Arsenal 'yaigaragaza' 3-0 Madrid, matokeo yanayoipa England timu 5 Mabingwa Ulaya

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Arsenal wamepata ushingi mnono, mtamu na wakushangaza wa mabao 3-0 dhidi ya Real Madrid katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Baada ya kipindi cha kwanza pale Emirates timu zote mbili kwenda sare tasa, kipindi cha pili kilikuwa cha arsenal, Declan Rice akifunga kwa mikwaju ya faulo miwili katika dakika ya 58, kisha Rice akaongeza bao la pili dakika 12 baadaye kwa mkwaju mwingine maridadi. Dakika tano tu baada ya hapo, kiungo anayecheza nafasi ya ushambuliaji, Mikel Merino aliongeza masaibu kwa wageni kwa kumalizia vyema pasi kutoka upande wa kushoto kwa kinda Myles Anthony Lewis-Skelly, miguu michache kutoka golini.

Eduardo Camavinga alitolewa kwa kadi nyekundu dakika za mwisho baada ya kupata kadi ya pili ya njano, ingawa kadi yake ya kwanza ilikuwa tayari imemfanya akose mchezo wa marudiano.

Madrid, moja ya vilabu vikubwa na vyenye historia katika michuano hiyo, kuchapwa idadi hiyo ya mabao, ikiwa na wachezai bora kwa sasa duniani, Vinícius Júnior na Kylian Mbappé Lottin ni kumbukumbu isiyofutika kwa arsenal.

Timu hizo mbili zitarudiana tena Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Bernabeu.

Mara ya mwisho Arsenal kushinda, Ilikuwa msimu wa 2005-06, Thierry Henry akifunga bao pekee na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, kufuatia sare tasa ya 0-0 katika uwanja wa Highbury.

Kwa ushindi huu, arsenal imeiwezesha england sasa kupata nafasi moja zaidi ya ya timu zake kushiriki michuano ijayo ya Klabu bingwa. Maana yake sasa zitakwenda timu tano badala ya timu nne.

/

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jude Bellingham na wenzake wa Madrid walikuwa hoi katika mchezo huo

Baada ya mchezo huo, ulihudhuriwa na masupa staa wengi wa zamani, kulikuwa na maoni kadhaa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Cesc Fabregas: Kiungo wa zamani wa Arsenal na Hispania anasema...

"Ningependa kusema imekwisha (Arsenal kafuzu nusu fainali). Lakini baada ya bao la kwanza nilisema walihitaji la pili na baada ya la pili walihitaji la tatu.

Lakini Real Madrid ni Real Madrid".

Matt Upson: Beki wa zamani wa Uingereza ameiambia BBC Radio 5 Live

"Ni mapema sana kuzungumzia nusu fainali.

Real Madrid imekuwa katika hali mbaya au mbaya zaidi kuliko hii hapo awali na kufanikiwa kupata suluhu. Ikiwa kuna timu yoyote nyumbani ambayo itaigeuza matokeo basi itakuwa wao.

Je, watakuwa na uwezo? Itabidi tusubiri na kuona, lakini Arsenal watajiamini zaidi katika mechi ya marudiano"

Declan Rice: mfungaji wa mabao mawili na nyota wa mchezo....

"Sijui kama nitasahu. Nimeangaliasimu yangu basi na imekuwa wazimu. Kufunga goli langu la kwanza la free-kick katika mchezo kama huu ni jambo maalum. Na kisha nilipopata ya pili. Nilikuwa na ujasiri tu. Sina la kusema kweli.

"Kuifunga Real Madrid katika mashindano haya. Ni usiku mkubwa kwetu.

"Kocha alisema hata kama tunaongoza kwa mabao 3-0 ubora wa mtu mmoja mmoja walio nao Madrid unatisha. Huko Bernabeu mambo maalum hutokea kwao. Tunataka kuwa katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa."

Matokeo mengine ya klabu bingwa Ulaya, Bayern Munich imechapwa nyumbani 2-1 na Inter Milan, leo PSG inaikaribisha Aston Villa, Borrusia Dortmund itakuwa kumenyana na Barcelona