Mhalifu nguli aliyeiba choo cha dhahabu cha mabilioni, akahukumiwa kulipa pesa ya 'mkate' mmoja

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika tukio lililoonekana kama sinema ya wizi wa kihistoria, genge la wahalifu limekutwa na hatia kwa kuiba choo cha dhahabu chenye thamani ya pauni milioni 4.8 kutoka kwenye maonyesho ya sanaa katika jumba la kifahari la Blenheim Palace, Oxfordshire. Kwa pesa ya Tanzania hiyo ni karibu zaidi ya 15.3bilioni au 960.4mil za Kenya ambazo unaweza kujenga madarasa zaidi ya 600 ya Sekondari.

Choo hicho cha dhahabu, kilichopewa jina la America na msanii maarufu Maurizio Cattelan, kilikuwa sehemu ya maonyesho ya sanaa yaliyokuwa yakifanyika kwenye kasri hilo la kifalme. Siku chache baada ya hafla ya uzinduzi wa maonyesho hayo mnamo Septemba 2019, genge la wahalifu lilivunja lango la kasri kwa kutumia magari mawili yaliyoibwa, kuvunja dirisha, na kung'oa choo hicho kabla ya kutoweka nalo ndani ya dakika tatu pekee.

Kiongozi wa genge hilo anaitwa James Sheen, mwenye umri wa miaka 40 kutoka Oxford, ambaye alikamatwa baada ya polisi kupata vipande vya dhahabu kwenye mavazi yake na sampuli za DNA yake kwenye eneo la tukio. Sheen, ambaye ana historia ndefu ya uhalifu, alikuwa tayari ameshahukumiwa kwa makosa ya ulaghai, wizi na hata kumiliki silaha.

Sheen ni mtu anayetajwa kama mhalifu sugu, akikamatwa mara kadhaa, lakini tukio la hivi karibuni la wizi wa choo cha dhahabu ambalo sasa amekiutwa na hatia, limemuweka zaidi kwenye uso wa dunia. Makala haya inakupitisha kwanza kwenye uchunguzi baada ya choo hicho cha kipekee kuibiwa mpaka hukumu iliyotoka Machi 18, 2025.

Uchunguzi na kukamatwa Sheen na wenzake

Mbinu za polisi, zikiwemo uchunguzi wa DNA, CCTV na uchambuzi wa simu, zilisaidia kuthibitisha kuwa Sheen na washirika wake walihusika katika wizi huo.

Michael Jones, mwenye umri wa miaka 39, alikutwa na hatia ya kupanga uhalifu huo, huku Fred Doe, 36, akikutwa na hatia ya kula njama kuuza dhahabu hiyo. Hata hivyo, Bora Guccuk, mfanyabiashara wa vito kutoka London, aliachiliwa huru baada ya mahakama kutopata ushahidi wa kutosha kuthibitisha ushiriki wake.

Baada ya wizi huo, ndani ya siku chache, choo hicho kilivunjwavunjwa na kuuzwa kwa mafundi dhahabu. Hakuna hata gramu moja ya dhahabu iliyopatikana tena.

Ujumbe wa WhatsApp uliopatikana kwenye simu ya Sheen ulionyesha picha ya mfuko uliojaa pesa taslimu na ujumbe uliosema "520,000 ha ha ha", ishara kwamba dhahabu hiyo ilikuwa tayari imeshauzwa.

Mhalifu sugu aliyedharau sheria

Hii si mara ya kwanza kwa Sheen kuhusika katika uhalifu mkubwa. Katika miaka 20 iliyopita, amekwishahukumiwa mara sita, huku magenge aliyoyaongoza yakipata faida ya zaidi ya pauni milioni 5 kutokana na uhalifu wa aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ulaghai, wizi wa mashine za ATM kwa kuzilipua, na uporaji wa mashindano ya farasi huko Newmarket, ambapo aliiba vikombe vya dhahabu na fedha vyenye thamani ya pauni 400,000.

Licha ya kuwa mmoja wa wahalifu wanaojulikana zaidi Uingereza, mamlaka imeshindwa kurejesha pesa nyingi alizopata kwa njia haramu. Mahakama iliamuru Sheen alipe faini ya pauni 1 pekee kama sehemu ya adhabu yake, huku uchunguzi wa kifedha ukiendelea dhidi yake.

Pauni 1 ni fedha ndogo mno thamani yake ni kama mkate mmoja katika nchi nyingi za Afrika, ukilinganisha na mabilioni ya fedha aliyoiba kupitia matukio mbalimbali ya wizi katika miaka 20 iliyopita.

Matokeo ya kesi na mjadala wa sheria

Baada ya hukumu kutolewa, viongozi wa sheria na wanasiasa wameelezea wasiwasi wao kuhusu namna mfumo wa sheria unavyoshindwa kuwashughulikia ipasavyo wahalifu wa aina ya Sheen.

Waziri wa zamani wa Mambo ya ndani, David Blunkett, alikiri kuwa sheria ya Proceeds of Crime Act, iliyoundwa kurudisha mali za wahalifu, imeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali na mafunzo kwa maafisa wa utekelezaji wa sheria.

Kwa sasa, mamlaka inaendelea kufuatilia mali za Sheen huku akiendelea na kifungo cha miaka 17 kwa makosa mengine aliyoyafanya huko nyuma kabla ya wizi wa choo cha dhahabu.

Licha ya mafanikio ya kuwafikisha baadhi ya wahusika mahakamani, kutorejeshwa kwa dhahabu hata gramu moja kunaacha maswali mengi kuhusu mtandao mpana wa uhalifu wa kifedha unaoendelea bila kukamatwa.

Wezi wa choo cha dhahabu hatimaye wamefungwa, lakini je, haki imetendeka kikamilifu?