'Acha kufyatua risasi! Binti yangu amekufa'

    • Author, Shaimaa Khalil
    • Nafasi, BBC News Jerusalem
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Tahadhari: Taarifa ina maelezo ya kutamausha

Kabla tu ya Mwaka Mpya, Shatha al-Sabbagh mwenye umri wa miaka 21 alikuwa akienda kununulia chokoleti watoto wa familia yake kutoka duka moja huko Jenin, katika eneo la West Bank unaokumbwa vita vya mara kwa mara.

Mwanafunzi huyo wa taaluma ya uanahabari alikuwa ameanza kuonyesha ukakamavu wake, akiangazia mateso ya Wapalestina.

Binti huyo alikuwa ameandamana na mama yake, wapwa wawili wachanga na jamaa mwingine.

"Alikuwa akicheka na kusema tutakesha leo," anasema mama yake.

Mara ghafla akapigwa risasi kichwani.

Kwa Umm al-Motassem, mama wa Shatha, ana majonzi na unyonge wa kumpoteza binti yake.Anavuta pumzi ya uchungu.

"Macho ya Shatha yalikuwa wazi. Ilionekana kama alikuwa ananitazama alipokuwa amelala kwa mgongo huku damu zikimtiririka kutoka kichwani mwake.

"Nilianza kupiga kelele, 'Acha kufyatua risasi! Binti yangu ameuawa. Binti yangu ameuawa.'"

Lakini mashambulizi yaliendelea kwa takribani dakika 10.

Shatha alifariki akiwa amezungukwa na damu yake mwenyewe.

Familia ya Shatha inawashutumu kikamilifu majeshi ya Usalama ya Mamlaka ya Palestina (PA) kwa mauaji yake, wakisema eneo lao liko chini ya udhibiti wa PA.

"Haiwezi kuwa mtu mwingine isipokuwa PA… kwa sababu wana uwepo mkubwa sana katika mtaa wetu – hakuna mtu mwingine anaweza kuingia au kutoka," aliiambia BBC.

Lakini PA inalaumu "waasi" - neno wanalo tumia kumaanisha wanachama wa Kikosi cha Jenin, ambacho kinajumuisha wapiganaji kutoka vikundi vya silaha ikiwemo Jihad ya Kiislamu ya Palestina (PIJ) na Hamas.

PA ilianzisha operesheni ya kiusalama katika kambi hiyo ya Jenin mwezi jana ikilenga kundi lilojihami kwa silaha lililopo katika eneo hilo ambalo wanaliona kama tishio dhidi ya mamlaka yake.

Zaidi ya wiki nne sasa, operesheni hiyo inaendelea.

Kundi hilo la waasi linadaiwa kulipua gari na kutekeleza uhalifu na ''shughuli haramu.''

Kwa mujibu wa Brigadia Jenerali wa PA Anwar Rajab wamewapata na silaha na vilipuzi.

Akisema kuwa, ''Lengo letu ni kuondoa vilipuzi vilivyotegeshwa ardhini katika kambi hiyo na kundi hilo la waasi''.

Hata hivyo jenerali Rajab ameshutumu vikali Iran kwa kufadhili kundi hilo la waasi. Nao kundi hilo la Jenin limekanusha kusaidiwa na Iran.

Katika video iliyosambaa mitandaoni ,msemaji Nour al-Bitar amedai kuwa PA ilikuwa ikijaribu kuwaharibia sifa na kuwapaka matope akiongeza kuwa wapiganaji wake hatawasalimisha silaha kwao.

"Kwa mamlaka ya PA na rais Mahmoud Abbas tumefikiaje hapa?'' anauliza, akiwa ameshikilia kifaa ambacho anadai ni kilipuzi ambacho kilirushwa kambini humo na maafisa wa usalama.

PA, inayoongozwa na Rais Abbas, tayari ilikuwa haipendwi na Wapalestina wengi waliokasirishwa na kukataa kwake mapambano ya kijeshi na ushirikiano wake wa kiusalama na Israel.

Hasira hii iliongezeka baada ya PA kuanzisha operesheni kali dhidi ya vikundi vya silaha katika kambi hiyo, operesheni ambayo haijaridhisha wengi wakidai PA inawakandamiza.

Israel inavyoona vikundi hivyo kama magaidi, lakini wengi wa wakazi wa Jenin wanaviangalia kama njia ya kupinga utawala wa kikoloni.

"Hawa 'waasi' ambao PA inawaelezea – hawa ni vijana wanaosimama nasi wakati jeshi la Israel linavamia kambi yetu," anasema Umm al-Motassem.

Angalau watu 14 wameuawa katika operesheni hiyo, akiwemo mtoto wa miaka 14, kulingana na wizara ya afya ya Palestina.

Sasa wengi wa wakazi wa Jenin wanasema wanawahofu PA kama wanavyohofu mashambulizi ya kijeshi ya Israel.

Kifo cha Shatha al-Sabbagh kimeongeza tu chuki dhidi yao.

Kabla ya kuuawa, Shatha alichapisha machapisho kadhaa kwenye mitandao ya kijamii akionyesha uharibifu wa operesheni ya PA huko Jenin - pamoja na mashambulizi ya Israeli dhidi ya kambi hiyo mwaka jana.

Machapisho mengine yalionyesha picha za vijana wenye silaha waliouawa katika mapigano, akiwemo kaka yake.

Kifo chake kilikemewa na Hamas, ambapo kilimtaja kaka yake kama mwanachama aliyeuawa wa kikundi hicho, Brigedi za Izzedine al-Qassam.

Kikundi hicho kilielezea mauaji yake kama "mauaji… ya kikatili" kama sehemu ya "siasa za kinyanyaso dhidi ya kambi ya Jenin, ambayo imekuwa mfano wa msimamo na upinzani."

Mustafa Barghouti, kiongozi wa chama cha kisiasa cha Mpango wa Kitaifa wa Palestina, anaona mapigano huko Jenin kama matokeo ya mgawanyiko kati ya makundi makuu ya Wapalestina - Fatah, inayounda sehemu kubwa ya PA, na Hamas, ambayo imetawala Gaza tangu 2007.

"Kitu cha mwisho ambacho Wapalestina wanahitaji ni kuona Wapalestina wanapigana wenyewe wakati Israel inaangamiza kila mtu," anasema.

Ndani ya kambi, wakazi wanasema maisha ya kila siku na shughuli za kawaida zimesitishwa kabisa.

Umeme umekatwa na familia nyingi zinahangaishwa na njaa kutokana na uhaba wa chakula, hali ya baridi kali na mapigano ya risasi yasiyokwisha.

Wakazi waliokuwa wakizungumza nasi walitaka majina yao kubadilishwa, wakisema wanahofia kulipwa kisasi na PA.

"Mambo ni mabaya hapa. Hatuwezi kusafiri kwa uhuru kwenye kambi," anasema Mohamed.

"Maduka yote, mikahawa na maduka yamefungwa. Mgahawa ninaofanya kazi nao ufunguliwa kwa siku moja na kufungwa saa kumi. Wakati unafunguliwa, hakuna anayekuja kununua.

"Tunahitaji maziwa kwa watoto, tunahitaji mkate. Watu wengine hawawezi kufungua milango yao kwa sababu ya risasi zisizoisha."

Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu, OCHA, limesema linahitaji uchunguzi wa kile inachokielezea kama ukiukwaji wa haki za binadamu na vikosi vya PA.

Jenerali Rajab alisema baadhi ya "wahalifu" waliovamia kambi ya Jenin wamekamatwa na wengine wenye kesi za wazi watafikishwa mbele ya sheria.

Lakini Mohamed anaelezea operesheni ya PA - na watu wasio na hatia wanakutana na mashambulizi ya risasi - kama "adhabu ya pamoja."

"Ikiwa wanataka kuwashughulikia wahalifu, haitakiwi kuadhibu kambi nzima. Tunataka maisha yetu turudishiwe."

