Hivi ndivyo Kishikwambi (iPad) kilichotupwa mtoni miaka mitano iliyopita kilivyofichua njama kubwa za mauaji

    • Author, Thomas Mackintosh
    • Nafasi, BBC News, London
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kulikuwa na matukio matatu makubwa ya uhalifu, wizi wa mali za thamani kwenye jumba la makumbusho la Uswizi. Kumpiga risasi mchekeshaji maarufu huko Woodford, London mashariki na wizi katika jumba la kifahari huko Sevenoaks, Kent.

Matukio haya awali yalionekana kama hayana uhusiano, lakini kumbe yalikuwa yanahusisha mtandao mmoja wa uhalifu wa kimataifa, ambapo polisi waliubaini baada ya uchunguzi wa miaka sita.

Ushahidi muhimu ulikuwa ni Kishkwambi ama iPad, iliyopatikana kwenye mto, ikichimbiwa chini kwa zaidi ya inchi kadhaa kando ya Mto Thames chini ya mkondo kutoka eneo la O2 Arena.

Kubainika kwa Kishkwambi hiki, ilikuwa muhimu kwa uchunguzi ambao umesababisha watu watatu kupatikana na hatia huko Old Bailey ya kujaribu kumuua mmoja wa majambazi mashuhuri wa Uingereza waliokuwa na silaha.

Ilikuwa imekaa chini ya maji kwa zaidi ya miaka mitano hadi ilipopatikana na afisa wa polisi akitumia kifaa cha kugundua vyuma, ilikuwa asubuhi moja ya Mwezi Novemba 2024.

Wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi waliweza kuisafisha na kufungua sehemu ya ya kuwekea kadi ya Sim, ambapo bado kulikuwa na kadi ya Simu ya rangi ya pinki ya Vodafone.

Kumbukumbu za simu zilipigwa na kuingia ambazo zilizopatikana kutoka kwenye kadi hiyo ya sim zilitoa ushahidi mzito dhidi ya wanaume watu watatu Louis Ahearne, Stewart Ahearne, na Daniel Kelly, wote ambao pia walihusika katika wizi wa jumba la makumbusho nchini Uswisi mwezi mmoja kabla ya shambulio la risasi dhidi ya mchekeshaji.

Mkuu wa Upelelezi, Det Supt Matthew Webb alijiuliza kuhusu kesi hii:

"Nimejiuliza sana kuhusu hili. Je, walijikwaa kwa makosa yao wenyewe, au walikuwa na kiburi cha kufikiri kwamba hawatawahi kukamatwa?"

Njama ya Mauaji Iliyopangwa kwa Umakini

Ndugu wa Ahearne na Kelly walikuja kuwa lengo la uchunguzi wa polisi baada ya milio ya risasi kusikika katika usiku wa kiangazi kwenye eneo la kifahari la Woodford mnamo 11 Julai 2019.

Risasi sita zilipenya kupitia glasi ya jumba la kifahari la mchekeshaji *Russell Kane, ambalo lilikuwa limekodishwa kwa **Paul Allen*.

Moja ya risasi ilikata kidole cha Allen, nyingine ilimpiga kwenye koo na kutua kwenye uti wa mgongo wake, hali iliyomsababishia kupoteza damu nyingi na kushindwa kupumua.

"Ameshambuliwa kwa risasi! Ameshambuliwa!" Jade Bovington, mpenzi wa Allen, alipiga kelele kwa hofu.

Wakati Jade alipokuwa akiita ambulansi kwa hofu, majirani na mlinzi wa kibinafsi walikimbia kutoa msaada wa kwanza.

Shahidi mmoja alieleza kumuona mwanaume asiyejulikana akiruka juu ya ukuta mfupi, akipita katikati ya vichaka, na kuingia kwenye gari lililokuwa linamsubiri – ambalo liliondoka kwa kasi.

Hadi leo, Allen anategemea kiti cha magurudumu, akiwa amepooza kuanzia sehemu ya juu ya kifua chake kushuka chini.

Allen alikuwa mmoja wa wahalifu waliopata umaarufu zaidi Uingereza baada ya kuhusika katika wizi mkubwa wa kutumia silaha mnamo 2006. Genge lake lilivamia hifadhi ya pesa ya Securitas huko Tonbridge, Kent, na kuiba pauni milioni 53 kwa kutumia bunduki, ikiwemo AK-47.

Allen alikimbilia Morocco lakini alikamatwa Rabat akiwa na mshirika wake Lee Murray, ambaye bado anahudumia kifungo nchini humo. Januari 2008, Allen alirudishwa Uingereza na kuhukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani.

Baada ya kuachiliwa mwaka 2016, Allen alihamia Woodford na familia yake baada ya jaribio la awali la mauaji nyumbani kwake Woolwich mnamo Septemba 2018.

Miezi kumi baadaye, risasi zilimpata akiwa jikoni nyumbani kwake mpya Woodford.

Uchunguzi kwenye eneo la tukio

Waendesha mashtaka walidai kuwa Ahearnes na Kelly walihusika katika mpango wa kumuua Allen, mpango ambao ulihusisha gari la kukodi, ufuatiliaji wa karibu, na simu zisizosajiliwa za malipo ya awali.

"Hii ilikuwa jaribio la mauaji lililopangwa kwa umakini mkubwa na kundi la watu waliobobea katika uhalifu wa kiwango cha juu," alisema mwendesha mashtaka Michael Shaw KC.

