Utafiti mpya wa ngozi unaweza kusaidia kupunguza dalili za kuzeeka

Muda wa kusoma: Dakika 5

Pallab Ghosh

Mwandishi wa BBC wa masuala ya Sayansi

Ugunduzi wa kisayansi uliofanywa na timu ya kimataifa ya watafiti hatimaye inaweza kuwa na matokeo muhimu: kupunguza kasi ya dalili za kuzeeka.

Timu ya wanasayansi imegundua jinsi seli za ngozi zinavyotokana na seli zinazoweza kuzalisha seli zaidi zinazofanana nazo (au sterm cells) katika mwili wa binadamu, na timu hiyo hata imeweza kuzalisha sehemu ndogo za ngozi katika maabara.

Utafiti huo ulikuwa sehemu ya mpango mpana wa kujifunza jinsi vipengele vyote vya mwili wa binadamu vinajengwa katika kiwango cha seli.

Mbali na kupunguza kasi ya mchakato wa kuzeeka, matokeo ya utafiti yanaweza pia kutumika kuunda ngozi bandia kwa kupandikiza na hivyo kuzuia makovu.

Mradi wa unaojulikana kama The Human Cell Atlas ni moja wapo ya mipango ya kabambe zaidi katika biolojia. Mradi huo ni wa kimataifa, lakini kituo chake kiko katika Taasisi ya Sanger huko Cambridgeshire, Uingereza.

Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa mradi huo, Profesa Muzlifa Haniffa, utafiti unaofanywa ndani ya mfumo wake utawasaidia wanasayansi sio tu kutibu magonjwa mbalimbali, lakini pia kutafuta njia mpya za kudumisha afya zetu kwa muda mrefu na, labda, hata muonekano wa ujana zaidi.

"Ikiwa tunaweza kudhibiti ngozi yetu na kuzuia kuzeeka, tutakuwa na makunyanzi machache," profesa anasema. "Kama tunaweza kuelewa jinsi seli zinavyobadilika kuanzia mapema hadi kuzeeka katika utu uzima, basi tunaweza kujiuliza: tunawezaje kufufua viungo, tunawezaje kufanya moyo kuwa wa umri mdogo, tunawezaje kuifanya ngozi kuwa changa?"

Bila shaka, bado hii ni njia ndefu, lakini watafiti pia hawakomei hapo, kwani wanaendelea na utafiti wao, ikiwa ni pamoja na kuelewa ni jinsi gani seli za ngozi zinavyokua katika kiinitete katika hatua za mwanzo za maendeleo ya binadamu.

Wakati yai linaporutubishwa kwa mara ya kwanza, seli zote za binadamu ni sawa. Lakini ndani ya wiki tatu, jeni fulani ndani ya seli asilia zikisambaza maagizo ya utaalam na mkusanyiko ili kuunda sehemu mbalimbali za mwili wetu.

Watafiti wameweza kujua ni jeni gani, kwa wakati gani na katika maeneo gani yanaundwa ili kuunda kiungo kikubwa cha binadamu - ngozi.

Chini ya darubini, wakati unatibiwa, jeni hizi zinaonekana kama taa ndogo.

Jeni zenye muundo wa machungwa huunda uso wa ngozi. Jeni za rangi ya manjano huamua rangi yake, lakini kuna nyingine nyingi ambazo huunda miundo inayotengeneza nywele, jasho, na kuzilinda dhidi ya ushawishi wa nje.

Unaweza pia kusoma:

Kimsingi, wanasayansi wamepewa seti ya maagizo ya kuunda ngozi ya binadamu na wamechapisha maagizo haya katika jarida la Nature. Ikiwa unajifunza kusoma maagizo haya, uwezekano wa ajabu utafunguliwa mbele yako.

Kwa mfano, wanasayansi tayari wanajua kwamba tishu za kiinitete huponya bila kuacha makovu.

Seti mpya ya maelekezo ina habari juu ya jinsi hili linavyotokea, na maarifa haya yanaweza kusaidia kujaribu kubaini athari kwa ngozi ya watu wazima, kwa mfano wakati wa upasuaji.

Ugunduzi mwingine muhimu ni kwamba seli za kinga zina jukumu muhimu katika utunzaji wa mishipa ya damu katika ngozi, na wanasayansi waliweza kunakili maagizo ya jeni yanayofanana katika maabara.

Walitumia mchanganyiko maalumu kuchochea na kuzima jeni kwa wakati na mahali sahihi, na hivyo kukuza ngozi bandia kutoka kwa seli asilia katika maabara.

Hadi sasa, wamezalisha tu sehemu ndogo na nywele chache.

Profesa Haniffa anasema lengo la mwisho, ni ukamilifu wa teknolojia.

"Kujua jinsi ya kutengeneza ngozi ya binadamu, tunaweza kuitumia kutibu wagonjwa wenye majeraha ya kuungua na kufanya upandikizaji wa tishu," anasema. "Mfano mwingine ni kama tunaweza kutengeneza nywele, tunaweza kukuza nywele katika watu wenye upara."

Ngozi iliyokuzwa na maabara pia inaweza kutumika kujifunza magonjwa ya ngozi ya ya kuzaliwa na kupima matibabu mapya ya hali hizi.

Maelekezo ya kuchochea na kuzima utendaji wa jeni hutumwa katika kiinitete na kuendelea kufanya kazi baada ya kuzaliwa na kuwa watu wazima, kuruhusu viungo na tishu zetu zote kukua.

Mradi wa The Human Cell Atlas umechambua seli milioni 100 kutoka sehemu mbalimbali za mwili katika kipindi cha miaka minane tangu uanzishwe. Matokeo yake, atlases mbaya za ubongo na mapafu ziliundwa, na wanasayansi sasa wanaendelea kufanya kazi kwenye figo, ini, na moyo.

Hatua inayofuata, kwa mujibu wa profesa wa Chuo Kikuu cha Cambridge Sarah Teichman, ambaye ni mmoja wa waanzilishi na viongozi wa mradi huo, ni kuchanganya seli binafsi katika mfumo mzima wam wili.

"Ni jambo la kufurahisha sana kwa sababu inatuwezesha kuangalia mfumo mzima wa muundo wa utendaji wa mwili wa binadamu, na kuelewa binadamu kwa njia mpya," aliiambia BBC. "Itasababisha vitabu vya kiada kuandikwa upya juu yetu, tishu zetu na viungo, na jinsi zinavyofanya kazi."

Katika wiki na miezi ijayo, "maagizo ya maumbile" ya jinsi sehemu zingine za miili yetu zinavyokua zinapangwa kuchapishwa, zikitupa picha kamili zaidi ya jinsi wanadamu "wanavyoumbika."

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi