Nani atakuwa mfungaji bora wa Euro 2024?

Chanzo cha picha, BBC Sport
Taji la Henri Delaunay linaweza kuwa tuzo kuu katika michuano ya Uropa msimu huu, lakini kwa mchezaji binafsi kuna nafasi pia ya kuwa mfungaji bora na kutwaa Kiatu cha Dhahabu.
Gerd Muller, Marco van Basten, Alan Shearer na Fernando Torres ni miongoni mwa walioongoza orodha ya wafungaji kwa miaka mingi.
Kwa hivyo ni nani atafanya hivyo wakati huu?
BBC Michezo imewatathmini baadhi ya wagombea...
Romelu Lukaku (Ubelgiji)

Chanzo cha picha, Getty Images
Romelu Lukaku atapendwa sana na wengi baada ya kufunga mabao 14 na kuvunja rekodi ya kufunga kwenye mechi moja ya kufuzu kwa Ubingwa wa Ulaya.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ubelgiji akiwa amefunga mabao 83 katika mechi 114 na michuano ya Euro msimu huu wa kiangazi itakuwa ni michuano yake ya sita mikubwa akiwa na Red Devils.
Alitwaa Kiatu cha Shaba kwenye Kombe la Dunia la 2018 baada ya kufunga mara nne katika mechi saba.
Cody Gakpo (Uholanzi)

Chanzo cha picha, Getty Images
Cody Gakpo anaonekana kuwa mshindani mkuu wa Kiatu cha Dhahabu kutoka Uholanzi.
Mshambuliaji huyo wa Liverpool alikuwa mfungaji bora wao kwenye Kombe la Dunia la 2022 akiwa na mabao matatu, baada ya kufunga katika mechi zao zote tatu za makundi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amefunga mabao tisa katika mechi 23 za kimataifa kwa ujumla.
Gianluca Scamacca (Italy)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashabiki wanaofuatilia Ligi Kuu ya England mara kwa mara watamkumbuka Gianluca Scamacca kwa muda mfupi aliocheza West Ham msimu wa 2022-23, ambapo alifunga mabao matatu pekee ya ligi.
Lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amegundua upya kiwango chake bora tangu arejee Atalanta, akifunga mara 19 katika mashindano yote na kuisaidia timu hiyo ya Italia kushinda Ligi ya Europa.
Alifunga bao lake la kwanza kwa Italia katika mechi yao ya kufuzu dhidi ya Uingereza kwenye uwanja wa Wembley mnamo Oktoba.
Robert Lewandowski (Poland)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa Poland Robert Lewandowski ilivunja mioyo ya Wales kwa ushindi wa hatua ya mtoano kwa mikwaju ya penati na kuwa moja ya timu za mwisho kupata nafasi yao huko Ujerumani.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 hakika anajua wavu ulipo. Ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Poland akiwa na mabao 82 katika mechi 148 na amefunga zaidi ya mara 600 kwenye soka la klabu na nchi katika kipindi chake cha miaka 19.
Alifunga mabao matatu katika mechi nyingi zaidi kwenye Euro 2020 na Euro msimu huu wa kiangazi utakuwa mchuano wake wa sita wa kimataifa.
Cristiano Ronaldo (Ureno)

Chanzo cha picha, Getty Images
Huyu ni mchezaji mwingine ambaye hahitaji kutambulishwa. Nyota wa kandanda Cristiano Ronaldo anaonyesha dalili ndogo ya kupunguza kasi yake hata akiwa na umri wa miaka 39.
Ndiye mfungaji bora wa muda wote wa soka la kimataifa na amefunga mabao 128 akiwa na Ureno na ndiye aliyeweka rekodi ya kucheza mechi 206.
Msimu huu wa kiangazi utakuwa mchuano wake wa 12 wa kimataifa na unampa nafasi ya kushinda Viatu vya Dhahabu mfululizo, baada ya kuongoza orodha ya wafungaji kwenye Euro 2020 akiwa na mabao matano.
Harry Kane (England)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mfungaji bora wa muda wote wa Uingereza Harry Kane atakuwa tena kiini cha matumaini yao ya kumaliza miaka 58 ukame wa mataji msimu huu wa joto.
Nahodha huyo wa Three Lions anaingia kwenye michuano hiyo akiwa nje ya msimu wa kwanza akiwa na Bayern Munich, ambapo alifunga mabao 45 katika mechi 45.
Licha ya mafaniko ya kibinafsi, Kane ameendelea kusubiri kwa muda mrefu kupata heshima ya kwanza baada klabu yake ya Bayern kumaliza msimu bila taji lolote.
Kylian Mbappe (Ufaransa)
Mshambulizi mahiri wa Ufaransa, Kylian Mbappe ndiye anayepigiwa upatu kufunga mabao mengi kwenye michuano ya Euro 2024.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amefunga mabao 46 katika mechi 77 pekee akiwa na Les Bleus, ambao wanalenga kunyanyua kombe hilo kwa mara ya tatu baada ya ushindi wa mwaka 1984 na 2000.
Mbappe alishinda Kiatu cha Dhahabu kwenye Kombe la Dunia la 2022 akiwa na mabao manane - ikiwa ni pamoja na hat-trick kwenye fainali hiyo kuu ya fainali dhidi ya Argentina.