Hata kutoka nje kutafuta chakula au maji ni hatari, anasema Sadaf mwenye umri wa miaka 20.

"Unapotoka nyumbani, tunasema sala yetu ya mwisho. Tunajiandaa kiakili kwamba huenda tusirudi tena.

"Kuna baridi sana. Tumebomoa milango ya nyumba yetu kutumika kama kuni ili tuwashe moto wa kujipa joto."

BBC imesikia maelezo ya kufanana kutoka kwa wakazi wanne wa kambi.

Mazungumzo yangu na Sadaf yanavurugwa na sauti ya risasi. Haijulikani ni kutoka wapi wala nani anayepiga. Inaanza na kuisha mara kadhaa.

"Labda ni risasi za onyo," anapendekeza, akiongeza kuwa hii hutokea wakati vikosi vya PA vinabadilisha zamu.

Sadaf anaendelea kuelezea uhalisia wa mambo kambini, "taka zimejaa mitaani na karibu kuingia nyumbani." Inasikika tena sauti ya risasi.

Mama ya Sadaf anajiunga na mazungumzo. "Sikilizeni hili… Je, mtu anaweza kulala na hii sauti ikitokea?"

"Tunalala kwa zamu sasa. Tunaogopa sana kwamba watavamia nyumba zetu. Tunaogopa operesheni hii kama tunavyoogopa wakati askari wa Israeli wanatuvamia."

Watu wanasema vikosi vya usalama vimepiga na kuharibu kwa makusudi gridi za umeme na jenereta, na kuacha kambi hiyo gizani.

PA tena inalaumu "waasi" - na inasisitiza kuwa imeleta wafanyakazi kutengeneza gridi hiyo ya umeme.

Vikundi vya silaha vinataka "kutumia mateso ya watu kuishinikiza PA kuacha operesheni," anasema Jenerali Rajab.

Anasema operesheni ya kiusalama itaendelea hadi malengo yake yatimizwe.

Jenerali Rajab anasema lengo la PA ni kuanzisha udhibiti wa kambi ya Jenin na kuhakikisha usalama na utulivu.

Anaamini kuwa kuondoa udhibiti wa vikundi vya silaha kutasitisha kisingizio cha Israel kushambulia kambi hiyo.

Mwisho wa Agosti, jeshi la Israel lilifanya operesheni kubwa ya siku tisa ya "kupambana na ugaidi" katika mji wa Jenin na kambi hiyo, ambayo ilisababisha uharibifu mkubwa.

Angalau Wapalestina 36 walikufa - 21 kutoka mkoa wa Jenin - kulingana na wizara ya afya ya Palestina.

Wachambuzi wanasema PA inajaribu kurejesha mamlaka yake katika Ukingo wa Magharibi na kuonyesha kwa Marekani kwamba ina uwezo wa kuchukua jukumu katika utawala wa baadaye wa Gaza.

"Nini madhara ya hilo?" anasema Jenerali Rajab.

"Gaza ni sehemu ya taifa la Palestina. Gaza na West Bank si sehemu tofauti. Hakuna taifa la Palestina bila Gaza. Rais Mahmoud Abbas amesema hivyo na tutalifuata.''

Lakini "Marekani ,ambayo ni wandani wa karibu wa Israel inataka PA kuongoza Gaza baada ya vita .

Lakini Netanyahu ameonekana kuwa na maamuzi tofauti kuhusu uongozi wa PA unaopigiwa upatu na mataifa ya magharibi.

Kwa wakaazi wa kambi ya Jenin, hakuna kilichobadilika ni vita tu na hasara kwa wingi.

''PA inasema wako hapa kwa usalama wetu. Usalama uko wapi wakati binti yangu ameuawa kikatili? Usalama uko wapi na mchana kutwa ni milio ya risasi zisizoisha?'' Umm al-Motassem analia akiuliza maswali haya .

''Wanaweza kulenga waasi lakini kwanini binti yangu auawe katika pilkapilka hizo? Haki itapatikana hadi pale nitajua ni nani alikatiza maisha ya mwanangu.'' anasema.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid