Wachezaji wa Afrika wanaosaka heshima na historia Ulaya

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ademola Lookman (kushoto) atachuana na mchezaji mwenzake wa Nigeria, Victor Boniface (kulia) katika fainali ya Ligi ya Europa siku ya Jumatano.

Mashindano makubwa ya vilabu barani Ulaya yanafikia kilele chake na wachezaji kadhaa wa Kiafrika wanatarajia kuandika historia.

Kuna uwakilishi mkubwa kutoka Afrika katika fainali zote tatu za Ulaya, timu sita zinazoshiriki zote zina Waafrika katika safu zao za kwanza.

Kuna wachezaji wa Afrika ambao wametoa mchango muhimu na ambao utawawekea historia katika muda wa wiki moja na nusu ijayo.

Pia unaweza kusoma

Boniface akisaka kombe la tatu

Kikosi cha Bayer Leverkusen, kitamenyana na Atalanta katika fainali ya Ligi ya Ulaya UEFA, Jumatano – kinasaka ushindi wa makombe matatu katika msimu huu.

Leverkusen walifanikiwa kuweka rekodi barani Ulaya kwa michezo 51 bila kushindwa – walipoifunga dhidi ya Augsburg siku ya Jumamosi huku Victor Boniface wa Nigeria, akifungua ukurasa wa mabao kwa mabingwa hao wa Ujerumani.

Mshambulizi huyo, pamoja na mwenzake Nathan Tella wa Nigeria, watamenyana na mchezaji mwenzao wa kimataifa wa Nigeria, Ademola Lookman wa Atalanta, ambaye alikuwa muhimu katika kusaidia Super Eagles (Nigeria) kumaliza kama washindi wa pili katika Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi Februari.

Kutakuwa na sura za wachezaji wa Afrika Magharibi katika fainali hiyo itakayofanyika Dublin, Ireland wachezaji kutoka Burkina Faso, Ivory Coast na Mali pia wakiwakilisha.

Odilon Kossounou wa Leverkusen anaweza kuongeza taji la Ligi hiyo ya Ulaya kwenye medali yake ya washindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika, aliyoitwaa akiwa na Ivory Coast.

Huku mlinzi mwenzake Edmund Tapsoba na mshambuliaji wa Morocco Amine Adli pia wakiwa wamecheza mara kwa mara Leverkusen msimu huu.

Winga Lookman na mshambuliaji wa Mali El Bilal Toure wote walifunga katika mechi ya mkondo wa pili ya nusu fainali na kuisaidia Atalanta kufika fainali ya kwanza ya Ulaya kabla ya wawili hao kukosa kunyanyua kombe la Coppa Italia dhidi ya Juventus wiki iliyopita.

Je, El Kaabi kutwaa ubingwa?

rdf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ayoub El Kaabi amefunga mabao 32 tangu ajiunge na Olympiakos akitokea Al-Sadd ya Qatar Agosti mwaka jana.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya kuweka rekodi ya mataji 47 ya ligi ya Ugiriki, Olympiakos bado hawajanyakua taji kubwa la Ulaya.

Miamba hao kutoka bandari ya Piraeus wanaweza kuweka rikodi mpya dhidi ya Fiorentina ya Italia kwenye ligi ya Europa Conference wiki ijayo - na Ayoub El Kaabi wa Morocco amekuwa chanzo kikuu cha kusonga mbele hadi fainali.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ndiye mfungaji bora katika mashindano ya msimu huu akiwa na mabao 10 - huku nusu ya idadi hiyo akiipata katika ushindi wa nusu fainali dhidi ya Aston Villa.

El Kaabi alifunga magoli matatu katika mechi ya kwanza, ushindi wa 4-2 ugenini, na kuongeza magoili mawili katika mchezo wa marudiano na kupata ushindi wa jumla wa 6-2.

Mshambulizi mwenzake wa Morocco, Youssef El Arabi na kiungo wa Guinea, Mady Camara pia walikuwepo katika michezo hiyo.

Fainali ya Jumatano, Mei 29 itachezwa katika uwanja wa wapinzani wao timu ya AEK Athens, kutaufanya ushindi wa taji hilo kuwa mtamu zaidi kwa Olympiakos.

Watacheza na La Viola, ambao wana mshambuliaji wa Angola, M'bala Nzola na kiungo wa kati wa Ghana, Alfred Duncan katika safu yao.

Nzola amefunga mabao matatu - ikiwa ni pamoja na bao la dakika za majeruhi katika mechi ya mkondo wa kwanza wa mchujo wa robo fainali dhidi ya Club Bruges - na kutoa pasi mbili za mabao, huku Duncan amecheza mechi tano ugenini.

Haller kusaka ushindi

x

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Je, Sebastien Haller atakuwa fiti kuisaidia Borussia Dortmund kushinda taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa tangu 1997?

Borussia Dortmund watamenyana na wababe wa Uhispania Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa huko London Jumamosi, Juni 1 katika uwanja wa Wemblay.

Sebastien Haller wa Borussia Dortmund, mshambulizi mwenye umri wa miaka 29 alifanikiwa kurejea tena uwanjani baada ya kupona saratani ya tezi dume na alifunga bao la ushindi katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Ivory Coast mwezi Februari.

Sasa, anaweza kuwa mtu wa tatu kutwaa ubingwa wa bara la Afrika na Ulaya katika msimu huo huo.

Wachezaji wawili wa zamani wa Cameroon, Samuel Eto'o na Geremi Njitap waliisaidia Real kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2000 baada ya kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huo huo.

Haller ana jeraha la kifundo cha mguu katika wiki za hivi karibuni na anaweza kuwekwa benchi, na mlinzi wa Algeria, Ramy Bensebaini bila shaka atakosa kuicheza Dortmund baada ya kupata jeraha mwezi Machi.

Real wanasaka ushindi wa 15 wa Kombe la Ulaya/Ligi ya Mabingwa, huku kocha wao Carlo Ancelotti akitafuta kubaki na kombe hilo.

Brahim Diaz, ambaye aliichezea Morocco kwa mara ya kwanza mwezi Machi baada ya kuamua kuichezea Morocco badala ya Uhispania, amefunga mabao nane na alitoa pasi za mwisho saba kwa Real katika ligi ya La Liga.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 kwa kiasi kikubwa amekuwa akitumika kama mchezaji wa akiba katika klabu hiyo ya Madrid, lakini ana matumaini ya kushinda kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya kuwa kwa mkopo nchini Italia akiwa na AC Milan kwa misimu mitatu.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah