Martha Koome - Kutoka kuwa mwanaharakati wa haki za wanawake hadi jaji mkuu wa Mahakama ya Juu

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Aliteuliwa kuwa jaji mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kenya Mei 2021, Martha Koome ametoa uamuzi muhimu zaidi katika maisha yake mafupi kama jaji mkuu wa taifa kwa kuunga mkono ushindi wa Naibu Rais William Ruto dhidi ya Raila Odinga katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9.

Alitoa uamuzi wake kwa utulivu na baadhi wanaweza kusema kwa njia ya nyepesi, lakini maneno yake yalikuwa na nguvu - hakukuwa na "njama" dhidi ya Bw Odinga, na timu yake ya wanasheria ilishindwa kuwasilisha hoja za kuthibitisha kuwa matokeo yalichakachuliwa ili kumpendelea Bw Ruto.

Koome mwenye umri wa miaka 62 aliteuliwa kuwa jaji mkuu Mei mwaka jana na Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta baada ya kuwa juu ya wagombea 10 waliohojiwa mbele ya hadhira ya moja kwa moja ya televisheni na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC).

"Mwanamke huyu ana pumzi yenye hewa safi. Anajibu maswali jinsi yalivyoulizwa na kwa kweli anagonga muhuri wake wa kitaaluma juu yao," mtu mmoja alitoa maoni wakati huo kuhusu utendajikazi wake.

Wakati wa mahojiano yake alirejelea uzoefu wake mgumu aliopitia huko Meru katika maeneo ya mashambani mashariki mwa Kenya katika familia yenye wake wengi - alizaliwa mwaka wa 1960, miaka mitatu kabla ya mwisho wa utawala wa kikoloni.

"Mimi ni mwanakijiji kwa maana halisi. Wazazi wangu walikuwa wakulima wadogo na tulikuwa watoto 18 kutoka kwa mama wawili Kwa hiyo, kwetu sote, hasa wasichana - ilikuwa ni kazi kukabiliana na usawa."

Na alishinda vikwazo zaidi kufikia hatua ya jaji mkuu kwa vile hakupendelewa, huku wachambuzi na wataalamu wakimpa nafasi Fred Ngatia kuwa mshindi kwani alimwakilisha Kenyatta kwenye mzozo wa uchaguzi wa 2017.

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Fred Ngatia, ambaye amemwakilisha rais, alikuwa mpinzani mkuu wa Martha Koome

Mahakama ya Juu zaidi ilibatilisha ushindi wa rais Kenyatta katika uchaguzi huo, ikitaja kasoro kadhaa. Kura mpya uliamriwa, ambapo Kenyatta aliibuka tena mshindi baada ya Bw Odinga kususia marudio hayo.

Bw Ngatia huenda hakushinda kesi ya uchaguzi wa rais, lakini ufasaha wake na ufafanuzi wake wa sheria katika mahakama wakati huo ulimletea alama za juu zaidi machoni pa Wakenya kote katika mgawanyiko huo.

Hata hivyo Jaji Koome alikuwa mtulivu, mwenye kujiamini na alipimwa wakati wa kuhojiwa kwa muda wa saa nne na rekodi yake kuhusu watoto na haki za kijinsia pamoja na jukumu lake katika kuandaa katiba ya Kenya ya 2010, hasa Mswada wa Haki, zilijieleza.

Alizungumza kwa majigambo kuhusu jinsi katiba inavyoharamisha ubaguzi wa kijinsia tofauti na ile ya zamani ambayo "ilikuwa ikiwabagua wanawake moja kwa moja".

"Hawakuweza kutoa uraia, iliruhusu mila na desturi ... kama vile ndoa za utotoni, na ukeketaji. Tumetoka mbali," aliambia jopo la mahojiano.

ggg

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Martha Koome alisaidia kuandaa katiba mpya ya Kenya, ambayo ilipitishwa baada ya kura ya maoni mwaka 2010.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka 2020, Jaji Mkuu Koome alikuwa mshindi wa pili wa Tuzo Umoja wa Mataifa ya 'Person of the Year Award' nchini Kenya "kwa utetezi wake wa haki za watoto katika mfumo wa haki".

Pia amewahi kuwa kamishna katika Kamati ya Umoja wa Afrika ya Haki na Ustawi wa Watoto.

Ameolewa na ana watoto watatu, ana taaluma ya kuvutia iliyochukua miongo mitatu baada ya kuhitimu sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo 1986 - na amepata digrii zingine tofauti tofauti katika kipindi cha miaka kadhaa.

Alianza kama mtaalamu wa sheria mnamo 1988, kabla ya kuanzisha kampuni yake ya uwakili kama mshirika mkuu mnamo 1993. Wakati wa kufanya kazi zake, alipata umaarufu kwa kutetea haki za binadamu, akiwakilisha wafungwa wa kisiasa wakati wa utawala wa Rais Daniel arap Moi.

Alikuwa miongoni mwa wanasheria waliohusika katika kelele za miaka ya 1980 ya kufuta Kifungu cha 2A cha katiba ambacho kiliifanya nchi kuwa nchi ya chama kimoja.

Mara nyingi wenzake hawakutaka kuwawakilisha wateja wa kike, hivyo yeye alichukua kesi zao na kuja kuona jinsi ilivyokuwa vigumu kupata haki kwa wanawake mahakamani linapokuja suala la haki ya kumiliki mali ndani ya ndoa na mirathi kwani sheria ilikuwa 'imetawaliwa na mfumo dume".

Hii ilimchochea kutafuta mageuzi ili kuhakikisha sheria "inalinda familia kwa sababu familia ndio msingi wa jamii," Jaji Koome alisema katika mahojiano yake.

Alikua kile alichokiita "motomoto" katika harakati zake na alikuwa mwanachama mwanzilishi wa Shirikisho la Wanasheria Wanawake (Fida), ambalo tangu wakati huo limekuwa likitoa uwakilishi wa bure kwa waathirika wa kijinsia na unyanyasaji wa kijinsia nchini Kenya.

Mnamo 2003, Rais Mwai Kibaki alimteua kuwa jaji wa Mahakama Kuu.

Kwa miaka nane iliyofuata aliongoza mahakama ya ardhi na mazingira pamoja na kitengo cha familia jijini Nairobi.

Pia alihudumu katika mahakama za satelaiti ambapo alijinasibu kwa kuondoa mlundikano mkubwa wa kesi kwa kasi ambayo alisema haikuwahi kufanyika katika bara.

Alipandishwa cheo katika Mahakama ya Rufaa mwaka wa 2012, miaka minne baadaye alituma maombi ya kuwa jaji wa Mahakama ya Juu bila mafanikio.

'Chakula cha mchana kinaweza kusuluhisha'

Changamoto yake kubwa wakati wa mahojiano yake na JSC ilikuwa kutetea sehemu yake katika kesi ya dharura ya Mahakama ya Rufaa katika mkesha wa marudio ya uchaguzi wa 2017.

Jaji wa Mahakama Kuu alikuwa ametoa uamuzi kuhusu kesi siku hiyo kwamba maafisa wote wa uchaguzi na manaibu wao walikuwa wameteuliwa kinyume cha sheria.

ggg

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Baada ya kuapishwa kwake Novemba 2017 Rais Kenyatta (katikati) alipeana mkono na David Maraga (kushoto), ambaye sasa amestaafu kama jaji mkuu.

Yeye na majaji wengine wawili waliokata rufaa walibatilisha hili, na kuruhusu kura kuendelea, amri ya muda ya kuepusha mgogoro wa kikatiba, alisema.

Suala la jopo la mahojiano lilikuwa ukweli kwamba uamuzi huo ulitolewa baada ya saa rasmi za kazi na bila pande zote kuwepo - sio uamuzi wenyewe.

Jaji Koome ambaye hakuwa na wasiwasi alieleza kuwa katika mazingira ya kipekee na umuhimu kwa taifa mahakama ya rufaa inaweza kufanya hivyo na alirudia mara kadhaa kwamba Mahakama ya Juu iligundua kuwa hakukuwa na tatizo na maafisa wa uchaguzi na kesi hiyo ilikuwa imebatilishwa tangu mwanzo.

Martha Koome ni mkuu wa 15 wa mahakama ya juu zaidi nchini Kenya tangu uhuru.

Aliwahi kujieleza kama mchezaji mzuri katia timu na akasema hatasita kumpigia simu rais kama jaji mkuu ili kuzungumza nae kama ikihitajika.

Hii anaamini ndiyo njia bora ya kumaliza makabiliano - ikisaidiwa na chakula.

Alipoulizwa jinsi ambavyo angeshughulika na majaji wenzake wa Mahakama ya Juu kama kungekuwa na msuguano, chakula cha mchana kilikuwa suluhisho lake.

"Chakula huwasaidia watu kuzungumza vizuri... kwa hivyo tutakuwa na mapumziko kadhaa, kula [hapo] ili kuelewa tatizo ni nini."

Haijulikani kama alilazimika kuwachukua majaji wengine saba kwa chakula, lakini hukumu yao ilikuwa kauli moja.

Hilo limeongeza uaminifu wa mahakama na jaji mkuu machoni pa Wakenya wengi.