Viwanja 10 vitakavyotumika kwenye mashindano nchini Ujerumani

D

Chanzo cha picha, EPA

Uerumani ni mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Ulaya 2024 (Euro 2024), miaka 18 imepita tangu kuandaa Kombe la Dunia, ambalo Italia ilishinda.

Fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya zitafanyika msimu wa joto kati ya Juni 14 na Julai 14 katika viwanja 10 katika miji 10 ya Ujerumani. Viwanja tisa kati ya kumi vilitumika katika Kombe la Dunia la 2006, isipokuwa Dusseldorf Arena.

Ni muhimu kukumbuka kuwa jiji la Munich ni mwenyeji kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuwa miongoni mwa majiji11 kuwa mwenyeji wa shindano hilo katika msimu wa joto wa 2021.

Pia unaweza kusoma

Olympiastadion, watazamaji elfu 71

X

Chanzo cha picha, REUTERS

Ni uwanja ambao mechi za timu ya Hertha Berlin (ambayo kwa sasa inashiriki ligi ya daraja la pili) huchezwa, ulikuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya 1936, fainali ya Kombe la Dunia ya 2006 na fainali ya Ligi ya Mabingwa 2015, na umekuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la Ujerumani kila mwaka tangu 1985.

Uwanja wenye uwezo wa kubeba watazamaji elfu 71 katika jiji la Berlin, utakuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la mataifa ya Ulaya 2024 mnamo Julai 14.

Ulifunguliwa Agosti 1936 wakati wa utawala wa Wanazi na ukakarabatiwa 2000 na 2004. Berlin, ambao kwa sasa ndio mji mkuu wa Ujerumani baada ya kuunganishwa 1990, ni moja ya miji inayovutia.

Jiji hilo linalovutia watalii, limejaa historia na utamaduni, kama vile lango la Brandenburg na mnara wa televisheni wenye urefu wa mita 368.

Allianz Arena, elfu 66

K

Chanzo cha picha, PA MEDIA

Uwanja huo ulijengwa na Bayern Munich na timu ya Munich 1860, ulifunguliwa mwaka 2005, kabla ya Bayern kuchukua umiliki kamili.

Ulikuwa mwenyeji wa ufunguzi wa Kombe la Dunia la 2006 na fainali ya Ligi ya Mabingwa ya 2012, wakati Chelsea ilipoishinda mwenyeji Bayern Munich kwa mikwaju ya penalty. Pia mechi za Kombe la Ulaya la 2020 katika msimu wa joto wa 2021 zilichezwa.

Ndio uwanja wa mechi ya ufunguzi kati ya Ujerumani na Scotland Juni 14 na moja ya mechi mbili za nusu fainali.

Munich ni nyumbani kwa watu milioni 1.6. Ni jiji la tatu kwa ukubwa nchini Ujerumani, eneo lililojaa historia, majumba, bustani na kitovu cha unywaji bia.

Signal Iduna Park, elfu 62

I

Chanzo cha picha, REUTERS

Uwanja wa timu ya Borussia Dortmund ni mojawapo ya viwanja maarufu duniani kutokana na ukuta wa njano wa mashambiki. Ulifunguliwa mwaka 1974 na ukafanyiwa ukarabati 2003.

Umetumika kwenye mechi muhimu, ikiwa ni pamoja na Fainali ya Kombe la UEFA ya 2001 kati ya Liverpool ya Uingereza na Alaves ya Uhispania.

Utatumika kucheza moja ya mechi mbili za nusu fainali katika Kombe la Ulaya la 2024.

Dortmund ni kitovu cha utamaduni wa eneo la Ruhr. Eneo hilo lilikuwa maarufu miaka hamsini kwa makaa ya mawe, chuma na bia, lakini kwa sasa ni maarufu kwa teknolojia.

MHPArena, elfu 51

JK

Chanzo cha picha, EPA

Uwanja huo umekarabatiwa na kuwa wa kisasa zaidi tangu kujengwa kwake 1933. Ulitumika katika katika Kombe la Dunia la 1974 na 2006, Kombe la Ulaya la 1988 na fainali ya Kombe la Ligi ya Mabingwa 1959 na 1988, pamoja na Riadha ya Dunia ya 1993.

Upo katika mji wa Stuttgart, ni mojawapo ya miji muhimu ya viwandani na makao makuu ya watengenezaji magari Mercedes na Porsche.

Volksparkstadion, elfu 49

K

Chanzo cha picha, EPA

Uwanja huo ulifunguliwa kwa mara ya kwanza mwaka1953, ukafanyiwa ukarabati mwaka 2000, na kuandaa mechi za Kombe la Ulaya la 1988 na Kombe la Dunia la 1974 na 2006.

Volksparkstadion upo katika mji wa Hamburg, mji wenye bandari kubwa ya kimataifa, historia tajiri ya kitamaduni, usanifu mzuri majengo na maisha ya usiku ambayo huwa kivutio kwa watalii wengi.

Mercur Spiel Arena, elfu 47

J

Chanzo cha picha, EPA

Unamilikiwa na timu ya Fortuna Düsseldorf, ambayo ilishiriki mara ya mwisho ligi kuu katika msimu wa 2019/2020.

Uwanja huo, ambao zamani ulijulikana kama Reheinstaedon, ulikuwa mwenyeji wa mechi za hatua ya makundi za Kombe la Ulaya la 1988.

Dusseldorf, mji mkuu wa jimbo la Rhine-Westphalia Kaskazini, mji huo una wakazi 650,000. Rhine-Westphalia ni jimbo lenye watu wengi zaidi nchini Ujerumani.

RheinEnergieStadion, elfu 43

K

Chanzo cha picha, PA MEDIA

Uwanja wa klabu ya Cologne, ilishuka daraja hadi daraja la pili, ulikarabatiwa kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia 2006, baada ya kufunguliwa mwaka 1923 na kufanyiwa ukarabati wa awamu ya kwanza mwaka 1975.

Ulikuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Ulaya 1988, Kombe la Shirikisho 2005 na Kombe la Dunia la 2006.

Tangu 2010, hutumika kwa fainali ya Kombe la Wanawake la Ujerumani, pamoja na mechi za kandanda za Amerika, kwa mpira wa magongo na matamasha.

Cologne nyumbani kwa zaidi ya watu milioni moja. Ni nyumbani kwa maeneo muhimu zaidi ya watalii nchini Ujerumani kama Kanisa Kuu la St. Peter, urithi wa dunia wa UNESCO.

Deutsche Bank Park, elfu 47

M

Chanzo cha picha, REUTERS

Uwanja wa timu ya Eintracht Frankfurt ulifunguliwa Mei 1925. Ulikuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Dunia la 1974, ikijumuisha ufunguzi, Kombe la Ulaya la 1988, Kombe la Shirikisho la 2005 na Kombe la Dunia la 2006.

Frankfurt ni eneo la kimataifa la fedha na biashara, mji huo uko kwenye kingo za mto Main. Ni jiji la tano kwa ukubwa nchini Ujerumani na maghorofa yake ya kipekee limepewa jina la utani "Manhattan.”

Red Bull, elfu 40

J

Chanzo cha picha, EPA

Ni uwanja wa kisasa wenye paa la kisasa ambalo lilifunguliwa mwaka 2004. Ni uwanja pekee utakao chezewa kombe la Ulaya katika eneo la iliyokuwa Ujerumani Mashariki.

Ulitumika katika mechi za Kombe la Dunia la 2006. Ni uwanja wa klabu mpya ya RB Leipzig tangu 2010.

Mji wa Leipzig umejaa historia na ndipo alipoishi mwanamuziki Johann Bach siku za nyuma. Mji huo ulishuhudia maandamano ya amani mwaka 1989 huku Ujerumani ikijiandaa kuunganisha sehemu hizo mbili.

Veltins, elfu 50

K

Chanzo cha picha, REUTERS

Uwanja huo ulifunguliwa mwaka 2001 na ni nyumbani kwa timu ya Schalke FC, bingwa mara saba wa Ujerumani na kwa sasa inashiriki ligi ya daraja la pili.

Una paa linaloweza kufunguliwa na kufungwa. Uwanja huo uliandaa fainali ya Ligi ya Mabingwa ya 2004 na robo fainali ya Kombe la Dunia la 2006.

Upo katika jiji la Gelsenkirchen, lililokuwa maarufu kwa makaa ya mawe na chuma, lakini siku hizi ni kijani kibichi, sinema, safari za boti, na viwanda vya kale.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah