's Square.

Akiwa amevalia mavazi meupe, alipewa jina jipya ambalo lilimtukuza Mtakatifu Francis wa Assisi, aliyekuwa mhubiri wa Karne ya 13 na mpenda wanyama.

Papa mpya aliweka misheni ya maadili kwa wafuasi bilioni 1.2 wa kanisa lake. "Oh, napendelea Kanisa maskini, na kwa watu maskini," alisema.

Jorge Mario Bergoglio alizaliwa huko Buenos Aires, Argentina, tarehe 17 Desemba 1936 – yeye ni mtoto mkubwa kati ya watoto watano. Wazazi wake walikimbia nchi yao ya asili ya Italia ili kuepuka maovu ya ufashisti.

Alipenda mchezo wa tango (ngoma ya asili ya Argentina) na akawa shabiki wa klabu yake ya soka ya mtaani ya, San Lorenzo.

Alipona baada ya kuugua nimonia, na kufanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu ya pafu lake. Na hilo lilimuacha katika hatari ya kuambukizwa katika maisha yake yote.

Akiwa mzee pia alipatwa na maumivu kwenye goti lake la kulia, ambayo aliyataja kuwa ni "unyonge wa kimwili."

Bergoglio akiwa kijana alifanya kazi kama mlinzi wa klabu ya usiku na kufanya kazi ya ufagiaji, kabla ya kuhitimu chuo kama mwanakemia.

Alifanya kazi katika kiwanda cha ndani na Esther Ballestrino, mwanaharakati aliyefanya kampeni dhidi ya udikteta wa kijeshi wa Argentina. Mwanamke huyo alitekwa, akapotea na hakupatikana tena.

Akawa Mjesuti, akasoma falsafa na kufundisha fasihi na saikolojia. Alitawazwa muongo mmoja baadaye, na kuwa mkuu wa mkoa wa kanisa hilo nchini Argentina 1973.

Tuhuma

Wengine wanaamini alishindwa kusema vya kutosha kupinga majenerali wa utawala katili wa kijeshi wa Argentina.

Vilevile, alituhumiwa kuhusika katika utekaji nyara wa makasisi wawili wakati wa vita vibaya vya Argentina, kipindi ambacho maelfu ya watu waliteswa au kuuawa, au kutoweka, kutoka 1976 hadi 1983.

Mapadre hao waliotekwa na jeshi, waliteswa lakini hatimaye wakapatikana wakiwa hai - wakiwa hawajifahamu na wakiwa nusu uchi.

Lakini tuhuma za kuhusika alizikanusha, akisisitiza kuwa alifanya kazi nyuma ya pazia ili waachiliwe.

Alipoulizwa kwa nini hakuzungumza, kukemea utawala wa kijeshi, alisema hali ilikuwa ngumu sana. Kwa kweli - akiwa na umri wa miaka 36 - alijikuta katikati ya machafuko ambayo yangemtikisa hata kiongozi mwenye uzoefu. Hakika aliwasaidia wengi waliojaribu kuikimbia nchi hiyo.

Ujumbe wa Amani

Alikuwa Askofu Msaidizi huko Buenos Aires mwaka 1992 na kisha akawa Askofu Mkuu.

Papa Yohane Paulo II alimteua kuwa kardinali mwaka 2001 na akachukua nyadhifa katika utumishi wa umma wa Kanisa.

Katika mahubiri yake, alitoa wito wa umoja katika jamii na kukosoa serikali ambazo zilishindwa kuwapa kipaumbele watu maskini zaidi katika jamii.

Akiwa Papa, alifanya juhudi kubwa kuponya mpasuko wa miaka elfu moja na Kanisa la Othodoksi la Mashariki.

Francis alifanya kazi na Waanglikana, Walutheri na Wamethodisti na kuwashawishi marais wa Israeli na Palestina kuungana naye kuombea amani.

Baada ya mashambulizi ya wapiganaji wa Kiislamu, alisema si sawa kuuhusisha Uislamu na vurugu.

Kama Mmarekani wa Kusini anayezungumza Kihispania, alihusika kama mpatanishi wakati serikali ya Marekani ilipoelekea kwenye maelewano ya kihistoria na Cuba. Ni vigumu kufikiria Papa wa Ulaya kuhusika katika jukumu muhimu kama hilo la kidiplomasia.

Misimamo ya jadi

Alisema Kanisa linapaswa kuwakaribisha watu bila kujali mwelekeo wao wa kijinsia, lakini akasisitiza watu wa mapenzi ya jinsia moja kuasili watoto ni aina ya ubaguzi dhidi ya watoto.

Kulikuwa na mjadala baada ya kukubali aina fulani ya miungano ya jinsia moja kwa wanandoa wa jinsia moja, lakini Francis hakukubali kuiita ndoa. Akisema, litakuwa ni "jaribio la kuharibu mpango wa Mungu."

