Kwa nini baadhi ya Wakorea Kaskazini wanataka kupigana na Urusi nchini Ukraine?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Kundi la waasi wa Korea Kaskazini walioko Korea Kusini wanatetea misheni ya uthubutu na ambayo haijawahi kushuhudiwa: kusafiri hadi mstari wa mbele nchini Ukraine na kuwasaidia wanajeshi wa Korea Kaskazini waliotumwa huko.

Wanasema ujuzi wao wa kipekee wa fikra na muundo wa jeshi la Korea Kaskazini unawawezesha vya kutosha kuwashawishi wanajeshi kuasi, ambao wanasema wamefunzwa kuona vifo vyao kuwa "vitukufu."

Hatua ya Korea Kaskazini kupeleka wanajeshi 10,000 nchini Urusi kwa ajili ya kupigana nchini Ukraine imeibua wasiwasi miongoni mwa waasi nchini Korea Kusini.

Idara ya ujasusi ya Korea Kusini inakadiria kuwa kila mwanajeshi aliyetumwa anaweza kupata dola 2,000 kwa mwezi, jambo ambalo litakuwa suluhu kwa Pyongyang.

Wakati wanajeshi wa Korea Kaskazini walipotumwa katika Vita vya Vietnam katika miaka ya 1970, ushiriki wao nchini Ukraine ungekuwa wa kwanza wa aina yake katika vita vya kisasa.

Korea Kaskazini na Korea Kusini zimekuwa vitani tangu kumalizika kwa Vita vya Korea (vilivyodumu kutoka 1950 hadi 1953), vikisaidiwa na China na Marekani mara zote, na kusalia katika uhusiano wa mvutano.

Takriban raia 34,000 wa Korea Kaskazini wamehamia Kusini tangu kugawanywa kwa Peninsula ya Korea zaidi ya miaka 70 iliyopita.

Wito wa kuchukua hatua

Makundi mawili ya kiraia yakiongozwa na waasi wa Korea Kaskazini - Chama cha Wanajeshi wa Kikristo wa Korea Kaskazini na Jeshi la Waasi la Korea Kaskazini - walitoa taarifa ya pamoja kulaani "tabia isiyo na utu" ya serikali ya Korea Kaskazini na kuwataka walioasi kuruhusiwa kusafiri hadi Ukraine.

"Tunalaani vikali tabia ya kikatili ya utawala wa Kim Jong Un ambayo inawapeleka Watoto wa watu kama chakula cha mizinga ili kuhakikisha ufadhili wa utawala wake na kufanya vifaa vyake vya vita kuwa vya kisasa," walisema.

Sim Ju-il, afisa wa zamani na kiongozi wa Jumuiya ya Wanajeshi wa Kikristo wa Korea Kaskazini, alisema misheni hiyo ni ya dharura.

"Wanajeshi wa Korea Kaskazini waliopelekwa Korea Kaskazini wanaweza kupigana chini ya mafunzo potofu waliyopewa na malezi yao huko Korea Kaskazini, wakiamini kwamba 'kifo chao ni cha utukufu.' Lazima tuwaeleweshe [kwamba sivyo]," alisema.

"Ikiwa nitasonga mbele, labda nitakabiliana na bunduki na risasi za wanajeshi wa Korea Kaskazini. Lakini nitajaribu kuwaelewesha uhalisia wa vita," aliongeza.

Mikakati

Waasi wamependekeza mbinu mbalimbali za kuwafikia wanajeshi wa Korea Kaskazini waliopelekwa, kwa kutumia vita vya kisaikolojia kupitia vipeperushi vya kudondoshwa kwa ndege zisizo na rubani, matangazo ya megaphone na kampeni za mitandao ya kijamii.

"Tutatumia ndege zisizo na rubani kueneza vipeperushi [nyenzo za propaganda] na majukwaa ya mitandao ya kijamii kama YouTube.

Ikiwa tunaweza kukaribia mstari wa mbele, tunaweza kutumia megaphone kuendesha vita vya kisaikolojia," alisema Dk Ahn Chan-il, mkurugenzi wa Taasisi ya Dunia ya Mafunzo ya Korea Kaskazini na mkuu wa Jeshi la Waasi la Korea Kaskazini.

Dk. Ahn, ambaye alihudumu katika kikosi cha ulinzi wa raia nchini Korea Kaskazini, ana wasiwasi hasa kuhusu uwezekano wa kuhusika kwa kikosi maalum cha Korea Kaskazini, kikiwemo kikosi cha Storm Corps - kitengo kilichopewa mafunzo ya uvamizi,hujuma za miundombinu na mauaji - katika vita vya Ukraine.

"Iwapo vitengo viwili au vitatu vya jeshi la Korea Kaskazini vitatumwa [Urusi], bila shaka kazi yetu itakuwa imepungua.Hiyo ndiyo sababu ya kauli hii," alisema.

Ripoti zinaonyesha kuwa hivi karibuni baadhi ya waasi wameunda shirika linalolenga kuwahimiza wanajeshi wa Korea Kaskazini waliopelekwa nchini Ukraine kuasi.

Mbinu yao inahusisha kusambaza vipeperushi na taarifa kwa mfumo wa sauti kwa vikosi vya Ukraine vinavyotoa ushauri wa namna ya kujiepusha kuwa mstari wa mbele.

Changamoto

Vikwazo vya kiutendaji na vya kidiplomasia vinakwamisha mipango hii.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini imeiwekea Ukraine marufuku ya kusafiri, huku ukiukaji ukiwa na adhabu ya kifungo cha hadi mwaka mmoja gerezani au faini ya hadi dola 7,000.

Pia kuna wasiwasi kwamba kutuma waasi nchini Ukraine kunaweza kuzichokoza Pyongyang na Moscow, na hivyo kuyumbisha usalama wa kikanda.

"Ni vizuri kusema, 'Tutakwenda kupigana,' lakini kutuma wanajeshi ni suala muhimu katika masuala ya uhusiano wa kidiplomasia," alisema Lee Min-bok, mkuu wa Baloon group, kundi jingine la Korea Kaskazini lililoasi.

Wengine wanashangaa kama wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaweza kushawishiwa kuasi.

Lee Woong-gil, afisa wa zamani wa kundi la wanausalama kitengo cha uvamiaji Korea Kaskazini, alionya kwamba majaribio kama hayo yanaweza kuleta matokeo mabaya: "Ukijaribu kuwashawishi wafanye makosa, watakupiga risasi kichwani," alisema.

Pia anabainisha kuwa baadhi ya waasi, ambao wameishi Korea Kusini kwa miaka mingi, hawana ujuzi wa kisasa wa mienendo ya ndani ya jeshi la Korea Kaskazini.

Bwana Sim, kutoka Jumuiya ya Wanajeshi wa Kikristo wa Korea Kaskazini, anakiri kwamba ni vigumu kukiuka nidhamu na uaminifu uliokita mizizi kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini.

Kim Jong Un anataka watu waseme, "Jeshi la Korea Kaskazini halina mzaha" wakati vitengo vyake vinapotoka [kwenye uwanja wa vita] na kupigana vyema.

"Je, wanajeshi wa Korea Kaskazini wangekuwa wamejiandaa siku moja au mbili kabla [pekee]? Lazima wangepanga na Urusi na kutoa mafunzo ipasavyo," anasema.

"Wanajeshi wa Korea Kaskazini wamedhamiria na wako tayari kupigana kwa ujasiri na kufa kwa ajili ya kiongozi na chama. Sio kama tulikusanya tu watu ambao hawakuwa na pesa au chakula na kuwapeleka."

Dk. Doo Jin-ho wa Taasisi ya Udadisi wa Ulinzi ya Korea alisema kutangaza kwa vipaza sauti kulikuwa hatari sana: "Mara tu wanapowasha matangazo ya vipaza sauti [ya kupinga Korea Kaskazini], watashambuliwa mara moja kwa ndege zisizokuwa na rubani," alionya.

Afisa wa zamani wa Storm Corps Lee Woong-gil anapendekeza njia zisizo za moja kwa moja za mawasiliano.

Anaamini kuwa ujumbe wa video au rekodi za sauti zinaweza kuwa bora zaidi kuliko mawasiliano ya moja kwa moja:

"Itakuwa muhimu zaidi kutuma video fupi za waasi wa Korea Kaskazini ambao walikuja hapa [Korea Kusini] na wanaishi kwa furaha kama hivi.

Kwa sababu wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaweza kupata ugumu wa kupata nyenzo kama hizo, Bw. Lee anapendekeza kutuma vicheza MP3 au simu kuu kuu zilizopakiwa kama hizo.

Ustahimilivu

Licha ya hatari na mashaka haya, waasi wanabaki watiifu kwa kazi waliyotumwa.

"Sisi [waasi] ni watu wanaofanya kile tunachofikiri ni sawa. Ingekuwa na maana gani kuishi siku za mwisho za maisha yetu kwa ksuhiriki namna hii," Bw Sim alisema.

Wakati mipango ya waasi hao ikiendelea kuchunguzwa, serikali ya Ukraine tayari imechukua hatua.

Alitoa video ya propaganda ikiwalenga wanajeshi wa Korea Kaskazini, iliyopewa jina la Neno kwa Askari wa Jeshi la Wananchi wa Korea,ikipatikana kwenye majukwaa ya kijami ikiwemo YouTube na Telegram.

Wizara ya mambo ya nje na nyingine kwa Pamoja za Korea Kusini zilisema "hazina maoni" kuhusu iwapo waasi wa Korea Kaskazini watasafiri hadi Ukraine.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine Heorhii Tykhyi aliiambia BBC kwamba waasi wa Korea Kaskazini "wanakaribishwa" na kuhimizwa kujiunga na "jeshi letu la kimataifa".

"Tungefurahi kuwakaribisha nchini Ukraine na kufanya kazi nao.

Ujuzi wa vikosi vya Korea Kaskazini, lugha na uelewa wao wa namna walivyo vinaweza kuwa muhimu sana kwetu," alisema.

Pia alisema: "Kushirikiana kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin na wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita dhidi ya Ukraine kunaleta tishio kubwa la kimataifa ambalo linahitaji mwitikio wa kimataifa.

Imetafsiriwa na Martha Saranga