Jinsi China inavyojaribu kuvunja ngome ya visiwa vya Marekani

Muda wa kusoma: Dakika 5

Mkutano wa kila mwaka wa Shangri-La uliofanyika Singapore mwishoni mwa juma ni muhimu sana kwa kuchunguza misimamo ya kiusalama ya Marekani na China katika ukanda wa Asia-Pasifiki. Hata hivyo, mwaka huu China haikutuma waziri wake wa ulinzi wala wajumbe wa ngazi ya juu. Hata kikao kilichoandaliwa na China kilifutwa.

Moja ya kauli zilizozua utata mkubwa ilitolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pat Hegseth, ambaye aliionya kuwa China inalenga "kuvamia" Taiwan na "kubadilisha kwa nguvu mlingano wa nguvu katika Bahari ya Kusini ya China na msururu wa Kwanza wa Visiwa.''

China imeendelea kuongeza uwepo wake wa kijeshi baharini kwa kasi. Mwezi uliopita, ilituma idadi kubwa ya ndege za kivita na meli za kivita ambayo haijawahi kushuhudiwa katika njia zote za baharini, hali inayoonekana kama changamoto ya moja kwa moja kwa uwepo wa kijeshi wa Marekani katika msururu wa Kwanza wa Visiwa.

Ukuaji wa ushawishi wa kijeshi wa China, ukiwemo ule wa shughuli zake katika Bahari ya Tasman na uhusiano wake wa karibu na mataifa ya visiwa vya Pasifiki, kunaweza pia kutishia ushawishi wa Marekani katika Msururu wa Pili wa Visiwa.

Makala hii inaangazia jinsi China inavyovunja Msururu wa Kwanza na wa Pili wa Visiwa kupitia upanuzi wa nguvu za kijeshi na diplomasia.

Misururu hii ni sehemu ya mkakati wa Marekani wa kuizuia China na kuikwamisha kueneza nguvu zake nje ya maeneo hayo. Msururu wa Kwanza wa Visiwa unapita kutoka visiwa vikuu vya Japani, kupitia Visiwa vya Ryukyu, Taiwan, Ufilipino, na kuishia katika pwani ya Vietnam.

Msururu wa Pili uko mashariki zaidi na unajumuisha Visiwa vya Bonin vya Japani, Visiwa vya Mariana ya Kaskazini, Guam, Palau, na sehemu ya magharibi ya New Guinea.

Unaweza pia kusoma:

Ongezeko la shinikizo katika msururu wa visiwa vya kwanza

Vyombo vya habari vya Taiwan vinaripoti kwamba China imepeleka nguvu kubwa za kijeshi katika Bahari ya Njano iliyopo Katikati mwa China na rasi ya Korea, Bahari ya Mashariki na Kusini ya China, pamoja na njia ya baharini ya Taiwan.

Meli zake mbili za ndege za kivita—Shandong zilizopo katika Bahari ya Kusini ya China na Liaoning karibu na Taiwan—zinaashiria ongezeko kubwa la mzozo.

Mwezi Mei peke yake, China ilirusha zaidi ya ndege 70 za kivita katika eneo la ulinzi wa anga la Taiwan kwa siku kadhaa na kufanya mazoezi karibu nae neo la Fujian atika kumbukumbu ya kuapishwa kwa Rais wa Taiwan, William Lai.

Kundi la meli za China kutoka kwa mashariki mwa maeneo makuu matano ya kijeshi ya Jeshi la Watu la China (PLA) lilivuka Bahari ya Pasifiki Magharibi kupitia njia ya bharini ya Miyako.

Wakati huo huo, meli ya ndege ya Liaoning ilifanya mazoezi yake ya kwanza ya kuchukua ndege na kutua katika Bahari ya Mashariki ya China mwishoni mwa mwezi Mei.

Mvutano pia uliibuka katika Bahari ya Njano, ambapo China ilianza ujenzi karibu na Kisiwa kinachogombaniwa cha Suwan. Miundo inayotarajiwa kukamilika mwaka 2025 itasaidia helikopta kutua na kuruka, pamoja na kuweka mifumo ya rada na sonari chini ya maji kwa ajili ya shughuli za kijeshi.

China pia imepeleka mabomu ya aina ya H-6 kwenye Kisiwa cha Woody katika Visiwa vya Paracel, jambo ambalo limepunguza muda wa majibu ya kijeshi.

Wachambuzi na waandishi wa habari nchini China wanaona kuwekwa kwa nguvu hizi kama "mafanikio ya kimkakati" dhidi ya udhibiti wa Marekani katika Msururu wa Visiwa wa Kwanza.

Je China imenufaika zaidi?

Katika hatua ya kihistoria, Kwa mara ya kwanza China ilituma meli zake zote mbili za ndege kufanya mazoezi nje —siku ambayo pia Marekani ilituma meli zake za ndege Nimitz na George Washington katika Bahari ya Kusini ya China na Pasifiki Magharibi.

Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wa China wanasema meli hizo za ndege zina jaribu kuzuia msaada wowote wa Marekani au ushirikiano kati ya Japan na Ufilipino.

Waandishi wa Habari wanahoji kuwa Marekani iko katika nafasi dhaifu kwa sababu Nimitz inakaribia kustaafu na George Washington ilikuwa imetoka tu kufanyiwa ukarabati.

Pia wanahoji kama Marekani inaweza kukabiliana na meli tatu za ndege za China kwa wakati mmoja hasa meli ya ndege ya Fujian inayokaribia kuanza huduma zake baada ya majaribio yake ya nane baharini

Li Rongmao, mchambuzi wa masuala ya China, anasema uhamishaji wa vikosi vya wanajeshi 9,000 kutoka Okinawa kwenda Guam na Hawaii, pamoja na wanajeshi wengine 4,500 kutoka Korea Kusini kwenda Guam, unaashiria "kuondoka kimkakati." Maeneo haya sasa yako ndani ya urefu wa makombora ya hypersonic ya China ya DF-17.

Hata hivyo, Japan iliripoti kwamba meli za kivita za China, Liaoning, zilivuka mara ya kwanza katika eneo la kipekee la kiuchumi la Kisiwa cha Minamitori, na kupelekea kwa kuvunja Msururu wa Pili wa Visiwa.

Siku moja baadaye, meli za Shandong zilionekana zikifanya operesheni kilomita 550 kusini-mashariki mwa Kisiwa cha Miyako. Hii ilikuwa operesheni ya kwanza ya pamoja ya meli zote mbili za ndege za China katika Bahari ya Pasifiki Magharibi.

Picha za ndege mbili za kivita za kizazi cha sita za China—Chengdu J-36 na Shenyang J-50—pia zimeonekana. Wachambuzi wanaamini kwamba aina hizi mpya, zenye uwezo wa kufika umbali wa kilomita 3,000, zimetengenezwa kwa ajili ya kutumika kwenye meli za kubebea ndege.

Mwezi Februari, jeshi la majini la China lilifanya mazoezi yake ya kijeshi kwa mara ya kwanza kabisa katika Bahari ya Tasman upande wa Kusini mwa Pasifiki, mashariki mwa Sydney.

Hatua hiyo iliitia hofu Australia na New Zealand, hasa wakati ambapo Australia ilikuwa katika juhudi za kurejesha udhibiti wa Bandari ya Darwin, iliyokodishwa kwa miaka 99 kwa kampuni ya Landbridge ya China.

Uhusiano unaozidi kuimarika wa kidiplomasia wa China pia unazua wasiwasi. Mnamo mwaka 2023, Visiwa vya Solomon vilisaini mkataba wa usalama na Beijing unaoruhusu polisi wa China kuwafundisha maafisa wa usalama wa ndani.

New Zealand ilipinga mkataba kama huo kati ya China na Visiwa vya Cook mapema mwaka 2024.

Baadhi ya mataifa ya Pasifiki pia yamekatisha uhusiano na Taiwan na kuhamia upande wa Beijing, yakiwemo Visiwa vya Solomon, Kiribati (2019), na Nauru (2024). Washirika wa pekee wa Taiwan waliobaki katika eneo la Pasifiki ni Visiwa vya Marshall, Palau, na Tuvalu—ambapo mawili kati yao yana mikataba ya ulinzi na Marekani.

Palau, inayochukuliwa kuwa muhimu kwa Mnyororo wa Pili wa Visiwa, inaripotiwa kuwa chini ya shinikizo la kiuchumi kutoka Beijing ili iachane na Taipei.

Mwezi Mei, China iliandaa mkutano wake wa tatu na viongozi wa visiwa vya Pasifiki huko Xiamen. Ingawa hakuna makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa, China iliahidi msaada unaohusiana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi wa dola milioni 2 na kujadili ushirikiano wa kibiashara na wa baharini.

Profesa Yu Li anasema kwamba kadri Beijing inavyojenga miundombinu na kutoa mikataba ya biashara, nguvu za China za kijeshi na za ushawishi zitaendelea kukua katika eneo la Pasifiki.