Muda mfupi baada ya kuwa Papa 2013, alishiriki katika maandamano ya kupinga uavyaji mimba huko Roma - akitoa wito wa haki za kuishi za watoto ambao hawajazaliwa "tangu wakati wa kutungwa mimba."

Ingawa alionekana kuruhusu uzazi wa mpango kutumika kuzuia magonjwa, lakini alisifu mafundisho ya Paul VI juu ya jambo hilo - ambaye alionya linaweza kuwafanya wanawake kuwa vyombo vya starehe kwa wanaume.

Mwaka 2015, Papa Francis aliiambia hadhira nchini Ufilipino kwamba uzazi wa mpango unahusisha "kuharibiwa familia kwa kuinyima watoto." Sio ukosefu wa watoto ambao aliona kuwa unadhuru, lakini ni uamuzi wa makusudi wa kutozaa.

Kukabiliana na unyanyasaji

Changamoto kubwa zaidi kwa Papa; ni kutoka kwa wale wanaomtuhumu kushindwa kukabiliana na unyanyasaji wa watoto na kutoka kwa wakosoaji wa kihafidhina ambao walihisi alikuwa akiidhoofisha imani hiyo. Hasa, kwa kuruhusu Wakatoliki kutalakiana na waliooa tena washiriki Ushirika.

Wahafidhina pia walilichukua suala la unyanyasaji wa watoto kama silaha katika kampeni yao ya muda mrefu.

Agosti 2018, Askofu Mkuu Carlo Maria Viganò, aliyekuwa Balozi wa Kitume nchini Marekani, alichapisha nyaraka ya kurasa 11. Inayoelezea mfululizo wa maonyo yaliyotolewa kwa Vatikani kuhusu tabia ya kadinali wa zamani, Thomas McCarrick.

Ilidaiwa kuwa McCarrick alikuwa mnyanyasaji ambaye aliwashambulia watu wazima na watoto. Askofu Mkuu Viganò alisema, Papa alimfanya McCarrick kuwa mtoa ushauri anayeaminika" licha ya kujua kuwa alikuwa muovu. Suluhu lilikuwa wazi, alisema: Papa Francis anapaswa kujiuzulu.

Mzozo huu ulitishia kulimeza Kanisa. Hatimaye McCarrick aliachishwa kazi Februari 2019, baada ya uchunguzi wa Vatikani.

Kuhimiza amani

Wakati wa janga la Covid, Francis alighairi kuonekana kwake mara kwa mara katika bustani ya St Peter's Square - kuzuia virusi kuenea. Katika mfano muhimu wa uongozi, pia alitangaza chanjo ni wajibu wa wote.

2022, alikuwa Papa wa kwanza kwa zaidi ya karne moja kumzika mtangulizi wake - baada ya kifo cha Benedict akiwa na umri wa miaka 95.

Wakati huo pia, alikuwa na shida zake za kiafya - na kulazwa hospitalini mara kadhaa. Lakini Francis alidhamiria kuendelea na juhudi zake za kukuza amani ya kimataifa na mazungumzo baina ya dini.

2023, alihiji Sudan Kusini, akiwasihi viongozi wa nchi hiyo kumaliza migogoro.

Alitoa wito wa kukomeshwa "vita vya kikatili" nchini Ukraine, ingawa aliwakatisha tamaa Waukraine kwa kuonekana kumeza ujumbe wa propaganda wa Urusi kwamba Ukraine ilichochea vita.

Jorge Mario Bergoglio alifika kwenye kiti cha enzi cha St Peter kwa nia ya kukibadilisha. Laini kutakuwa na wakosoaji watakaoonyesha udhaifu wake katika kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia wa makasisi.

Lakini pia alileta mabadiliko. Aliwateua zaidi ya makadinali 140 kutoka nchi zisizo za Ulaya na kulifanya Kanisa lenye mtazamo wa kimataifa zaidi kuliko ule aliourithi.

Alikuwa ni Papa aliyechagua kutoishi katika Jumba la Mitume la Vatikani - lakini aliishi katika jengo la karibu (ambalo Papa John Paul II alilijenga kama nyumba ya wageni).

Pia alidhamiria kuitikisa taasisi yenyewe, kwa kuimarisha kazi ya kihistoria ya Kanisa kwa kukata migogoro ya ndani, na kuawalenga maskini na kulirudisha Kanisa kwa watu.

"Kama ningelazimika kuchagua kati ya Kanisa lililojeruhiwa ambalo linakwenda mitaani na Kanisa lililo na wagonjwa, lililojitenga, ningechagua la kwanza," alisema baada tu ya kuchukua wadhifa huo.