Kwanini Putin anatumia wanajeshi wa Korea Kaskazini na anafaidikaje nao katika vita vya Ukraine?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuna ushahidi unaoongezeka kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini wanapigana pamoja na jeshi la Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.

Idara ya ujasusi ya Korea Kusini imesema Urusi ambayo ni jirani yake wa kaskazini imepeleka zaidi ya wanajeshi 10,000 katika uwanja wa vita wa Urusi, likiwemo eneo la Kursk, na Pentagon na wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa takwimu sawa hizo.

Mapema mwezi Novemba, idara ya ujasusi ya Ukraine iliripoti ushiriki wa kwanza wa mapigano kati ya jeshi la Ukraine na vikosi vya Korea Kaskazini katika eneo la Kursk. Wakati huo huo, Moscow haikatai uwepo wa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo lake, lakini haijaweka wazi mipango ya kuwatumia.

Je, Korea Kaskazini ina nguvu gani za kijeshi?

Wanajeshi wa Korea Kaskazini pia wamezoea hali ngumu, kwa kuwa serikali ni taifa maskini la kiimla lenye nidhamu kali, masharti ya utumishi wa muda mrefu, kuanzia miaka mitatu hadi kumi, kulingana na aina ya huduma, na hali ya huduma ya kijamii, na uasi wowote unaadhibiwa haraka.

Korea Kaskazini, kama jirani yake Korea Kusini, ni nchi yenye milima, na Pyongyang inaona jirani yake wa kusini kuwa adui yake, kwahivyo wanajeshi wanafundishwa kupigana katika maeneo ya milimani na kuwa na uvumilivu wa hali ya juu na kubadilika, na wanafanya vizuri kwenye ardhi milima.

Je, jeshi la Korea Kaskazini lina udhaifu gani?

Jeshi la wananchi wa Korea kwa sasa halina uzoefu halisi wa mapambano. Zaidi ya miaka sabini imepita tangu Vita vya rasi ya Korea vianze, na ingawa Korea Kaskazini imejihusisha na migogoro nje ya mipaka yake, kama vile Vietnam, Mashariki ya Kati na Afrika, migogoro hii ilitokea katika miaka ya 1960 na 1970.

Jeshi la Korea Kaskazini kwa kiasi kikubwa linachukua mafundisho ya kijeshi ya Usovieti, na mipango ya mapigano ikilenga kupelekwa kwa silaha kubwa na vifaru vinavyoungwa mkono na vikosi vitengo vya kijeshi.

Mwanzoni mwa vita na Ukraine, jeshi la Urusi lilitaka kufanya usajiri mkubwa. Hata hivyo, kulikuwa na vikwazo. Wakati wowote Waukraine walikuwa na uwezo wa kuzuia sehemu moja ya jeshi la Urusi, kama kudhibiti mashambulio ya anga, kuharibu mizinga, au kuvuruga hivyo ufanisi wa vitengo Urusi ilipungua kwa kiasi kikubwa.

Mwaka 2017, Korea Kaskazini iliunda tawi jipya ndani ya jeshi lake, linaloitwa Special Operations Forces. Kikosi hiki kinakadiriwa kuwa kati ya wanajeshi 100,000 na 200,000, ambao lengo lao ni kuzia mashambulizi ya anga, na kumvuruga adui nyuma ya mistari ya vita. Kikosi hiki kina wepezi, chenye mafunzo ya hali ya juu sana na uwezo wa kufanya shughuli mbali mbali za kijeshi kwa kujitegemea.

Urusi pia ina vitengo kadhaa kama hivyo, lakini wanajeshi wa Korea Kaskazini hawana ujuzi na mbinu maalum za vita vya Urusi na Ukraine, kama vile matumizi makubwa ya mashambulizi na ndege zisizo na rubani, vita vya kupambana na silaha kali.

Maswali mengi yanabaki kwa wataalamu, ikiwa ni pamoja na iwapo wanajeshi wa Korea Kaskazini wanasimamia haraka vifaa vya kijeshi vya Urusi, au wanatumia kwa kiasi kikubwa mifumo yao ya zamani ya Usovieti na China? Maadili yao ni yapi? Na wanashindaje kizuizi cha lugha, kwani mawasiliano kwenye uwanja wa vita ni muhimu kwa ajili ya kuishi?

Je, Urusi inapata faida gani kutokana na wanajeshi wa Korea Kaskazini?

Hivi karibuni Pyongyang inatuma vikosi maalum vya kijeshi nchini Urusi. Ukraine iliripoti kuwasili kwa majenerali watatu wa Korea Kaskazini nchini Urusi, mmoja wao, Kim Yong-bok, ni kamanda wa vikosi maalum vya Korea Kaskazini na anashikilia nafasi ya naibu mkuu wa wafanyakazi wa jumla, huku wengine wawili wakisimamia ujasusi na operesheni katika jeshi.

Gazeti la New York Times liliripoti katika toleo lake lililochapishwa Jumatano iliyopita (Novemba 6) kwamba vikosi vya Korea Kaskazini vilipata hasara yao ya kwanza katika vita na wanamaji wa Urusi, na kuongeza kuwa vikosi vya Korea Kaskazini vinapigana katika Brigedi ya 810 ya kikosi cha majini cha Urusi, ambayo kwa sasa inafanya kazi katika mkoa wa Kursk.

Putin na Kim wanabadilishana zawadi muhimu kwa ujumbe wa kisiasa

Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa, Serhiy Kyslytsya, pia alisema kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wanapewa nyaraka za Urusi na sare za kijeshi, na kwamba Korea Kaskazini inapanga kutuma karibu vitengo vitano vya mapambano, kila kimoja kikiwa na wanajeshi 2,000 hadi 3,000, kuisaidia Urusi.

Mkuu wa kituo cha taarifa za Ukraine Andriy Kovalenko , anadai kuwa vikosi vya Urusi katika eneo la Kursk vimeanza kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini kuhusu mashambulizi mbalimbali na ndege zisizo na rubani.

Je, majeshi ya Korea Kaskazini yanaweza kubadilisha mienendo ya vita?

Wanajeshi elfu 10 hadi 15 elfu hawana nguvu kubwa katika muktadha wa vita vya Ukraine.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi iliripoti mnamo Julai kwamba watu wapatao 190,000 walikuwa wametia saini kandarasi tangu mwanzo wa mwaka, au karibu wanajeshi wapya elfu moja kila siku kwa hivyo, jeshi la Urusi linaajiri mara mbili au tatu idadi ya wanajeshi wanaotumwa na Korea Kaskazini kila mwezi.

Bila kujali kizuizi cha lugha, wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaweza kutumwa vitani na mafunzo kidogo, kwa sababu tayari wanafahamu misingi ya kijeshi.

Pyongyang ina faida gani?

Korea ya Kusini tayari imenufaika na mauzo ya silaha kwa Urusi, huku ikikadiriwa kuwa thamani ya mauzo hayo yananzia dola bilioni 2 hadi dola bilioni 5. Kutuma nguvu kazi katika eneo la vita pia ni faida: kutokana na mshahara wa chini wa askari wa Urusi katika vita, Pyongyang inaweza kupata karibu dola milioni 250 kwa mwaka kwa wanajeshi 10,000.

Aidha, Korea Kaskazini inatarajia kufaidika na teknolojia ya kijeshi ya Urusi, hasa katika maeneo ya makombora, anga, majini na nyuklia, na kadri msaada wa Korea Kaskazini unavyoongezeka, ndivyo Pyongyang itakavyoweza kudai ujuzi wa siri za kijeshi za Urusi.

Vikosi vya Korea Kaskazini pia vinapata uzoefu katika mapambano ya kisasa, ambayo yanaongeza uwezo wao wa kijeshi, hasa kwa kuwa Korea Kaskazini bado iko katika vita na Korea Kusini.

Washirika wa Kyiv wanasemaje?

NATO, Marekani na nchi nyingine zinazoiunga mkono Ukraine zimeelezea wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa mzozo huo. Ikumbukwe kwamba vikosi vya Korea Kaskazini viko katika ardhi ya Urusi, sio eneo la Ukraine, na kwahivyo hadhi yao ni ya utata.

Haijulikani kwa ujumla jinsi washirika wa Magharibi wanavyoweza kubadilisha msimamo wao. Wanaweza kuongeza zana za kijeshi kwa Ukraine, na Korea Kusini, moja ya wazalishaji wakubwa wa silaha duniani, ina jukumu kubwa ikiwa itaamua kutoa msaada wa kijeshi kwa Kiev.

Vikwazo vipya dhidi ya Urusi pia ni chaguo lililopo, na nchi za Magharibi zinaweza pia kutumia kutoridhika kwa China, kwani Beijing inaweza kuona uhusiano wa karibu wa Urusi na Korea Kaskazini kama tisho kwa ushawishi wake juu ya Pyongyang.

Hata hivyo, hatua hizi haziwezi kuvuruga juhudi za Urusi na Korea Kaskazini za kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati nchi hizo mbili.

Na Dinah Gahamanyi