Kwa nini mashabiki wa Sudan Kusini waliimba wimbo wa taifa wa Sudan?

g
Maelezo ya picha, Sudan, ambayo inaongozwa na nahodha wa Bakhit Khamis (kushoto, aliyevaa fulana nyekundu ), iliwashinda majirani Sudan Kusini katika mchezo wa kwanza kwenye uwanja mpya wa taifa mjini Juba lakini bado ilipata uungwaji mkono wa mashabiki wa nyumbani

Katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimekuwa vikipamba moto kwa zaidi ya mwaka mmoja, wanasoka wa Sudan wanaendelea kutoa miale ya mwanga – nguvu ya mchezo ya kuunganisha watu ilidhihirika kikamilifu mjini Juba siku ya Jumanne.

Kulikuwa na matukio ya hisia wakati upande wa taifa wa Sudan uliposafiri hadi mji mkuu wa Sudan Kusini, nchi ambayo ilikuwa katika vita na jirani yake wa kaskazini kabla ya kupata uhuru.

Uhuru wa Sudan Kusini ulipatikana mwaka 2011 kama matokeo ya makubaliano ya mwaka 2005 yaliyomaliza mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe uliodumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Wakiweka kando mashindano ya zamani, sehemu kubwa ya umati wa watu walijiunga na wimbo wa taifa wa Sudan kabla ya mechi ambayo ilishuhudia wageni wakiendelea na mwanzo wao wa kutoshindwa katika kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA 2026.

"Mpira wa miguu ni matumaini makubwa kwa Sudan," mshambuliaji Mo Adam aliiambia BBC Sport Africa.

"Ninahisi kama ni lugha peke yake kama njia tofauti ya kueneza hisia chanya kwa nchi.

"Katika mchezo tuliona mashabiki wengi, iwe kutoka kaskazini au kusini, wote wanakuja kutuunga mkono. Hali ya hewa ilikuwa ya kushangaza.

"Mashabiki wa Sudan na Sudan Kusini walitukaribisha kwa mikono miwili."

Hata baada ya kupata uhuru, mgogoro nchini Sudan Kusini haukuisha. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka mwaka 2013 na hatimaye kumalizika kwa makubaliano ya kugawana madaraka miaka mitano baadaye.

Sasa ni Sudan ambayo imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miezi 14 iliyopita - ambapo raia wasiopungua 16,650 wameuawa kwa mujibu wa mradi wa data za eneo la vita na matukio wakati Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takriban watu milioni tisa wamelazimika kuyahama makazi yao.

Unaweza pia kusoma:

Mwandishi wa habari wa Sudan Abdul Musa, ambaye anafanya kazi kwa karibu na shirikisho la soka nchini mwake, alisema msaada huo wakati wa wimbo wa taifa ni "wakati wa ajabu".

"Licha ya vita na matukio yote ya kisiasa, mpira wa miguu ni lugha ya ulimwengu wote," alikiambia kipindi cha Newsday cha idhaa ya BBC ya Dunia.

"Ni mchezo wa kuungana na hivyo ndivyo tulivyohisi wakati wa wimbo. Baadhi ya wachezaji wa Sudan walibubujikwa na machozi.

"Inaonyesha tu jinsi watu walivyohisi kihisia wakati huo na jinsi watu bado wanahisi kana kwamba sisi ni kitu kimoja, na hakuna kitu kinachoweza kututenganisha."

Imani katikati ya usumbufu

g
Maelezo ya picha, Mashabiki wa Sudan walijitokeza katika uwanja wa taifa wa Juba wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimeshuhudia ligi ya ndani ya Sudan ikisimamishwa na Al Hilal na Al Merreikh, klabu mbili kubwa, zinataka kujiunga na ligi ya nchi nyingine msimu ujao.

Wakati huo huo, wachezaji wamelazimika kutafuta uhamisho wa mkopo mahali pengine barani.

Licha ya ushindi huo Sudan imevuruga matumaini hadi sasa katika kufuzu kwa Kombe la Dunia, ikishinda mara tatu na kutoka sare katika mechi zao za ufunguzi.

Kufuatia ushindi wao wa 2-0 nchini Mauritania Alhamisi iliyopita, mabao kutoka kwa Walieldin Khidir, Yasir Mozamil na Mohamed Abdelrahman yaliipa Sudan ushindi wa 3-0 dhidi ya Sudan Kusini.

Matokeo hayo yameifanya Sudan kuwa kileleni katika kundi B, mbele ya washindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2021 Senegal, na kumuacha Adam akiwa na ndoto ya kupata nafasi katika fainali za 2026 nchini Marekani, Canada na Mexico.

"Tuna pointi mbili mezani na nina matumaini kwamba tutaendelea kupata matokeo tunayoyatamani na kuyafikisha katika Kombe la Dunia," alisema Adam.

Sudan wanafundishwa na Kwesi Appiah ambaye alikuwa msaidizi wakati wa Ghana kuelekea robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010 na kisha kuchukua usukani wa Black Stars katika fainali za mwaka 2014.

"Ni nani mwingine ambaye ungechagua kukusaidia kufuzu kwa Kombe la Dunia?" Adam, mwenye umri wa miaka 23, aliongeza.

"Mwaka 2010 alikuwa huko wakati Asamoah Gyan alipohinda. Mara kwa mara tunazungumza juu ya uzoefu na anaamini tunaweza kupata Kombe la Dunia, na mimi pia [naamini hivyo]."

Washindi wa kundi hilo pekee ndio wanaohakikishiwa kufuzu, lakini taifa jingine la Afrika pia linaweza kupata mafanikio kupitia mchuano wa marudiano, na hivyo kuiwezesha Sudan kupata nafasi ya pili kama itamaliza nyuma ya Senegal au Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC).

Musa anasema kuna imani kubwa kwamba Sudan ambayo inashika nafasi ya 127 duniani na haijawahi kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia hapo kabla, inaweza kufuzu kwa kiwango cha juu.

"Hali zote ni dhidi yetu kwa kweli na hali ya kurudi nyumbani ni changamoto," Musa alisema.

"Wachezaji wanaamini wanaweza kufanya hivyo. Waanamini sasa kwamba wanaweza kufikia hatua ya kucheza fainali. Ni imani ya ajabu waliyonayo.

"Hakuna mtu aliyetarajia lakini ndoto zinatimia. Ni matumaini yetu kuwa tunaweza kufikia malengo yasiyofikirika."

Siku ya kihistoria mjini Juba

f
Maelezo ya picha, Sudan Kusini ilijiunga na Fifa mwaka 2012 na kushika nafasi ya 167 duniani na nafasi ya 47 barani Afrika.

Mechi ya mjini Juba siku ya Jumanne ilikuwa ni tukio la ziada wakati Sudan Kusini ilipofungua uwanja mpya.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit aliungana na Gianni Infantino, rais wa shirikisho la kandanda duniani Fifa, katika uwanja huo kwa ajili ya sherehe za kuapishwa.

"Kwa uwanja huu, tunatoa ujumbe wa matumaini kwa watu wote wa Sudan Kusini," Infantino alisema katika hotuba yake katika ukumbi huo wenye uwezo wa kuchukua watu 7,000.

"Kwa mpira wa miguu, tunaunganisha dunia, tunaunganisha Sudan Kusini, tunaunganisha Afrika, tunaunganisha watu wote wanaopenda mchezo wetu, watu wote wanaopenda amani, watu wote wanaopenda umoja.

"Na tunafanya hivi hapa, katika mji mkuu wenu, Juba."

Fifa ilikuwa imewekeza karibu dola milioni 7 (£5.49m) kusaidia ukarabati wa uwanja huo, ambao ulianza mwaka 2019.

Sudan Kusini sasa inaweza kuwa na uwanja wao wenyewe, lakini bado hawana ushindi katika kundi B, baada ya kupata pointi mbili pekee katika michezo yao minne hadi sasa.

Huku kufuzu kwa kombe la dunia kunaonekana kuwa jambo lisilowezekana, je mashabiki wanaweza kuwaunga mkono majirani zao wa kaskazini?

"Kwa upande wa kaskazini na kusini, sioni tofauti yoyote," Adam alisema.

"Sisi sote ni ndugu na kabla ya mgawanyiko tulikuwa taifa moja. Natumai tutaendelea kustawi na kudumisha umoja miongoni mwetu."

Adam, ambaye anachezea klabu moja nchini Australia, pia ameona familia yake ikiathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

"Ilikuwa vigumu sana," alisema.

"Wengi wa familia yangu wamehamia Misri na wengine wamekwenda Sudan Kusini pia. Ni matumaini yangu kuwa kila mtu anaweza kuwa salama na siku moja atarudi nyumbani katiak nchi yetu pendwa."

g

Sudan inakaa kileleni mwa jedwali la kundi B baada ya mechi nne za mbio za kufuzu kwa mechi 10, ambayo itaanza tena mwezi Machi mwaka ujao.

Mahojiano ya Mark Lomas na Nishat Ladha.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi