Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
CHAN 2024: Afrika Mashariki fungu la kukosa, Uganda nje kama Tanzania na Kenya
Uganda imeondolewa rasmi kutoka robo fainali za CHAN 2024 baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Senegal katika mechi iliyochezwa jioni hii kwenye Mandela National Stadium, Kampala. Goli la ushindi la Senegal limefungwa na Oumar Ba katika dakika ya 62 ya kipindi cha pili, likimaliza ndoto ya Cranes kufikia nusu fainali.
Hii inafuata matokeo ya jana ambapo timu nyingine za taifa za Afrika Mashariki pia zilitolewa. Kenya ilitolewa na Madagascar baada ya sare ya 1-1 katika dakika 90, na Madagascar kushinda 4-3 kupitia mikwaju ya penalti. Kenya walijitahidi ili kutinga nusu fainali ya kwanza ya michuano mikubwa ya Afrika, baada ya miaka 38, lakini walishindwa.
Tanzania pia walitolewa kutoka mashindano baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Morocco katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Goli la ushindi la Morocco lilifungwa na Oussama Lamlaoui dakika ya 65 ya kipindi cha pili. Taifa Stars walikuwa wameongoza kundi lao bila kufungwa mechi hata moja, lakini Morocco walionyesha ubabe na kuondoa Tanzania.
Kwa matokeo haya, ingawa kuna jirani Sudan, hakuna timu ya Afrika Mashariki ambao walikuwa wenyeji, Tanzania, Kenya na uganda, iliyosalia katika robo fainali ya CHAN 2024. Sasa nusu fainali ni Senegal dhidi ya Madagascar huku Morocco ikisubiri mshindi kati ya Sudan dhidi ya Algeria.
Uganda ilipambana kiume
Mechi ya robo fainali ya CHAN 2024 kati ya Uganda na Senegal ilichezwa kwa ushindani mkubwa, huku pande zote mbili zikijitahidi kutafuta bao la mapema.
Senegal walionekana kuwa na udhibiti mzuri wa mpira katika dakika za mwanzo, wakitumia krosi za haraka na kushambulia kwenye pembeni, huku Uganda ikijitahidi kutafuta nafasi ya kushambulia kutoka katikati ya uwanja.
Uganda walijaribu kutawala mchezo, lakini Senegal walijibu kwa ulinzi imara na mikakati ya kuharibu mashambulizi ya Uganda. Hatimaye, dakika ya 62 goli la Oumar Ba liliweka Senegal mbele, likilazimisha Uganda kucheza kwa dharura lakini bila mafanikio.
Mechi ilimalizika 1-0 kwa ushindi wa wageni, ikimaliza safari ya Uganda katika mashindano haya kwa mwaka huu.
Kenya ilitawala mchezo wake wa robo fainali
Katika mchezo wa mwenyeji mwingine, Kenya walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Alphonse Omoja dakika ya 38, kabla ya Razafimahatratra wa Madagascar kusawazisha dakika ya 60.
Baada ya kutoka ya sare ya 1-1 katika dakika 120, Madagascar walishinda 4-3 kwa mikwaju ya penalti, huku Toky Rakotondraibe akifunga mkwaju wa penalti baada ya Alphonce Omija kukosa.
Harambee Stars, ilikuwa ikiwania kutinga nusu fainali ya kwanza ya bara baada ya miaka 38.
Tanzania ilishindwa kuendeleza ubabe
Tanzania kama ilivyokuwa kwa Kenya ilitawala kipindi cha kwanza na kukosa nafasi kadhaa za wazi za kufunga magoli.
Katika dakika ya 65 ya kipindi cha pili Morocco ilizima ndoto za Tanzania kwa holi safi lililofungwa na mshambuliaji Oussama Lamlaoui.
Tanzania ambayo iliongoza kundi B kwa kutinga robo fainali kibabe bila kufungwa hata mechi moja ikashindwa kendeleza ubabe mbele ya Morocco baada ya hapo.
Morocco imetwaa ubingwa wa CHAN mara mbili huku Taifa Stars ikitinga hatua hii kwa mara ya kwanza baada ya kushiriki mara tatu.
Awali Kocha wa Taifa Stars Hemed Suleiman alisema kuelekea mchezo huo "Nimeangalia makundi yote naamini kwamba kila timu katika kundi lolote ni mzuri na inaweza kuleta ushindani. Sisi tupo tayari kukabiliana na Morocco."
Katika hatua ya makundi, Morocco ilikuwa tayari imeshinda mechi tatu na kuchapwa moja dhidi ya Kenya.
Imefunga mabao manane sawa na wastani wa kufunga mabao mawili katika kila mechi na kuruhusu mabao matatu.