Wanasayansi wanajifunza kuzungumza lugha ya nyangumi

    • Author, Katherine Latham
    • Nafasi, BBC

Ilikuwa mwaka 2021, nje ya pwani ya kusini-mashariki mwa Alaska, ambapo timu ya wanasayansi sita ilicheza rekodi ya sauti ya salamu kupitia spika iliyo chini ya maji.

Walipigwa na butwaa walipogundua nyangumi mmoja waliyemwita Twain alipojibu sauti hiyo.

"Ni ajabu," anasema Josie Hubbard, mtaalamu wa tabia za wanyama katika Chuo Kikuu cha California, Davis ambaye nae alikuwa kwenye chombo hicho.

“Lazima uzime chombo umbali wa mita kadhaa walipo nyangumi. Katika tukio hili, Twain mwenye umri wa miaka 38 alikwenda kwenye chombo, na kukizunguka kwa dakika 20,” anasema Hubbard.

Twain alipoondoka, Hubbard alikwenda chini ya chombo na ndipo wakagundua nyangumi huyo alikuwa akijibu sauti ya spika kwa dakika zote 20. Sauti ndefu inayokuja na kupotea, ikiwa na mapigo na milunzi.

Pia unaweza kusoma

Tabia za Nyagumi

Nyangumi huonyesha orodha ndefu ya tabia zinazofanana na za wanadamu. Wanashirikiana wao kwa wao na viumbe wengine. Wanafundishana stadi za maisha, kama kutunza watoto na kucheza.

Tofauti na wanadamu, wanatumia zaidi sauti kuliko macho kwenye mambo yao mengi. Sauti zao zinaweza kusafiri mbali na kwa kasi ndani ya maji kuliko inavyo safiri hewani.

Nyagumi aina ya Cetaceans kwa mfano, wanategemea kelele kuwasiliana wao kwa wao, kusafiri, kutafuta wenza na chakula, kulinda maeneo na rasilimali zao, na kuepuka wanyama wanaokula wenzao.

Watoto wao hulia kama watoto wachanga wa kibinaadamu, wengine wanaaminika kuwa na majina, na makundi yao kutoka sehemu tofauti za bahari huwa na lahaja za kieneo.

Nyangumi wamesikika wakiiga lahaja za vikundi vya kigeni - na wengine wanafikiriwa kuwa huiga hata sauti ya kibinaadamu.

Rikodi ya kwanza ya nyimbo za nyangumi ilirikodiwa mwaka 1952 na mhandisi wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Frank Watlington.

Takriban miaka 20 baadaye, mwanabiolojia wa baharini Roger Payne aligundua sauti hizi zilipangwa kwa kujirudiarudia. Hilo lilibadilisha uelewa wa sauti za nyangumi na kuzua shauku iliyopelekea miongo kadhaa ya utafiti.

Kipi kifuatacho

Watafiti wanatumai kuchambua sauti za nyangumi kunaweza kutusaidia kuelewa sauti zao. Watafiti wanakisia kuwa sauti za nyangumi zina ujumbe wenye maana.

Hata hivyo, wanasema, uelewa wetu wa mawasiliano ya nyangumi bado uko katika hatua ya awali sana.

Katika kipindi chote cha kubadilishana sauti, Twain mara kwa mara alitoa sauti kulingana na muda sauti ya spika inavyotoka. Ikiwa kila baada ya sekunde 10 nae alitoa sauti kila baada ya sekundu hizo. Walifanya hivyo mara 36 kwa dakika 20.

"Changamoto kubwa kwetu ni kuelewa sauti hizo na kuamua maana yao, ili tuweze kujua maana. Nadhani AI itatusaidia kufanya hivyo," anassema Brenda McCowan, mtafiti katika timu hiyo.

Wataalamu wengine

Umbali wa zaidi ya maili 5,000 (km 8,000), kundi la wataalamu wa akili bandia, lugha asilia, waandishi, wataalamu wa lugha, wanabiolojia wa baharini, wataalamu wa roboti - wanatarajia kutumia AI - kufafanua sauti za nyangumi.

Timu hii nyingine ilizinduliwa mwaka 2020, Ceti (Cetacean Translation Initiative), ikiongozwa na mwanabiolojia wa baharini David Gruber, imekuwa ikirekodi kundi la nyangumi katika pwani ya Dominica, kisiwa cha Karibea, kwa kutumia maikrofoni kwenye maboya, samaki wa roboti na vifaa vilivyowekwa kwenye migongo ya nyangumi.

"Ni vigumu kwetu kuelewa ulimwengu wao, zaidi ya maingiliano haya mafupi sana ya sauti. Huyu ni kiumbe wa kipekee, mpole, na kuna mengi tu yanayoendelea katika maisha yake," anasema Gruber.

"Kila wakati tunapotafiti, tunapata utata na namna mpya zaidi katika mawasiliano yao."

Anaamini tutafikia hatua ya maendeleo ya kiteknolojia ambayo tutaweza pengine kuelewa mawasiliano ya nyangumi.

Taarifa zilizokusanywa zinafanyiwa uchambuzi kwa kutumia mashine ili kugundua maana ya sauti hizo, na matokeo yatachapishwa mwaka 2024.

Samantha Blakeman, meneja wa data za baharini wa Kituo cha Kitaifa cha Oceanography, "AI inaweza kuturuhusu kuelewa mifumo ya mawasiliano ya viumbe vingine vingi. Nadhani litakuwa jambo zuri kwa ulimwengu - ikiwa tunajali kuhusu kile ambacho nyangumi wanasema."