Wakazi wanaokimbia vita Gaza wakabiliwa na baridi

    • Author, Yolande Knell
    • Nafasi, Middle East correspondent
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Pwani ya Gaza imeacha kuwa ni ya kubarizi na ziara za burudani.

Maelfu ya watu sasa wanapaita nyumbani baada ya kutoroka makwao wakati wa vita.

Siku za hivi karibuni mambo yamegeuka karaha:upepo wa bahari umekuwa ukipeperusha mahema ambayo wameyaezeka kando mwa bahari.

“Hakuna kilichobaki ndani ya mahema yetu,si magodoro,vyakula na malazi yamepeperushwa hadi baharini”anasema Mohammed al-Halabi anayeishi Deir al-Balah.

“Tuliokoa kitoto cha miezi miwili aliyekuwa amevutwa na upepo huo hadi baharini”.

Zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Gaza milioni 2.3 haina makazi na tisa kati ya kumi wanaishi kwenye mahema ,Umoja wa mataifa wasema.

Huku nyuzi za joto zikibadilika mara kwa mara ,watu wengi wanakabiliwa na maradhi.Kumekuwa na mafuriko na maji chafu kila mahali.

“Miguu ya watoto wangu ,vichwa vyao -vimeingiwa na baridi,”Shaima Issa anaiambia BBC akiwa Khan Younis.”Mwanangu ana joto jingi mwilini kutokana na baridi inayomuingia mwilini.Ni kama tunaishi barabarani tukifunikwa tu na kitambara.Kila mtu hapa ni mgonjwa na anakohoa.”

“Tukinyeshewa tunatota sana,”anaongezea jirani yake ,anayeitwa Salwa Abu Nimer ,akilia.

“Mvua nyingi inasababisha mafuriko,na hatuna cha kujizuia.Maji yanaingia kwa mahema ,na inatubidi tuvae nguo zikiwa baridi.”

“Hakuna unga,hakuna chakula,hakuna vinywaji,hakuna makazi,”anaendelea kueleza.

“Ni maisha gani haya ninayoishi?nahangaika mwisho wa dunia kutafutia wanangu cha kutia mdomoni.”

Huku hali ikizidi kuwa mbaya kaskazini,maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaibua wasiwasi wa upungufu wa dawa,vyakula,makazi na mafuta kote Gaza,wakielezea hali kuwa “mbaya zaidi.”

Kuna foleni kwa maeneo yanayotoa msaada katikati na kusini Gaza ambapo watu wengi wanaishi sasa.

Kwa siku za kawaida,mpiga picha wetu amenasa mamia ya watu wakifurika nje ya maduka ya kuoka mikate na bidhaa hiyo imekuwa adimu sana.

Na kuna wakati kuna mkanyagano waking’ang’ania kidogo kilichobakia.

“Nataka mkate.Nina maumivu,kisukari na shinikizo la dami.Siwezani na mvutano katika foleni;naogopa naweza ishiwa na pumzi nife,”anasema Hanan al-Shamali,ambaye ni mkaazi wa Deir al-Balah lakini amelelewa kaskazini mwa Gaza.

“Ninahitaji mikate ili nikawalishe mayatima ambao naishi nao.Kila asubuhi huja hapa.Mwisho wa siku napata mkate na pia mara nyingi wakati mwingi nakosa mkate.”

Katika kivukio cha Kerem Shalom ,eneo kuu la kuvuka kutoka Israel hadi Gaza,wiki jana wanahabari walionyeshwa malori ambayo yalikuwa yamebeba bidha tofauti baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Misaada inayoingia katika kambi ya Palestina imebaki kuwa kidogo sana ukilinganisha na mwaka jana.

Israel inalaumu mashirika yakutoa misaada kwa changamoto za usambazaji.

“cha kutamausha bado tunaona kuchelewa kwa misaada inayopaswa kusambazwa kama unavyoona malori 800 yamenizunguka.”anasema Shimon Freedman,msemaji wa Cogat ,sehemu ya jeshi la Israel ambalo ulinda kivukio hicho.

Lakini nchini Gaza,wafanyikazi wa haki za binadamu wanasema magenge yamekuwa yakivamia malori ya misaada yanatoka katika kivukio hicho kutokana na ulegevu wa usalama.

Hili limepelekea shirika kubwa zaidi la UN kusitisha kutumia njia hiyo kusambaza misaada yao.

Kwa picha kamili,anasema Antoine Renard,kiongozi wa programu ya chakula ulimwenguni chini ya UN,Palestina wanakabiliwa na “dhiki ya kuishi”.

Viwango vya njaa ,kukatika tamaa na uharibifu tunaouona sasa nchini Gaza ni hali mbaya zaidi ikilinganishwa na hapo awali.

Watu wameanza kukata tamaa ,”Bwana Renard anasema.

“Hakuna chakula cha kutosha kinachoingia na sokoni hakuna cha mno.”

Uharibifu unaoendelea Gaza ,unaonekana kiza kisichokuwa na mwangaza hivi karibuni huku vita vikiendelea.

Raia wa Gaza wanachotarajia ni dhiki,huku baridi ikiendelea kuwapiga wakijaribu kuhepa makombora yanayorushwa bila mpangilio.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid