Madai kwamba mhubiri Mkristo anacheza na simba ni ya 'uwongo'

Video inayomuonyesha mwanaume aliyevalia suti ya buluu akiwashika simba watatu imesambaa mitandaoni katika nchi kadhaa za Afrika, lakini madai kuwa mwanaume huyo ni mchungaji na anaonyesha uwezo wake wa kucheza na simba, kama watumiaji wengi wa mitandao wanavyodai ni ya uongo.

Katika filamu fupi, mtu aliyevaa suti ya bluu anaonekana akicheza na simba na wakati mmoja, akiweka mkono wake kwenye kinywa cha mmoja wao.

Nje ya uzio umati wa watu unatazama tukio hilo, wengine wakipiga picha au kuchukua video. Video inaonekana ni ya kweli na wala sio ya kutengeneza.

Kusambaa kwa video

Madai yameenea mitandaoni yakisema mchungaji wa kanisa akitengeneza upya hadithi ya Biblia ya Danieli katika zizi la simba ili kuthibitisha uwezo wake kwa waumini wake.

"Mchungaji Daniel aliwaleta waumini wa kanisa lake ili kuwaonyesha kwamba hakuna kitu kinachoweza kutokea kwa mtu wa Mungu," mwanablogu wa Nigeria aliandika kwenye Instagram.

Video hiyo imesambazwa sana nchini Ghana na Nigeria, lakini inaonekana inatoka Somalia.

Nchini Kenya, kituo cha televisheni cha ndani kiliiweka video hiyo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Na kupelekea mbunge wa Kenya, Ronald Karauri, kuandika kwenye mtandao wa X, zamani Twitter. "Ninajitolea kumpeleka Maasai Mara [mbuga ya wanyama], gharama zote nitalipa. Tutatafuta simba na yeye atatembea nao."

Mwanaume huyo ni nani?

BBC imemtambua mtu huyo, na si kiongozi wa kanisa. Baada ya ufuatiliaji, tulipata video kwenye YouTube ya mwaka wa 2021, iliyorekodiwa katika bustani ya watalii katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu - eneo hilo linalingana na lile la kwenye video ya sasa.

Pia, tuliweza kubaini kuwa mwanaume aliyehojiwa kwenye video ya Youtube ni Mohamed Abdirahman Mohamed, ni mtu yule yule katika video iliyosambazwa kote Afrika katika siku za hivi karibuni.

Yeye ni mlinzi wa bustani ya wanyama na amefanya kazi katika bustani hiyo kwa zaidi ya miaka minane.

Makala hayo yanaitaja mbuga ya watalii huko Mogadishu, na kwa kupekua jina kwenye TikTok kwa Kisomali, ilitupeleka kwenye akaunti ambapo video asili ilikuwa imewekwa.

Kuna video nyingine za Mohamed akiwa na simba, kongwe zaidi na ziliwekwa mwezi Machi mwaka huu.

Mohamed na BBC

Mohamed, mtu anayefuga simba, alizungumza na mwandishi wa BBC wa Somalia, Mohamed Abdiaziz mwaka jana.

Alisema amewafunza wanyama anaowachunga wakiwemo simba na nyoka na sasa anaweza kuwahudumia kwa usalama.

Wakati wa mahojiano na BBC Somali, alicheza na chatu, wakati fulani akiweka kichwa cha nyoka huyo mdomoni, na watu waliokaribu naye walipiga mayowe ya mshituko.

Mohamed alisema alijifundisha jinsi ya kufuga na kutunza wanyama pori na alikuwa na uhakika na uwezo wake.

"Hawana madhara, ni kama watoto wangu," aliiambia BBC Somali.