Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Carlo Maria Viganò, askofu mkuu mkosoaji wa Papa Francis ambaye alitengwa na Vatican ni nani?
Na Ian Aikman
Role,BBC News
Askofu Mkuu wa Italia Carlo Maria Viganò, mkosoaji mkubwa wa Papa Francis, alitengwa na Vatican, ofisi ya mafundisho ya Kanisa iliripoti Ijumaa wiki hii.
Kasisi huyo mwenye umri wa miaka 83 alipatikana na hatia ya mifarakano - ikimaanisha kuwa amejitenga na Kanisa Katoliki - baada ya miaka mingi ya makabiliano makali na papa.
Viganò, ambaye ni mhafidhina mwenye misimamo mikali , alikuwa ametoa wito wa kujiuzulu kwa Papa, akimtuhumu kwa uzushi na kukosoa misimamo yake kuhusu uhamiaji, mabadiliko ya hali ya hewa na wapenzi wa jinsia moja.
"Huku kwa waumini wa kanisa ni Moja la Katoliki na la Kitume, kwa Bergoglio Kanisa ni la umoja, la sinodi, linajumuisha, wahamiaji, linalohifadhi mazingira na rafiki wa wapenzi wa jinsi moja," aliandika katika taarifa yake ndefu iliyochapishwa tarehe 28, Juni.
"Sitambui mamlaka ya mahakama inayonuia kunihukumu, wala mkuu wake, wala yeyote aliyeiteua," aliongeza.
Askofu mkuu alikuwa kiongozi mkuu katika Kanisa na alihudumu kama mjumbe wa papa huko Washington kutoka 2011 hadi 2016.
Mnamo 2018 alijificha baada ya kudai kuwa Papa alifahamu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa na kadinali wa Marekani na hakuchukua hatua.
" Papa Francis lazima awe wa kwanza kuwa mfano mzuri kwa makadinali na maaskofu ambao walificha dhuluma za [Theodore] McCarrick na kujiuzulu pamoja ," alisema kisha.
Vatican ilikataa shtaka hilo na tangu wakati huo, Viganò hakuonekana tena.
Baada ya muda, askofu mkuu alijihusisha na wananadharia wa njama wa Marekani , akikosoa chanjo za Covid na akidai kuwepo kwa mradi wa "wa kimataifa" na ["anti-Christian" wa kupinga Kristu] wa Umoja wa Mataifa na makundi mengine.
Ofisi ya mafundisho ya Vatcan imesema kukataa kwake kumheshimu Papa Francis kuliwekwa wazi katika taarifa zake kwa umma.
"Monsignor Carlo Maria Viganò alipatikana na hatia ya uhalifu uliohifadhiwa [ukiukaji wa sheria] wa mifarakano ," taarifa hiyo ilisema, na kuongeza kuwa kutengwa "kumetangazwa."
Kutengwa kutamzuia Viganò kutimiza kazi yoyote ya kikanisa na kupokea sakramenti.
"Kashfa, makosa na uzushi wa Bergoglio"
Askofu mkuu alijibu uamuzi huo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuchapisha kiunganishi (link) ya amri ambayo ilitumwa kwake kwa barua pepe.
"Nilichodaiwa kuwa na hatia kwa kuhukumiwa kwangu sasa kimerekodiwa, kikithibitisha imani ya Kikatoliki ninayokiri kikamilifu," aliandika.
Viganò alikuwa ameshutumiwa kwa ubaguzi na kukana uhalali wa Papa mwezi uliopita.
Wakati huo, aliandika katika X kwamba aliona mashtaka dhidi yake kama "heshima."
"Ninakataa, nakataa na kulaani kashfa, makosa na uzushi wa Jorge Mario Bergoglio ," alisema, akitumia jina la kidunia la Papa wa Argentina.
Papa Francis amekabiliana na Wakatoliki wahafidhina kwa kufanya mabadiliko kuhusu jumuiya ya wapenzi wa jinsi moja ( LGBT+), kutetea haki za wahamiaji na kulaani ubepari "usiozuilika".
Mwaka jana, Francis alichukua hatua dhidi ya mkosoaji mwingine wa kihafidhina, Askofu Joseph E. Strickland wa Texas, ambaye alimfuta kazi alipokataa kujiuzulu baada ya uchunguzi.
Carlo Maria Viganò ni nani?
Alizaliwa Varese, Italia, mwaka wa 1941 na kutawazwa kuwa kasisi akiwa na umri wa miaka 27.
Anajulikana kuwa mshirika wa wale wanaoitwa makadinali wa "dubia" , ambao wamepinga hadharani Papa Francis kwa "uongozi wake usio rasmi."
Viganò ana udaktari katika Sheria ya Kiraia na Kanuni. Anazungumza Kiitaliano, Kifaransa, Kihispania na Kiingereza.
Alijiunga na huduma ya kidiplomasia ya Vatcan mwaka 1973 na alitumwa kwa ujumbe wa upapa nchini Iraq na Uingereza. Akiwa na umri wa miaka 51, mwaka wa 1992, alitawazwa kuwa askofu .
Alishikilia nyadhifa muhimu ndani ya Kanisa Katoliki, kama vile ubalozi wa kitume nchini Nigeria (1992-2009) chini ya mamlaka ya John Paul II, na katibu mkuu wa gavana wa Vatican City (2009-2011).
Katika jukumu hili la mwisho alikua mmoja wa mapadre walio karibu na Papa Benedict XVI .
Mnamo 2010, televisheni ya Italia ilichapisha hati za siri zilizoelekezwa kwa Benedict.
Uvujaji huo mkubwa uliitwa VatiLeaks na ulikuwa na barua kutoka kwa Viganò zilizotumwa kwa papa ambapo alishutumu "ufisadi, ubadhirifu na usimamizi mbovu" katika u Vatican na ufichaji wa baadhi ya wanachama wake baada ya kile kilichoelezewa kama kupata upungufu wa dola milioni.
Mnamo mwaka wa 2014, mtawa huyo wa zamani pia alikuwa kiiini cha mabishano pale alipoamuru majimbo kuu ya Saint Paul na Minneapolis, nchini Marekani, kusitisha uchunguzi wa uasherati wa Askofu Mkuu John Nienstedt, hali iliyoonekana kama "kuficha" vmakosa.
Na mnamo 2016, baada ya msisitizo wa Viganò, Papa Francis alikutana na Kim Davis, afisa wa Kentucky ambaye alikataa kutoa leseni za ndoa kwa wapenzi wa jinsia moja.
Wakati huu ulionekana kama sehemu mbaya kwa Kanisa Katoliki, kwa kuwa Davis alikuwa na madai ya sababu za kidini za uamuzi wake, ambao ulikataliwa mahakamani.
Mwaka huo huo, Papa alimwondoa katika majukumu yake kama balozi nchini Marekani.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi