Je, timu hii ya Man Utd ni 'moja ya timu mbaya zaidi kuwahi kutokea'?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Manchester United wakisaka bao la kusawazisha dhidi ya Arsenal siku ya Jumapili, anga ya buluu juu ya Old Trafford ilitoa nafasi ya ngurumo na mvua kubwa.
Hali hiyo inaweza kuwa kielelezo kwa msimu wa Man United, ambapo matumaini ya kumenyana na The Gunners pamoja na Manchester City kileleni mwa jedali yamegeuka na kuwa kampeni nyingine ya kukatisha tamaa.
Katika miaka ya nyuma, mechi kati ya Manchester United na Arsenal zilikuwa kati ya pande mbili zinazomenyana kileleni mwa jedwali, lakini safari hii jukumu la kikosi cha Erik ten Hag lilikuwa kuwa mharibifu katika mbio za kuwania taji la wapinzani wao, kazi ambayo walishindwa kutimiza.
"Hii ni moja ya timu mbaya zaidi za Manchester United kuwahi kutokea," kiungo wa zamani wa Mashetani Wekundu Robbie Savage alisema kwa ukali, huku akitazama timu yake ya zamani ikijaribu bila mafanikio kupata bao la kusawazisha dhidi ya The Gunners.
Mwishowe, bao la kipindi cha kwanza la Leandro Trossard lilithibitika kuwa muhimu Arsenal ilipoondoka Old Trafford na pointi tatu ambazo ziliwapandisha kileleni mwa jedwali na kuhakikisha wanapambana na Manchester City kuwania taji la Ligi Kuu hadi siku ya mwisho.
"Walionikatisha tamaa haswa nusu saa iliyopita, ilikuwa Manchester United," nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Roy Keane, alisema kwenye Sky Sports.
"Dhidi ya timu hiyo leo, Arsenal hawakuamini jinsi United ilivyokuwa katika hali mbaya."

Chanzo cha picha, Getty Images
"Wachezaji wanatakiwa kujitazama wenyewe''
Katika maelezo yake ya mpango wa kabla ya mechi, Ten Hag alikuwa ameitaka timu yake kuonesha umahiri wao na kurekebisha kichapo cha 4-0 walichokipata dhidi ya Crystal Palace wiki iliyopita.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini, kwa Keane, unahiri huo haukuonekana popote.
"Ukitazama nusu saa iliyopita - kufanya maamuzi, hakuna mtu anayemlaumu yeyote, watu wanafanya makosa na kuanguka, na kila mtu anaondoka tu, hakuna mtu anayemlaumu mwengine," aliongeza.
"Hii ndio ndio timu mbaya zaidi ya United - mbaya sana."
Hatahivyo ushindi mwembamba wa Arsenal dhidi ya Man United hauonekani kuwa matokeo mabaya kwa United ilioanza mechi hiyo ikiwa katika nafasi ya 8 na pointi 29 nyuma ya The Gunners.
Lakini kilikuwa ni kipigo chao cha 14 msimu huu katika Ligi ya Premia - zaidi ya timu nyingine yoyote ile katika nusu ya juu ya jedwali - ambacho kinawaacha katika hatari ya kutokuwepo tena katika soka ya barani Ulaya msimu ujao.
Pia wamepoteza mechi tisa nyumbani Old Trafford muhula huu - nyingi zaidi wakiwa nyumbani kwa msimu mmoja - na wameruhusu mabao 82 katika mashindano yote, ambayo ni mengi kwao tangu 1970-71.
"Unapopoteza michezo kwa jinsi Manchester United walivyo kwa sasa kutakuwa na maswali kutoka kwa meneja," mfungaji bora wa klabu hiyo Wayne Rooney alisema kwenye Sky Sports.
"Lakini nadhani wachezaji wanatakiwa kujiangalia. Kwa baadhi ya wachezaji inaonekana wanajaribu tu kufikia mwisho wa msimu.
"Iwapo wanamchezea Erik ten Hag sidhani kama wanafanya hivyo kwa kweli"

Chanzo cha picha, Getty Images
'Ni kama kuogelea huku ukiwa umeweka mikono yako mgongoni'
Mustakabali wa Ten Hag Old Trafford bado haujulikani. Ana mwaka mmoja kwenye mkataba wake lakini kumekuwa na uvumi unaokua ukiongezeka kwamba mmiliki mwenza Sir Jim Ratcliffe, ambaye alitazama mechi siku ya Jumapili, anaweza kufanya mabadiliko.
Kocha huyo wa zamani wa Ajax inaeleweka anaashiria kiasi cha majeraha ambayo timu yake imelazimika kukabiliana nayo msimu huu.
"Kila meneja anaweza kufanya vyema kila wakati," alisema baada ya mechi ya Jumapili. "Nimekuwa hapa kwa miaka miwili na mara moja tu nilikuwa na kundi kamili la wachezaji.
"'Ni kama kuogelea huku ukiwa umeweka mikono yako mgongoni na inabidi kuweka kichwa chako juu ya usawa wa maji."
Licha ya masuala ambayo United imekuwa nayo msimu huu, wanatarajiwa kucheza katika fainali ya kombe la FA.
Lakini wapinzani wao katika mchezo huo ni Manchester City na Ten Hag anajua kikosi chake kitahitaji kuonyesha umahiri wa hali ya juu zaidi ikiwa wanataka kumaliza msimu wa kusikitisha wakiwa juu.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












