'Neurasthenia': Fahamu ugonjwa wa ajabu wa wanaume ambao sayansi imeshindwa kuelezea

Chanzo cha picha, Alamy
'Usiogope Kuru.' Hicho ndicho kilikuwa kichwa cha habari katika gazeti la Singapore la Novemba 7, 1967.
Siku chache zilizopita, jambo la kushangaza lilitokea nchini humo ambapo maelfu ya wanaume waliamini kwamba uume unapungua kwa sababu ya ugonjwa huo na hatimaye kusababisha kifo.
Nchi ilipozidi kuingiwa na hofu, wanaume, kwa kuogopa ugonjwa huu, walianza tabia ya ajabu. Watu waliogopa kwamba uume wao unaweza kuvunjika na hivyo wengine wakaufunga kwa nguo na wengine kwa msaada wa mpira.
Katika hali hiyo, madaktari walitajirika na walioshauri tiba asilia pamoja na kienyeji walipata pesa nyingi.
Uvumi pia ulianza kuenea kwamba kupungua ghafla kwa ukubwa wa uume kulitokana na baadhi ya vyakula ambavyo waathirika walidaiwa kula.
Madai mojawapo yalihusisha nyama ya nguruwe. Wakati huo huo, serikali pia ilikuwa imezindua mpango wa chanjo. Katika hali hiyo, uuzaji wa nyama ya nguruwe uliathirika.
Ili kutuliza taharuki hiyo, idara ya afya ilieleza kuwa suala hilo halikuwa na ukweli wowote zaidi ya hofu ya kisaikolojia, lakini halina athari na takriban watu 500 walikimbilia hospitali kupata matibabu.
Ikumbukwe kwamba hofu ya kupoteza uume ni ya kawaida zaidi kuliko unavyoweza kufikiri na inaonekana mara kwa mara katika tamaduni duniani kote.
Katika Asia ya Kusini-mashariki na Uchina, sasa inaitwa 'Kuro', ikifananishwa na kasa kwa sababu anaweza kuficha kichwa chake ndani ya ganda lake.
Historia ya Kuru ilianza maelfu ya miaka iliyopita, lakini tukio la hivi karibuni zaidi lilitokea mashariki mwa India mnamo 2015 wakati watu 57, wakiwemo wanawake wanane, walikumbwa na hofu hiyo.
Wanawake hao waliogopa kwamba chuchu zao zilikuwa zikinywea.
Koro ni ugonjwa wa kisaikolojia unaopatikana tu katika jamii fulani. Katika eneo moja la Haiti, watu mara kwa mara wanaugua ugonjwa wa kufikiria sana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ugonjwa kama huo unapatikana pia huko Korea Kusini ambapo watu hupuuza hisia zao wanapoonewa ama kutendewa isivyo haki, baada ya hapo inakuja wakati ambapo dalili hatari huanza kudhihirika, kama vile kugubikwa na hisia za kuwashwa mwili.
Takriban watu 10,000 nchini Korea Kusini wanaugua ugonjwa huu kila mwaka, na wengi wao ni wanawake wazee walioolewa.
Magonjwa haya ya akili ni makubwa na huathiri afya ya akili ya idadi kubwa ya watu. Dalili zinazohusishwa na vyanzo vya kitamaduni zinaweza pia kuwa mbaya.
Athari za Koro zinaweza kuwa kali sana,kiasi kwamba wanaume walioathirika wanaweza hata kuharibu uume wao kwa kuhofia kuupoteza.
Kwa kushangaza, baadhi ya magonjwa haya sasa yametoweka, lakini pia kuna ambayo yanaonekana katika maeneo mpya ya dunia. Lakini magonjwa haya yalitoka wapi?
Swali hili halikuweza kujibiwa kwa miongo kadhaa, lakini sasa uvumbuzi mpya unaongeza uelewa kuhusu magonjwa ya akili.
Uzalishaji wa magharibi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Huu ni Ugonjwa wa kitamaduni unaoshangaza zaidi una historia ya kile wataalamu wanaita 'neurasthenia' nchini China yaani hali inayosababisha uchovu wa muda mrefu na hisia za uchovu au udhaifu baada ya kushughulisha mwili au akili kidogo tu, ambayo kwa kweli ni ugonjwa wa kikoloni wa karne ya 19.
Ugonjwa huo ulienezwa na daktari wa neva kutoka Marekani George Miller, ambaye aliamini kuwa ni uchovu katika mfumo wa neva.
Kevin Aho, wa Chuo Kikuu cha Florida Gulf Coast nchini Marekani, ambaye ametafiti juu ya historia ya ugonjwa huo, anasema ulipata umaarufu mkubwa ulipogunduliwa katika riwaya ya mwandishi maarufu Marcel Proust.
Neurasthenia polepole ilienea kwa makoloni ya Ulaya ulimwenguni kote, ambapo maofisa wa kwanza wa Ulaya na wake zao waliihusisha na umbali kutoka kwa nchi yao.
Kulingana na uchunguzi wa 1913, ugonjwa huo ulikuwa wa kawaida sana kati ya wenyeji wazungu wa India, Sri Lanka, China, na Japan.
Lakini basi hatua kwa hatua katika ulimwengu wa Magharibi ugonjwa huo ulihusishwa na matatizo makubwa zaidi ya kisaikolojia na sifa yake ilianza kupungua, mpaka ikasahaulika kabisa. Lakini katika maeneo mengine ilikuwa kinyume chake.
Katika baadhi ya maeneo ya Asia, watu bado wanaweza kusema wana neurasthenia badala ya sonona.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa mwaka wa 2018 nchini China, zaidi ya asilimia 15 ya watu walisema walikuwa na neurasthenia, wakati asilimia tano tu walitumia neno sonona.
Sababu za kitamaduni
Wazo mojawapo ni kwamba ubinadamu hukabiliwa na matatizo sawa ya kiakili, kama vile wasiwasi na mfadhaiko, lakini namna ya kuwasiliana inaweza kutofautiana kulingana na eneo na lugha.
Kwa mfano, katika enzi ya Victoria, mwanamke anayeomboleza kifo cha mume wake angesema kwamba alihisi udhaifu, lakini katika nyakati za kisasa, mwanamke huyo huyo angesema kwamba alikuwa anahisi sonona. Huko China, mwanamke anaweza kusema alikuwa na maumivu ya tumbo.
Mfano mwingine ni ulimwengu wa Kiislamu, ambapo imani ya kawaida ni kwamba majini wapo na wanaweza kuwa wema, waovu, na pia wanahusishwa na tabia za watu.

Chanzo cha picha, Alamy
Dhana hii ina nguvu sana miongoni mwa wagonjwa wangu wengi," anasema Prince Nawaz, daktari wa magonjwa ya akili katika Hospitali Kuu ya North Manchester nchini Uingereza.
Anaeleza kuwa dhana ya uwezo wa kuita mizimu imekuwepo katika utamaduni wa Kiislamu.
Utafiti wa wagonjwa 30 wa Bangladeshi mashariki mwa London uligundua kwamba ingawa watu hawa walikuwa na magonjwa kama vile 'schizophrenia' na ugonjwa wa 'bipolar', familia zao ziliamini kuwa walikuwa na majini.
Mateso ya kimwili na kisaikolojia
Dhiki pia hujipambanua kwa namna tofauti kote ulimwenguni.
Nchini Marekani, Uingereza na Ulaya, 'dhiki' ni jambo la fikra tu, na dalili kama vile huzuni, hasira na wasiwasi.
Lakini, katika maeneo mengi duniani kama vile China, Ethiopia na Chile, pia huathiri mwili.
Imethibitishwa kwa miaka mingi kwamba mawazo yetu yana ushawishi mkubwa juu ya hisia zetu na hata kwenye miili yetu.
Mfano mmoja wa hii ni 'kifo cha voodoo', ambacho hufahamika kama kifo cha ghafla kinachoweza kusababishwa na hisia za hofu.
Kisa kimoja maarufu kama hicho kilitokea huko New Zealand ambapo mwanamke wa eneo hilo alikula matunda kwa bahati mbaya kutoka mahali palitajwa kupigwa marufuku.
Alitangaza kwamba adhabu ya kosa hili itakuwa kifo, na mwanamke huyo alikufa siku iliyofuata.
