Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
WARIDI WA BBC : “Walinivua nguo zote kwa madai ya kuwa niliiba pete ya Bosi wangu Misri”
Na Anne Ngugi
BBC News Swahili
Irene Lavender mwanamke kutoka Kenya , mwenye miaka 25 aliondoka nchini mwake miaka mitatu na nusu iliyopita akitafuta maisha mazuri zaidi nchini Misri asijue kuwa mambo yaliomsubiria yalikuwa mazito na machungu .
Irene anasema kuwa baada ya kukamilisha shule ya sekondari hakupata kazi ya kuajiriwa , hali kadhalika wakati huo familia yake hususan mama yake mzazi hangemudu fedha za kumlipia chuo kwa mafunzo spesheli .Ndiposa mwanadada huyu aliamua kutafuta kazi za nyumbani nchini Misri kama njia ya kujikimu kimaisha .Mwaka wa 2020 Marchi 12 aliondoka kutoka nchini Kenya na kuelekea Misri .
“Nilipowasili Misri nilikuwa na msisimko wa kuzuru nchi nyengine , nakumbuka pia siku hio mvua ilinyesha sana , sikuwa nimezoea mazingira ya baridi iliyopitiliza , ila ilibidi nivumilie . Siku moja baada ya kuwasili, Misri ilitangazwa mlipuko wa Corvid 19 , hivyo basi kulazimisha mambo mengi kusimama ”anakumbuka Lavender
Ajira yenye dhuluma nyumba ya kwanza
Lavender alipata ajira ya kwanza akiwa Misri kwa jamii mmoja tajiri .Mwanadada huyu anasema kuwa ilikuwa mara ya kwanza kufanya kazi za ndani hivyo basi uzoefu wake ulikuwa mdogo wakati huo . Mwajiri wake mwanzoni alikuwa amemueleza kuwa kazi zake zitahusu kuwatunza watoto pekee , ila mwajiri wake alimficha kwamba angehusika na kazi za ziada kama za usafi , kufua na kadhalika .
“Jambo la kuridhisha ni kuwa watoto wa familia hio walinipenda sana , na kwa uzoefu wa kufanya kazi Uarabuni , iwapo watoto wa familia wangekuwa na urafiki na mfanyakazi basi alikubalika kwa urahisi , changamoto kuu niliyokuwa nayo ya kazi sikuwa na uzoefu wa kufanyakazi katika nyumba kubwa nikiifananisha na Kasri ”anakumbuka Irene
Baada ya kufanya kazi huko kwa wiki kadhaa Mwanamke aliyekuwa mwajiri wake Irene alianza kumzaba makofi na pia kumchapa kwa kila kosa ambalo angefanya .Kwa mfano anasema kuwa hakuwa na uzoefu wa kutumia mashine zinazotumia umeme kwa mfano za kufua , kuosha vyombo na hata za kupikia , hivyo basi hangeweza kuzitumia bila muongozo sahihi ambao hakupata wakati wa kuajiriwa kazi .
Irene anasema kuwa pia mwajiri wake alimshurutisha kufanya kazi kwa masaa 12 , kumaanisha kuwa kuna siku alisimama jikoni kwanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili kesho yake , huku mwajiri wake akiwa amemsimamia na kukagua kila kitu alichomuamrisha kufanya usiku huo kumaanisha kuwa hakulala usiku kucha .Na kwa hio mwanadada huyu anasema kuwa alichoka kupokea dhulma hizo na pia kelele za kila siku .
Cha kuzidisha uchungu kwenye kidonda Irene anasema kuwa mume wa mwajiri wake alikuwa na tabia za kumtomasa na kumshika shika kila wakati akiwa jikoni , huku akimwahidi kumpa pesa iwapo angesalia kimya kuhusu hali hio
“Kila wakati alipokuwa ananishika yule mwanamume alikuwa ananipa pesa , mimi nilizichukua kwani nilijua siku mmoja pesa hizo zingenisaidia kutoroka katika makao hayo kwani tayari nilikuwa nimechoka ”
Mwanamke huyu anasema kuwa kisa cha mwisho kilichomfanya atoke kwenye makao hayo ni kosa alilofanya la kutumia mashine ya kuosha vyombo visivyo na kilichofwatia na mwajiri wake kumtishia kumchoma kisu ila mume wa muajiri wake alimuokoa kutoka patashika hio .
Baada ya hapo Irene aliamua kutoroka kutoka makao hayo kwa usaidizi wa binamu wake aliyekuwa pia mjakazi huko Misri
Mateso ya kuvuliwa nguo nyumba ya kwanza
Irene alifanikiwa kupata ajira nyengine kwenye makao mapya huko Misri , kazi yake kuu ilikuwa kuwatunza watoto mapacha , na wakati mwingine kupakuwa chakula kwa jamii hiyo .
Katika makao hayo mwanadada huyu anasema kuwa mwanzo kila kitu kilikuwa shwari na hakuwa na shida na mwajiri wake , anakumbuka akiwa mkarimu kwake kiasi kwamba aliahidi kumrejesha chuo kikuu kwa mafunzo maalum , jambo ambalo halikufanyika.
Irene anasema kuwa mwajiri wake alikuwa na imani naye hasa kwa kuwa alikuwa na bidii ya kuwatunza watoto wake kama ilivyohitajika .
Ila anasema kuwa mwajiri wake (mama wa nyumba ) alianza kubadilika baada ya miaka miwili hivi , siku mmoja Irene anasema kuwa alisingiziwa kuwa alihusika na wizi wa mkoba maalum wa dhamani ambao ulikuwa wa muajiri wa kike , jambo ambalo lilimkasirisha mwanadada huyu na wakati wa likizo aliamua kuacha kazi katika makao hayo , Licha ya kuwa iligunduliwa kuwa yeye hakuhusika na kupotea kwa mkoba huo .
“Baada ya miezi mitatu nilipokea simu kutoka kwa mwajiri huyo huyo akinisihi nirejee kazini , nilimpa mwajiri wangu mazingira ya kurejea kazini ilikuwa ni iwapo atajadili swala la kusingizia kuwa nilihusika na wizi wa mkoba wake , aliridhia na kusema kuwa sio mimi niliyohusika , vile vile aliniongeza mshahara na ndiposa nikakubali kurejea huko “ anakumbuka Irene
Kisingizio cha wizi wa pete ya Bosi
Haikuchukua muda tena na mwanadada huyu anadai kuwa mwajiri wake alianza madai mapya kuwa mwanadada huyu alikuwa amehusika na wizi wa pete zake za dhamana kubwa.
Irene anasema kuwa kwa kipindi cha siku mmoja walishurutishwa kama wafanyakazi kuitafuta pete hio mchana kutwa , wakati huu wote Irene anasema kuwa mwajiri wake alitishia kuwa iwapo pete hio haingepatikana basi
‘damu ingemwagika’ . Irene anasema kwa kuwa hakuhusika alijua kuwa camera za CCCTV zingekuwa msema kweli . Ila mambo yalibadilika haraka mwanadada huyu anakumbuka siku zilizofuata mwajiri wake akihusika katika kumdhulumu , kumtusi kwa kupotea kwa pete .
“ Mwajiri wangu aliwaita wanaume wawili kwa kile alichokisema kuwa naadhibiwa ilinisema nilipoficha pete zake , Wanaume hao walinivua nguo zote huku wakisaka pete hio mwilini mwangu.Kitendo hiki kilinidhalalisha mno na kunipa aibu ambayo sitawahi kuisahau milele .”amakumbuka Irene
Ilipoonekana kuwa Irene alisimamia kidete kuwa hakuhusika na wizi huo , mwajiri wake aliwaachilia wanaume waliohusika na dhuluma , na akawasilishwa mikononi mwa polisi .
Irene anasimulia siku zilizojaa kiza kikuu ndani ya jela alikofungiwa huku akishurutishwa kusema alipoficha pete ya mwajiri wake .Hali iliendelea kuwa mbaya hadi alipowasilishwa mahakamani na Jaji akaamua kuwa hatma ya Irene ilikuwa arejeshwa nchini Mwake mara moja .
Irene alitejeshwa Kenya mwezi Machi mwaka huu .Mwanadada huyu anasema kuwa amesoma mengi kuhusiana na masaibu yake nchini Misri anatoa nsaha kwa watu wanaotafuta ajira nje ya nchi kwanza kuchunguza mazingira wanayopania kufanya kazi , na pia kuwa na watu wa karibu ambao wanaweza kuwafahamisha iwapo kutatokea dharura .
Imehaririwa na Seif Abdalla