Waridi wa BBC: 'Jinsi vipodozi vikali vilivyoharibu ngozi yangu'

    • Author, Martha Saranga
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Baada ya kufanya 'facial ', sura ilibadilika na kuwa ya kutisha.Nilishtuka baada ya kuamka asubuhi kila mtu ananishangaa sura imevimba na kuwasha," anasimulia Nice Aston ambaye ni mkazi wa jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania.

Nice mwenye miaka 32, anasema aliingia kwenye mtego baada ya kuuliza wenzake aliowaona wana ngozi nyororo usoni, walitumia nini? ndipo akaanza kutafuta vipodozi mtaani ili kuondokana na chunusi zilizompotezea hali ya kujiamini.

Anasema kuwa hakuwa na elimu yoyote kuhusu masuala ya ngozi wakati anaanza kutafuta ufumbuzi wa chunusi zilizomkera mwilini mwake kwa kipindi kirefu.

Hatahivyo, baada ya kuvunja ungo Nice aliamini chunusi zilizomtokea usoni mgongoni na kifuani zingekwisha kabisa kama ambavyo baadhi ya watu waliomzunguka walivyokuwa wakimuambia.

Anasema hakuona mabadiliko yoyote hata baada ya kukua, na alipoanza kujitegemea na kupata fedha aliamua kutafuta suluhisho la tatizo lake.

Nice anasema hali ya watu kumtania ilimfanya awe mwenye huzuni mara kwa mara.

"Nilijichukia, watu waliniambia 'una chunusi kama choroko'. Mwingine anakwambia mnajichubua ndio maana mnaharibika ngozi,"alieleza.

Anadai kuwa kauli za kuudhi kutoka kwa baadhi ya watu zilimsukuma kutaka mabadiliko kwa kutafuta vipodozi mbalimbali ambavyo navyo havikubadili hali yake kwa wakati huo.

Unaweza kusoma

Kwanini alitafuta vipodozi mtaani?

Katika kuhangaika kufuatilia suluhu ya masuala ya urembo na ngozi, Nice anasema alishauriwa kufanya 'facial' yaani kusafishwa uso kwa vipodozi akiamini kuwa itatibu tatizo la chunusi.

Anasema siku moja baada ya kufanya 'facial' aliamka na kukuta hali yake imekuwa mbaya huku sura ikiwa imevimba kama imeungua, kuwasha na ngozi kubanduka.

Anasema,"Niliogopa sana na kupiga simu kwa watoa huduma ya 'facial' nilikohudumiwa wakaniambia utakuwa umekosea masharti."

Nice anasema hatosahau namna aliivyojiskia vibaya na kujuta kufanya 'facial' na kwamba hali ya chunusi aliyokuwa nayo ilikuwa bora kuliko sura ya kutisha aliyoipata baadaye.

Nice anasema hakujua kuwa vipodozi alivyotumia vilikuwa na viambata vyenye sumu ambavyo viliharibu ngozi yake zaidi kuliko awali.

Unaweza pia kusoma

Nilikosa nafasi ya kazi katika kituo cha runinga kisa sura kuharibika

Katika hali isiyo ya kawaida, Nice anasema alienda kwenye usahili wa kazi ya utangazaji akaambiwa kuwa sura yake imeharibika na kwamba hawezi kuwa mtangazaji wa runinga.

Anasema aliamua kujifungia ndani bila kwenda kokote akiangalia filamu na kuchezea simu.

"Wakati mwingine nilikosa usingizi, na kupata maumivu makali ya kichwa na baadaye kutumia dawa za usingizi ili kunisaidia kukabiliana na tatizo langu japo ilikuwa ngumu kupata dawa hizo," alisema.

Tangu hapo alianza kumeza dawa za usingizi alizonunua kinyemela ili kumsaidia kupunguza mawazo na hata nyakati nyingi anadai ziliathiri mzunguko wake wa hedhi.

Niliamua kujitenga na familia yangu,faraja pekee ikiwa mchumba wangu

Nice hakuamini kilichomkuta na kwamba aliamua kujitenga na familia kwa kuhofia kutoeleweka kwa kile kinachoonekana usoni kwake.

"Sikuweza kuwasiliana na familia yangu kwani mama yangu ni mkali sana…kwa aina ya malezi aliyotulea nisingethubutu kueleza nimetumia nini na kupelekea kuharibu ngozi yangu," anasema.

Anasema faraja pekee aliyopata ni kwa mchumba wake ambaye mara zote hakuchoka kumsisitiza kuwa anapaswa kujikubali.

Anaongeza kuwa, "Baadae niliafiki kuonana na daktari bingwa wa ngozi ambaye kabla ya kunipatia matibabu alianza kwa kunipatia elimu kuhusu hali yangu ya chunusi na namna gani nilipaswa kujikubali."

Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa nimeweza kujikubali na kuachana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa za usingizi.

Alipatiwa matibabu na kuyafuatilia kwa uaminifu.

Watu walishangaa nilipoanza kupona na kujikubali

Baadhi ya watu waliona mabadiliko na kumuuliza kulikoni? "Nilianza kujichanganya na watu na hata kufungua mtandao wa kijami na kusimulia ushuhuda wangu ili watu wengine wajifunze,''anaeleza na kuongeza kuwa baadhi ya watu wakimuona hivi wanadhani anajichubua.

Kupitia mitandao yake ya kijami kama 'instagram' na 'Tiktok' Nice amepata wafuasi wengi huku wale wasiomwelewa wakikazana kumbeza na kumuita muongo wakati mwingine.

Anasema jamii bado ina idadi kubwa ya watu wasiozingatia afya ya ngozi na athari za matumizi ya vipodozi feki.

"Ni rahisi mtu kuniomba nimtajie ninachopaka na yeye akapake ang'ae haraka iwezekanavyo kutokana na kutojikubali rangi yake ya asili," anaeleza.

Chunusi zimenipa fursa

Nice anasema tatizo la chunusi lilimpa fursa kimaisha baada ya kutibiwa tatizo hilo, kwani alianza kutafuta maarifa kuhusu suala la ngozi na kusaidia watu wanaomzunguka.

'Watu wanaonifuata na hata kuniuliza kuhusu chunusi na namna nilivyopona ni wengi,hii imenifanya nitumie mitandao ya kijamii kutoa elimu na ushauri kwa vijana mbalimbali ambao ndio hasa wamekuwa wakinifikia kutaka ushauri'

Kupitia mitandao yake ya kijami kama instagram na Tiktok Nice amepata wafuasi wengi huku wale wasiomwelewa wakikazana kumbeza na kumuita muongo wakati mwingine.

Wakati mwingine baadhi ya wauzaji wa vipodozi huripoti machapisho yangu ya elimu kuhusu vipodozi feki ili nifungiwe ukurasa wangu wa mtandao.

Ushauri kwa jamii

Baada ya kujifunza kupitia changamoto zangu ninapenda kuwasihi wazazi wakae na vijana wao hasa kipindi cha balehe wawafundishe mabadiliko wanayopitia ili wasijikatae na kuanza kufanya mambo yasiyo faa.

Malezi na makuzi yangu yananihuzunisha kwani wazazi walikuwa wakali sana kiasi kwamba sikuweza kueleza pale nilipoona chunusi nyingi usoni na kila mtu ananibeza.

Nilitamani wazazi wanisikilize kuhusu changamoto yangu lakini haikuwezekana kutokana na ukali uliopitiliza.

Mtaalamu wa ngozi aeleza hatari ilivyo

Mtaalamu wa tiba ya ngozi nchini Tanzania, Eli Minja anasema kazi ya vipodozi ni kuboresha mwonekano wa mtu na sio kubalisha ngozi yake, ila, kuna baadhi ya vipodozi vinachanganywa na kemikali zinazobadilisha ngozi na kusababisha athari.

Mtaalamu huyo anasema matumizi ya baadhi ya vipodozi uleta athari kutokana na aina ya kemikali iliyochanganywa, muda wa matumizi na hata sehemu inapopakwa.

Eli anaongeza kuwa athari hizo upelekea ngozi kuwa nyembamba na kuchubuka kwa urahisi, kupata vidonda na michirizi lakini pia kuzeeka mapema.

Pia anasema athari nyingine ni kama kupungua kwa kinga ya ngozi, inayoleta urahisi wa kupata marathi kama fangasi au hata saratani ya ngozi.

Unaweza pia kusoma

Imehririwa na Lasteck Alfred