Lakini je, kifo kinaweza kusababishwa na woga wa mtu binafsi kiasi hiki? Haiko wazi. Hata hivyo, kuna uthibitisho kwamba mawazo na hisia zetu zina matokeo katika mwili.
Ugonjwa wa ajabu unaoambukiza kwa njia ya hewa

Chanzo cha picha, Getty Images
Bonnie Kaiser, mtafiti wa masuala ya saikolojia ya binadamu katika Chuo Kikuu cha California, anasema kumekuwa na maambukizi yaliripotiwa ambapo maana yake inayotokana na uzoefu huo ilikuwa na athari kimwili.
Anatoa mfano wa 'Keol Goyo', ambayo ni ya kawaida miongoni mwa wakimbizi wa Cambodia nchini Marekani.Ilikuwa ya kushangaza.
Huko Cambodia, inaaminika kuwa kuna njia au vijia ndani ya mwili ambavyo kitu kama hewa hupita, na ikiwa hizi zimezuiwa, kiwango cha hewa hii mwilini kinaweza kuongezeka, na kusababisha mtu kupoteza kiungo au hata kufa.
Wakati wa utafiti katika kliniki ya magonjwa ya akili nchini Marekani, wagonjwa 100 walichunguzwa na 36 walidai kuwa na uzoefu kama huo.
Katika ugonjwa huu, kwanza afya inadhoofika,baadae mgonjwa huhisi kusinzia na huu ndio wakati anagundua kuwa ugonjwa huu unaanza.
Kisha kuna hali ambayo hawezi kuzungumza au kusogea.
Katika hali kama hiyo, ndugu au jamaa zake humkanda au kuuma vifundo vyake kwa meno yao.
"Watu wengi hupuuza wanapohisi kusinzia," asema Bonnie Kaiser. "Lakini ikiwa mtu anaichukulia kama dalili ya mwanzo wa ugonjwa wa celiac, wanafikiri kitu kibaya sana kitatokea.
Kisha wanakuwa na wasiwasi na hivyo ndivyo kila kitu kinabadilika."
"Kwa kweli, watu hutofautiana uzoefu wa magonjwa mengi ya akili, na uzoefu wao wa kitamaduni huamua jinsi wanavyokabiliana nayo," anasema.
Kuchunguza tena magonjwa kutoka Magharibi
Kutokana na kuongezeka kwa ujuzi kuhusu magonjwa ya kitamaduni, wanasaikolojia sasa wanahoji iwapo baadhi ya magonjwa ya akili yanayopatikana katika ulimwengu wa Magharibi pia yanaangukia katika kundi hili.
Baadhi ya magonjwa ni ya kawaida duniani kote, kama vile schizophrenia. Bulimia haijazoeleka sana katika tamaduni za Mashariki, wakati ugonjwa wa kabla ya hedhi haujafahamika nchini China, Hong Kong, na India.
Pia imejadiliwa, kwa utata, kwamba sonona ilielezewa zaidi na ulimwengu unaozungumza Kiingereza, ambao unaamini kwamba mtu anapaswa kuwa na furaha wakati wote.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa zama za kisasa, itakuwa ni makosa kufikiri kwamba magonjwa ya kisaikolojia au ya akili hayana umuhimu kwa maisha yetu ya kila siku.
Aho anasema kwamba hatuangalii magonjwa ya akili katika muktadha wa kijamii au kihistoria.
"Hakuna matibabu ya kulingana ambayo ni sawa kwa kila mtu," anasema. "Watu wenye imani maalum za kitamaduni, anasema, wanaweza kufaidika zaidi na tiba ya kisaikolojia."
Katika kitabu chake, 'Crazy Like This,' Ethan Waters anaandika kwamba katika miongo michache iliyopita, ugonjwa wa akili umeongezeka nchini Marekani hatua kwa hatua, na watu wameanza kuzoea changamoto za kihisia na kisaikolojia taratibu, kama vile huzuni au wasiwasi.
Anasema mchakato huu sio tu hatari kwa kutofanya uchunguzi sahihi na kutibu tatizo lakini pia kukosa fursa ya kubaini chanzo hasa cha maradhi ya kisaikolojia.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












