Marekani inaihami vikali Taiwan kimya kimya

Na Rupert Wingfield-Hayes

BBC News, Taiwan

Wakati Rais wa Marekani Joe Biden alipotia saini hivi majuzi kutoa ruzuku ya $80m kwa Taiwan kwa ajili ya ununuzi wa zana za kijeshi za Marekani, China ilisema "inachukizwa na kupinga" kile Washington ilichokifanya.

Kwa mtazamaji wa kawaida haikuonekana kama kiasi kikubwa. Ilikuwa chini ya gharama ya ndege moja ya kisasa ya kivita. Taiwan tayari ina oda ya zaidi ya $14bn ya vifaa vya kijeshi vya Marekani. Je, msaada wa $80m ni muhimu zaidi?

Ingawa hasira ni jibu la msingi la Beijing kwa usaidizi wowote wa kijeshi kwa Taiwan, wakati huu kuna kitu tofauti.

$80m sio mkopo. Inatoka kwa walipa kodi wa Marekani. Kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 40, Marekani inatumia pesa zake yenyewe kutuma silaha mahali ambapo haitambuliwi rasmi. Haya yanajiri chini ya mpango unaoitwa fedha za kijeshi za kigeni (FMF).

Tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka jana, FMF imekuwa ikitumika kutuma takriban $4bn za msaada wa kijeshi kwa Kyiv. Imetumika kupeleka mabilioni mengine Afghanistan, Iraq, Israel na Misri na kadhalika. Lakini mpaka sasa imewahi kutolewa tu kwa nchi au mashirika yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa. Taiwan sio miongoni mwa nchi hizo .

Baada ya Marekani kubadili utambuzi wa kidiplomasia kutoka Taiwan hadi China mwaka 1979, iliendelea kuuza silaha kisiwani humo chini ya masharti ya Sheria ya Mahusiano ya Taiwan. Jambo kuu lilikuwa ni kuuza silaha za kutosha ili Taiwan iweze kujilinda dhidi ya shambulio linalowezekana la Wachina, lakini sio nyingi sana hivi kwamba zinaweza kuvuruga uhusiano kati ya Washington na Beijing. Kwa miongo kadhaa, Marekani imekuwa ikitegemea hili linaloitwa uhusiano wenye utata wa kimkakati kufanya biashara na China, huku ikibaki kuwa mshirika mkuu wa Taiwan.

Lakini katika muongo uliopita usawa wa kijeshi katika Mlango-Bahari wa Taiwan umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika upande wa China.Mbinu ya zamani haifanyi kazi tena. Washington inasisitiza sera yake haijabadilika lakini, kwa njia muhimu, imebadilika. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imekuwa uepesi wa kukanusha FMF inadokeza utambuzi wowote wa Taiwan. Lakini huko Taipei ni dhahiri kwamba Marekani inafafanua upya uhusiano wake na kisiwa hicho, hasa kwa kuzingatia kasi ambayo Washington inaisukuma Taiwan kwa kuipa silaha tena. Na Taiwan, ambayo imezidiwa na Uchina, inahitaji msaada huo.

"Marekani inasisitiza haja kubwa ya kuboresha uwezo wetu wa kijeshi. Inatuma ujumbe wa wazi wa uwazi wa kimkakati kwa Beijing kwamba tusimame pamoja," anasema Wang Ting-yu, mbunge wa chama tawala mwenye uhusiano wa karibu na Rais Tsai Ing- wa Taiwan- wen, na kwa wakuu wa bunge la Marekani.

Anasema $80m ni ncha ya kile kinachoweza kuwa jiwe kubwa la barafu, na anabainisha kuwa mnamo Julai Rais Biden alitumia mamlaka yake kuidhinisha uuzaji wa huduma za kijeshi na vifaa vya thamani ya $500m kwa Taiwan. Bw Wang anasema Taiwan inajiandaa kutuma vikosi viwili vya wanajeshi wa nchi kavu Marekani kwa ajili ya mafunzo, ikiwa ni mara ya kwanza hii kutokea tangu miaka ya 1970.

Lakini muhimu ni pesa,mwanzo anaosema unaweza kuwa msaada wa hadi $ 10bn katika miaka mitano ijayo.

Mikataba inayohusisha zana za kijeshi inaweza kuchukua hadi miaka 10, anasema I-Chung Lai, rais wa Wakfu wa Prospect, taasisi yenye makao yake makuu Taipei. "Lakini kwa FMF, Marekani inatuma silaha moja kwa moja kutoka kwenye hifadhi yake na ni pesa za Marekani - kwa hivyo hatuhitaji kupitia mchakato mzima wa kuidhinisha."

Hii ni muhimu kutokana na kwamba Bunge lililogawanyika limeshikilia msaada wa mabilioni ya dola kwa Ukraine , ingawa Taiwan inaonekana kuwa na uungwaji mkono zaidi wa pande mbili. Lakini vita vya Gaza bila shaka vitapunguza usambazaji wa silaha za Marekani hadi Taipei, kama vile vita vya Ukraine. Rais Biden anatafuta msaada wa vita kwa Ukraine na Israel, ambayo inajumuisha pesa zaidi kwa Taiwan pia.

Uliza Wizara ya Ulinzi ya Kitaifa huko Taipei pesa za Marekani zitatumika kwa ajili gani, na jibu ni tabasamu la kujua na midomo iliyofungwa vizuri.

Lakini Dk Lai anasema inawezekana kukisia kwa ufahamu: Makombora ya Javelin na ya Stinger - silaha zenye ufanisi mkubwa ambazo vikosi vinaweza kujifunza kutumia haraka.

"Hatuna vya kutosha, na tunahitaji mengi," anasema. "Nchini Ukraine, Stinger zimeisha haraka sana, na jinsi Ukraine imekuwa ikizitumia inaonyesha kuwa tunahitaji labda mara 10 ya idadi tuliyo nayo sasa."

Tathmini ya waangalizi wa muda mrefu ni butu: kisiwa hicho hakijatayarishwa kwa ajili ya mashambulizi ya Wachina.

Orodha ya matatizo ni ndefu. Jeshi la Taiwan lina mamia ya vifaru vya vita vya zamani, lakini mifumo michache ya kisasa ya makombora mepesi. Muundo wa kamandi ya jeshi lake, mbinu na mafundisho yake hayajasasishwa kwa nusu karne. Vitengo vingi vya mstari wa mbele vina 60% tu ya wafanyikazi wanaopaswa kuwa nao. Operesheni za kukabiliana na ujasusi za Taiwan nchini China zinaripotiwa kuwa hazipo na mfumo wake wa kujiandikisha kijeshi umevunjwa.

Mwaka 2013 Taiwan ilipunguza utumishi wa kijeshi kutoka mwaka mmoja hadi miezi minne tu, kabla ya kuirejesha hadi miezi 12, hatua ambayo itaanza kutumika mwaka ujao. Lakini kuna changamoto kubwa zaidi. Inajulikana kwa utani kama "kambi ya majira ya joto" na vijana wanaopitia.

"Hakukuwa na mafunzo ya kawaida," anasema mhitimu wa hivi majuzi. "Tulikuwa tukienda kwenye safu ya kulenga risasi mara moja kila baada ya wiki mbili, na tulitumia bunduki za zamani za miaka ya 1970. Hatukulnga shabaha. Lakini hakukuwa na mafundisho sahihi ya jinsi ya kulenga shabaha, kwa hivyo kila mtu aliendelea kukosa kulenga shabaha kwa njia sahihi . Hatukufanya mazoezi yoyot. Kuna mtihani wa wa kutathmini uthabiti wa mwili mwishoni, lakini hatukujitayarisha."

Alielezea mfumo ambao makamanda wakuu wa jeshi huwaona vijana hao kwa kutojali kabisa na hawana nia yoyote ya kuwafundisha, kwa sababu watakuwa hapo kwa muda mfupi.

Mjini Washington kuna hisia kali kwamba Taiwan inakosa wakati wa kufanya mageuzi na kujenga upya jeshi lake. Kwa hivyo, Marekani pia inaanza kufundisha tena jeshi la Taiwan.

Kwa miongo kadhaa, viongozi wa kisiasa na kijeshi wa kisiwa hicho wameegemea sana kwenye imani kwamba kuvamia kisiwa hicho ni kibarua kigumu sana na ni hatari kwa Uchina kujaribu. Badala yake kama Uingereza, Taiwan ilitanguliza jeshi lake la wanamaji na anga - kwa gharama ya jeshi lake.

"Wazo lilikuwa wakiisakama China katika Mlango-Bahari wa Taiwan na kuwaangamiza kwenye fukwe. Kwa hiyo, tunaweka rasilimali nyingi katika ulinzi wa anga na bahari," anasema Dk Lai.

Lakini sasa China ina jeshi kubwa zaidi la wanamaji duniani na jeshi la anga la juu zaidi. Zoezi la michezo ya kivita lililoendeshwa na taasisi ya mikakati mwaka jana liligundua kuwa katika mzozo na China, jeshi la wanamaji la Taiwan na jeshi la anga litaangamizwa katika saa 96 za kwanza za vita.

Chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa Washington, Taipei inabadili mkakati wa "ngome ya Taiwan" ambayo ingefanya kisiwa hicho kuwa kigumu sana kwa China kukiteka.