Wakati wa kuchunguza jinsi watatu hao walivyojua mahali Allen alikokuwa akiishi, polisi waligundua kuwa uhalifu wao ulienea hadi bara la Ulaya.

Katika kesi ya wiki saba kwenye Mahakama ya Old Bailey, waendesha mashtaka walieleza kuwa wizi wa kimataifa ulithibitisha kuwa Ahearnes na Kelly walikuwa "wahusika wa kiwango cha juu" cha uhalifu.

Lakini, bila polisi kujua, walipokuwa wakifuatilia mali za kale zilizoibwa, watatu hao walifanya makosa sawa yaliyowaruhusu polisi kufuatilia uwepo wao katika shambulio la risasi la Woodford.

Watatu hao walianza kujaribu kutupa vitu walivyobanwa na vilivyokuwa vikifuatiliwa na vingine wakisafiri mpaka Hong Kong kujaribu kuuza baadhi ya vitu walivyoiba.

Saa chache baada ya shambulio la risasi, eneo la uhalifu huko Woodford lilianza kuchunguzwa kisheria. Maganda sita ya risasi yaliyofyatuliwa kutoka kwenye bunduki aina ya Glock yalipatikana.

Sampuli za DNA zilizokusanywa kutoka kwa uzio zilionyesha kuhusika kwa Louis na Kelly.

Kupitia picha za CCTV, polisi waliweza kutambua nambari ya gari ya Renault Captur ya rangi ya kijivu inayomilikiwa na kampuni ya kukodi ya Avis.

Rekodi zilionyesha ilikuwa imekodishwa na Stewart kutoka tawi la Dartford siku mbili kabla ya shambulio hilo la risasi, na kurudishwa siku iliyofuata.

Uchunguzi zaidi wa CCTV ulibaini kuwa dakika 90 kabla ya ufyatuaji risasi gari hilo la Renault ilikuwa imeingia kwenye karakana ya Shell kwenye Barabara ya Shooters Hill, karibu na Greenwich Park.

"Walisimama kwenye kituo cha mafuta kwa sababu Louis Ahearne alikuwa na kiu," Shaw aliambia mahakama.

"Uzuri wa vituo vya mafuta ni kwamba vina CCTV nzuri sana," Shaw aliongeza.

Uchunguzi wa kwenye mto Thames

Mnamo Oktoba 2024, miezi minne kabla ya kesi ya Old Bailey kuanza, Louis alitoa maelezo yake ya utetezi ambayo yalikuwa na taarifa moja ya kushangaza.

Alisema kuwa, wakati wakirudi Woolwich, gari iliyotumika kwa uhalifu huo, Renault ilikuwa imesimama katika barabara ya John Harrison. Louis alisema alijiweka mahali ambapo angeonekana na Camera za CCTV za mtaani kwamba "akipunga hewa" huku mwenzake Kelly akitoweka kuelekea kwenye Mto Thames kwa ajili ya kutuma ushahidi, ikiwemo Kishkwambi au ipad.

Det Supt Webb anakumbuka: "Tulijua gari lilikuwa limesimama katika barabara ya John Harrison Way na kwamba Kelly alitoka kwenye gari. Sikujua alikoenda, sikujua kilichotokea.

"Mara moja, tulikuwa tukifikiria ikiwa mtu anataka kutupa kitu muhimu labda itakuwa bunduki."

Kauli ya utetezi ya Louis ilichangia kubainika kwa iPad hiyo iliyotupwa kwenye mto Thames, ambayo ilimkasirisha sana Kelly, ambaye aligundua imetolewa kauli hiyo kabla ya kesi kuanza.

Kelly na Stewart walikaa kizimbani kwa ukimya wakati wote wa kesi hiyo, na walikataa kutoa ushahidi, kwa kuwa wote walionyesha hofu juu ya usalama wao hapo awali. Louis alidokeza mahakamani kwamba ni Kelly ndiye aliyefyatua risasi risasi kule Woodford.

Lakini Det Supt Webb walisema iPad ndio kiini cha kubainika kwa yote haya.

"Det Insp Matthew Freeman alinipigia simu na kusema tumeenda kwenye Mto wa Thames na tumepata iPad.

"Siwezi kurudia maneno niliyotumia lakini Ilikuwa muhimu sana kutegua fumbo."

Polisi waligundua kuwa mpango wa mauaji ulitekelezwa kwa umakini mkubwa, ukihusisha gari la kukodi, ufuatiliaji wa karibu, na simu zisizosajiliwa za malipo ya awali.

Takwimu za CCTV zilionyesha gari la Renault Captur lililokodishwa na Stewart Ahearne siku mbili kabla ya shambulio.

Takwimu za simu zilionyesha iPad na iPhone 6 ya Kelly zilikuwa zimewasiliana na namba chache, ikiwemo za ndugu wa Ahearne.

Simu hizo zilifuatiliwa hadi kwa Kelly, ambaye alikuwa amenunua simu 59 zisizosajiliwa kupitia Amazon na eBay.

Simu hizo za muda mfupi zilifutwa kutoka mtandao muda mfupi kabla ya Allen kupigwa risasi.

Louis Ahearne, Stewart Ahearne, na Daniel Kelly , walipatikana na hatia ya kula njama ya mauaji na wanatarajiwa kuhukumiwa tarehe 25 Aprili, 2025.

Lakini kwa Mkuu wa Upelelezi, Det Supt Webb, anasema uchunguzi haujakamilika.

"Hii ni mojawapo ya kesi ambapo unavyoendelea kuchunguza, ndivyo unavyoendelea kugundua mengi," anasema.