Kwa nini Iran haina haraka kuisaidia Hezbollah?

Chanzo cha picha, NurPhoto
Wiki iliyopita, Hezbollah nchini Lebanon imekumbwa na msururu wa mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa ambayo baadhi ya watu wanasema yamesababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kundi hilo katika miongo minne.
Kwanza, vifaa vya mawasiliano vya kikundi hilo – ‘pagers’ na ‘walkie-talkies’ - vilianza kulipuka nchini kote, na kuua kadhaa na kujeruhi mamia.
Kisha yakaja mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya shabaha za Hezbollah na mauaji ya makamanda wakuu.
Kwa maneno mengine, kundi hilo linakabiliwa na umwagaji damu mbaya zaidi tangu vita vya mwaka 2006 na Israel.
Hezbollah ni kundi kubwa zaidi la wanamgambo katika kile kinachojulikana kama "Axis of Resistance," muungano wa wanamgambo wa kikanda unaoichukia Israel.
Mara nyingi huitwa "jeshi lisilo la serikali lenye nguvu zaidi ulimwenguni."
Tangu kuanzishwa kwake, limefurahia uungwaji mkono kamili na usioyumba wa Iran.
Wengi walitarajia kwamba mashambulio yenye nguvu ya Israel, ambayo yamedhoofisha sana muundo wa Hezbollah, yangesababisha jibu la uamuzi zaidi kutoka kwa Iran. Lakini majibu kama hayo bado hayajafika.
Licha ya madai ya muda mrefu ya Iran kwamba Hezbollah ni "mstari mwekundu," na ukweli kwamba kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah hivi karibuni alisema kuwa Israel "ilivuka mistari yote myekundu," Iran haijaonyesha dalili yoyote ya jibu la kuzuia au la fujo.
Hata matamshi makali ya Wairani kuhusu kulipiza kisasi dhidi ya Israeli yanasikika kuwa yamezuiliwa wakati huu.
Maafisa wa Iran wanasemaje?

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wazo la msimamo wa Iran linaweza kupatikana kutokana na maoni ya hivi karibuni ya Rais wa nchi hiyo Masoud Pezeshkian, ambaye alihudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York.
Kwa mujibu wa rekodi ya sauti ya mkutano huo na waandishi wa habari wa Marekani, Pezeshkian alitoa kauli isiyo ya kawaida, akipendekeza kwamba Iran inaweza kufikiria kuacha kutumia nguvu za kijeshi ikiwa Israel itafanya vivyo hivyo.
Hii ni kinyume kabisa na msimamo wa Iran chini ya miezi miwili iliyopita, pale Iran ilipoapa kujibu vikali Israel kufuatia mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran.
Mabadiliko kuelekea sauti ya upatanishi zaidi huko New York yalikuwa ya kushangaza sana hivi kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alikuwa mwepesi kukanusha vikali ripoti kwamba Iran ilikuwa tayari kuvunja uhusiano wake na Israeli.
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Iran na Makamu wa Rais wa sasa Mohammad Javad Zarif alimuunga mkono Pezeshkian kwenye mitandao ya kijamii, akibainisha kwamba rais alilaani uhalifu wa Israel huku akiionyesha Iran kama mpigania amani na muungaji mkono wa kutokomeza silaha za nyuklia katika eneo hilo.
Zarif aliishutumu Israel kwa kuendeleza "masimulizi hatari na ya uwongo" kuhusu nia ya Iran, akimaanisha kuwa Iran, kinyume na madai ya Israel, haitafuti vita.
Pezeschkian mwenyewe, katika mazungumzo na waandishi wa habari wa Marekani, alisema kwa uwazi: "Hatutaki vita," akiishutumu Israel kwa kuweka mitego ya kuivuta Iran katika mzozo ambao, kulingana na yeye, hakutakuwa na washindi.
Je, Iran ilishtukizwa na shambulio la Israel?
Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi mkuu wa Iran, ambaye kijadi ana misimamo migumu zaidi kuhusu Israel na Marekani, aliitaja Lebanon kwa ufupi tu katika kujitokeza kwake hadharani mara ya mwisho siku tatu baada ya pager za Hezbollah kulipuka mbali na simu za upepo au walkie-talkie.
Badala yake, alitoa wito kwa mataifa ya Kiislamu kuungana katika kuipinga Israel na kukata uhusiano nayo kiuchumi na kisiasa.
Hali hii pia inaonekana katika vyombo vya habari vya Iran vinavyounga mkono serikali, ambavyo kijadi vinataka kulipiza kisasi dhidi ya Israel.
Baadhi ya sauti na vyanzo vikali sasa vinaangazia zaidi mawazo kama vile umoja wa Kiislamu katika uso wa Israeli - ingawa miito hii imeshindwa kuleta matokeo yaliyotarajiwa kwa miaka mingi.
Huku vyombo vingi vya habari vikiwa na vichwa vya habari vya uchokozi na picha za kutisha za makombora, sauti ya kulipa kisasi imetoweka, haswa baada ya mashambulio ya makombora ya Iran dhidi ya Israeli na mauaji ya kiongozi wa mrengo wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran.
Kwa mfano, gazeti la kihafidhina la Kayhan hivi majuzi lilichapisha tahariri chini ya kichwa cha habari dhidi ya Israeli “The Countdown Has Begun!” Hata hivyo, makala yenyewe inakiri kimyakimya kuhusu "ubora wa Israeli katika teknolojia na akili," ambayo inahusisha na msaada wa Magharibi, huku ikielezea Hezbollah kwamba inaungwa mkono na Iran, Palestina, Yemen, na makundi ya upinzani nchini Iraq pekee.
Sauti ya Kayhan inaweza kuashiria kwamba oparesheni tata kama vile ulipuaji wa mitambo ya mawasiliano ya Hezbollah, ambayo ilikuja kuwa utangulizi wa mashambulizi ya haraka na mabaya ya Israel, sio tu kwamba yaliifanya Hezbollah kuwa macho, lakini inaweza kuwa imeufanya uongozi wa Iran kurudi nyuma.
Mawazo haya yanaweza kufasiriwa kama kugeuza kisasi kilichoahidiwa. Lakini wengine wanapendekeza kwamba inaweza pia kuashiria kurudi nyuma kimkakati wakati Iran inapanga shambulizi la kushtukiza ili kulipiza kisasi.
Na ingawa hatua kama hizo huenda zisiwezekane kwa sasa , hatupaswi kusahau kwamba eneo la Mashariki ya Kati kwa muda mrefu limekuwa eneo ambalo matukio yasiyotabirika hutokea.
Imetafsiriwa na kuchapishwa na Seif Abdalla