Mtazamo huo utabadilika kuwa askari wa ardhini, askari wa miguu na mizinga - kuzuia uvamizi kwenye fukwe na, ikiwa ni lazima, kupigana na Jeshi la Ukombozi la Watuwa China (PLA) katika miji baada ya mingine na kutoka kwenye misingi iliyo ndani ya milima ya kisiwa iliyofunikwa na misitu. Lakini hii inarudisha jukumu la kuilinda Taiwan kwenye jeshi lake lililopitwa na wakati.

"Baada ya Marekani kukata mahusiano mwaka 1979, jeshi letu lilikabiliwa na kutengwa kabisa. Kwa hiyo wamekwama katika zama za Vita vya Vietnam vya mafundisho ya kijeshi ya Marekani," Dk Lai anasema.

Hili halikusumbua Taipei au Washington hadi hivi majuzi zaidi. Kupitia miaka ya 1990 na 2000 makampuni ya Taiwan na Marekani yalikuwa yakijenga viwanda kote China. Beijing ilikuwa ikishawishi kujiunga na Shirika la Biashara Ulimwenguni - na ilifanya hivyo. Ulimwengu ulikumbatia uchumi wa China, na Marekani ilifikiri biashara na uwekezaji zingelinda amani katika Mlango-Bahari wa Taiwan.

Lakini kuongezeka kwa ushawishi wa Xi Jinping, na chapa yake ya utaifa, na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kumesambaratisha mawazo hayo ya kufariji.

Kwa Taiwan somo kutoka kwa uvamizi wa Ukraine limekuwa la kushangaza. Silaha imetawala uwanja wa vita - ina kiwango cha juu cha moto na sahihi ni tisho bora la kuzuia uvamizi. Wafanyakazi wa Ukraine wamejifunza lazima wawe wanasafiri mara tu watakapofyatua makombora mengi - au ndani ya dakika chache,.

Lakini wanajeshi wengi wa Taiwan wana silaha za Vita vya Vietnam au hata bunduki za zama za Vita vya pili vya dunia .Hizi hupakiwa kwa mikono na ni ngumu na zinachukua muda kusongeshwa.

Udhaifu wa Taiwan unalazimisha Washington kuchukua hatua. Ndio maana wanajeshi wa nchi kavu wa Taiwan wanatumwa Marekani kupewa mafunzo na wakufunzi wa Marekani wanakuja Taipei kuungana na wanamaji wa Taiwan na vikosi maalum.

Lakini William Chung, mtafiti mwenzake katika Taasisi ya Utafiti wa Ulinzi na Usalama wa Kitaifa huko Taipei, anasema Taiwan bado haiwezi kutumaini kuizuia China yenyewe. Hili ni somo lingine kutoka kwa vita vya Ukraine.

"Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuamua kama Taiwan ni muhimu," anasema. "Ikiwa G7 au Nato wanadhani Taiwan ni muhimu kwa maslahi yao wenyewe, basi tunapaswa kuifanya hali ya Taiwan kuwa ya kimataifa - kwa sababu hiyo ndiyo itaifanya China kufikiria mara mbili kuhusu gharama."

Dk Chung anasema tabia ya China, bila kujua, imekuwa ikiisaidia Taiwan kufanya hivyo.

"China inaonyesha kuwa ina upanuzi katika Bahari ya Kusini ya China na Bahari ya Mashariki ya China," anasema. "Na tunaweza kuona matokeo nchini Japan ambapo bajeti ya kijeshi sasa inaongezwa maradufu ."

Matokeo yake, anasema, yanaunda upya ushirikiano katika eneo hilo - iwe ni mkutano wa kihistoria kati ya Marekani, Japan na Korea Kusini , umuhimu unaoongezeka wa ushirikiano wa kijeshi kama vile Quad (Japan, Marekani, Australia na India) na Aukus (Uingereza, Marekani na Australia) ambazo zinakimbia kujenga manowari zinazotumia nyuklia za kizazi kijacho, au uhusiano wa karibu kati ya Marekani na Ufilipino .

"China inajaribu kubadilisha hali ilivyo katika kanda," anasema. "[Na hiyo] inamaanisha usalama wa Taiwan umeunganishwa na Bahari ya Uchina Kusini na Bahari ya Uchina Mashariki. Inamaanisha kuwa hatujatengwa tena."

Sasa kuna mjadala mkali huko Washington kuhusu jinsi Marekani inapaswa kwenda katika kuiunga mkono Taiwan. Watazamaji wengi wa muda mrefu wa Uchina wanasema ahadi yoyote ya umma kutoka kwa Amerika ilisema ingechochea Beijing badala ya kuizuia. Lakini Washington pia inajua kwamba Taiwan haiwezi kutumaini kujilinda peke yake.

Kama mtazamaji mmoja wa muda mrefu wa China alivyosema: "Tunahitaji kunyamaza juu ya suala zima la utata wa kimkakati, huku tukiipa silaha Taiwan kwa meno."