Chanzo cha picha, Getty Images
Rasmus Hojlund (Denmark)

Chanzo cha picha, Getty Images
Rasmus Hojlund ni nyota anayechipukia wa kandanda ya Denmark ambaye tayari anaheshimika nyumbani na kimataifa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alifunga hat-trick katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa katika mechi ya kufuzu kwa Uropa dhidi ya Finland mnamo Machi 2023 na kumaliza michuano hiyo kama mfungaji bora kwa mabao saba katika mechi nane.
Aliigharimu Manchester United pauni milioni 72 kutoa klabu ya Atalanta msimu uliopita wa joto na licha ya msimu wa kupanda na kushuka aliweza kufunga mabao 16 katika mechi 43 katika mashindano yote huku Mashetani Wekundu wakinyanyua Kombe la FA.
Scott McTominay (Scotland)

Chanzo cha picha, Getty Images
Scott McTominay alikuwa hirizi ya Scotland wakati wa kampeni yao ya kufuzu kwani Tartan Army ilifikia Ubingwa wao wa pili mfululizo wa Uropa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alimaliza akiwa mfungaji bora wa taifa lake katika michuano ya kufuzu akiwa na mabao saba, huku Lukaku, Kane na Ronaldo pekee wakifunga zaidi.
Kama mchezaji mwenzake Rasmus Hojlund, McTominay anaelekea Ujerumani akiwa na furaha baada ya kusaidia Manchester United kuwashinda wapinzani wao Manchester City na kushinda Kombe la FA.
Aleksandar Mitrovic (Serbia)

Chanzo cha picha, Getty Images
Aleksandar Mitrovic ni kiungo muhimu kwa Serbia inapojiandaa kwa michuano yao ya kwanza ya Ulaya kama taifa huru.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, mfungaji bora wa muda wote wa Serbia akiwa na mabao 57 katika mechi 89 na aliongoza orodha ya wafungaji bora katika kufuzu akiwa na mabao matano.
Mitrovic amefurahia msimu mzuri katika ngazi ya ndani baada ya kuondoka Fulham kwenda Saudi Pro League mwezi Agosti, akifunga mabao 39 katika mechi 42 pekee katika michuano yote huku Al Hilal ikishinda taji.
Zeki Amdouni (Uswizi)

Chanzo cha picha, Getty Images
Zeki Amdouni alikuwa mmoja wa nyota waliochipukia katika kufuzu Ulaya, akifunga mabao sita katika mechi tano pekee huku Uswizi ikifuzu kwa michuano yao mikuu ya sita mfululizo.
Wamevuka hatua ya 16 bora mara moja tu wakati huo - na kufika robo fainali kwenye Euro 2020.
Iwapo watakwenda mbali zaidi 2024 basi Amdouni, ambaye alifunga mabao sita katika mechi 36 akiwa na Burnley iliyoshuka daraja msimu uliopita, anaweza kuwa mtu muhimu.
Alvaro Morata (Uhispania)

Chanzo cha picha, Getty Images
Alvaro Morata atakuwa nahodha wa Uhispania huku wakipania kunyanyua kombe hilo kwa mara ya tatu.
Mshambuliaji huyo mzoefu wa Atletico Madrid, ambaye alikaa Chelsea kwa miaka mitatu kati ya 2017 na 2020, amefunga mabao 34 katika mechi 74 za kimataifa.
Hakuna mchezaji mwingine katika kikosi cha Uhispania Euro 2024 ambaye amefikia idadi mara mbili.
Niclas Fullkrug (Ujerumani)

Chanzo cha picha, Getty Images
Niclas Fullkrug huenda alilazimika kusubiri hadi alipokuwa na umri wa miaka 29 ili kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa, lakini kwa hakika anaitumia vyema nafasi hiyo.
Mshambuliji huyo wa Borussia Dortmund, ambaye sasa ana umri wa miaka 31, amefunga mabao 11 katika mechi 15 za kimataifa na anatazamiwa kuongoza mashambulizi ya wenyeji msimu huu wa joto.
Aliifungia Dortmund mabao 15 msimu uliopita na kuisaidia kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo walichapwa 2-0 na Real Madrid.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












