Utamu na uchungu wa tozo Tanzania mpaka lini?

Na Beatrice Kimaro

Mchambuzi, Tanzania

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Kodi, ushuru na tozo ni msingi muhimu wa makusanyo ya mapato ya Serikali yoyote duniani.

Ni vyanzo vya asili, vinavyokubalika na kuwekewa misingi ya kisera, kisheria, kikanuni na matamko.

Kama ilivyo kwa nchi ningine duniani, Tanzania nayo inatumia njia hizi tatu ukiacha mikopo na ufadhili mwingine, kama njia muhimu za kukusanya mapato ya serikali.

Kwa mfano katika bajeti yake ya mwaka huu wa fedha (2022/2023), Serikali imepitisha bajeti ya shilingi trilioni 41, kati ya mapato hayo, kiasi kitakachokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kinakadiriwa kuwa shilingi trilioni 23 na mapato yasiyo ya kodi kutoka wizara, idara, taasisi na mamlaka za serikali za mitaa yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 4.

Sehemu kubwa ya watanzania wanakubaliana kwamba tozo na kodi ni muhimu kwa utekelezwaji wa bajeti hii na makusanyo yake. Na kwa serikali inayotaka kutoa huduma kwa watu wake, njia hizi zinakubalika kwa mantiki ya maendeleo. Lakini kwa nini kwa muda sasa suala la makato ya tozo nchini Tanzania limekuwa linapigiwa kelele?

Tozo zinazolalamikiwa na kelele zake zilipoanzia

Maelezo ya video, Tanzania: Agizo la wapangaji kupeleka 10% ya pango TRA imepokelewaje?

Katika kipindi cha wastani wa mwaka mmoja uliopita kumekuwa na kutambulishwa ama kupandishwa kwa tozo mbalimbali nchini Tanzania.

Julai 15, 2021 gharama za miamala ya fedha za mitandao ya simu nchini Tanzania ilipanda rasmi baada ya Serikali kupandisha tozo ya miamala inayofanyika kwenye mitandao yote. Lilikuwa jambo la kisheria, kwa sababu ni uamuzi uliopitishwa na bunge.

Tozo kwenye mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa iliongezeka pia kwa karibu shilingi 100 kwa lita, ingawa juhudi zilifanyika za kupunguza makali ya kupanda huku kwa serikali kutenga shilingi bilioni 100.

Tozo kwenye mita za umeme-Lipa Umeme Kadiri Unavyotumia (LUKU) na pia tozo kwenye kadi za simu. Na sasa kumeibuka hoja zingine zinazohitaji majibu ya serikali kuhusu tozo kwenye visimbuzi na tozo kwenye miamala ya benki.

Sintofahamu hii imeibua kelele nyngi mitandaoni, huku baadhi ya maoni, yakionesha wengi kutofurahia njia za makato haya licha ya kukubaliana na umuhimu wa mapato yanayopatikana kutoana na tozo hizo.

Utamu wa tozo

Hakuna asiyejua kwamba mapato makubwa ya serikali yanatafsirika kwenye maendeleo yanayopatikana. Kwa mfano taarifa iliyotolewa mwezi Januari, 2022 kwa tozo mpya zilizoanza Julai, 2021, zilisaidia kujenga madarasa 5,000 nchi nzima.

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu alisema “Shilingi bilioni 7 zilizopatikana kwenye tozo zilielekezwa katika elimu msingi”.

"Pia tunajenga vituo vya afya 233 katika halmashauri zetu zote Tanzania Bara, tarafa 207 hazikuwa na vituo vya afya, kupitia tozo za makusanyo ya ndani ujenzi wa hivi vituo unaendelea vizuri na upo katika hatua ya ukamilishaji’, alisema Ummy.

Kwa sentesi hizi za serikali, unaweza kukubaliana kwamba kama zinatumika vizuri tozo ni tamu, na utamu wake unawagusa wengi kupitia huduma katika sekta za elimu, afya barabara na maji.

Uchungu wa tozo

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Utafiti wa shirika la Twaweza uliotolewa Agosti 25, 2022 kuhusu tozo unaonesha wengi wa watanzania wanaamini kuhusu umuhimu wa tozo, lakini hawazikubali.

Karibu wananchi wote (90%) wanakubaliana na wazo la msingi kwamba makusanyo kama haya ya tozo na kodi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Lakini wengi (75%) wanasema viwango vikubwa vinavyowekwa vinawafanya kuhangaika kulipa. Na hapa ndipo panapoanzia uchungu wa kwanza.

Ukiwasikiliza wachumi na watu wa fedha, wanasema, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kufuatia janga la Covid 19 na vita vya Ukraine ukuaji wa uchumi umekuwa wa mashaka, gharama za maisha zimepanda na uwezo wa watu wa kununua bidhaa (purchasing power) umepungua.

‘Kama kipato ulichonacho leo, hakiongezeki, lakini tozo zinazongezeka kabla hujaweza kutumia kununua bidhaa, maana yake utauona ugumu fulani’, anasema Raphael Kugesha, mtaalam wa uchumi na maendeleo ya jamii.

Anachokisema mchumi huyu ndiyo msingi wa pili wa vilio na malalamiko mengi ya tozo yanayoendelea sasa na kuibua uchungu mwingine.

Lakini mbali na viwango vya makato vinavyopigiwa kelele, lakini namna ya kukata, kunaonekana kuwepo kwa kitu kinachoitwa Katika mfumo wa kodi ‘double taxation’. Kwa mfano mfanyakazi aliyelipwa mshahara anakatwa kodi inayoitwa PAYEE, akitoa benki mshahara huo huo kuupeleka kwenye simu atakatwa makato mengine, akimtumia mama yake kijijini, atakatwa VAT, atakatwa tozo na atakatwa gharama za kutuma. Uchungu mwingine.

 Athari za tozo ‘lukiki na za kiwango kikubwa kwa mlalahoi'

Zipo athari za moja kwa moja kiuchumi kwa uwepo wa tozo nyingi na za kiwango kikubwa, ambazo mzigo mkubwa unamuangukia ‘mlalahoi’ mwenye kipato cha kati na chini kabisa.

Athari ya kwanza ni kupungua kwa mzunguko wa fedha, kitu ambacho kitaaathiri kipato cha ‘mlalahoi’.

Mlalahoi huyu akiwa na kipato duni, atakosa uwezo wa kununua bidhaa na huduma na hapo ndipo ugumu wa maisha utakapomuelemea.

Akikutwa na ugumu huu wa maisha, atakutana na msongo wa mawazo, atashindwa kuzalisha na mwishowe hataweza kuwa na uwezo wa kuchangia kwenye kodi na tozo kwa kiwango kinachopaswa ama tarajiwa.

Athari nyingine ni kuathiri biashara hasa za mitandaoni na kupunguza mapato kwa kampuni za simu. Twaweza kwenye utafiti wao mpya wa sasa kuhusu tozo, 44% ya wananchi wamepunguza matumizi ya miamala ya fedha kupitia simu tangu Julai 2021. Sababu inayotajwa ni kuongezeka kwa gharama ikiwemo tozo ya miamala.

Jambo ingine, utitiri wa tozo na makato mengine kwenye miamala ya simu, ama luku, mabenki, au visimbuzi vikithibitika, vitaongeza gharama za huduma.

Kupanda kwa gharama za huduma, kutamkosesha ama kumpunguzia huduma mwananchi mlalahoi ambazo angependa kuzipata.

Tozo hazikwepeki lakini moja ya suluhu yake ni hii

Kenya, ni moja ya nchi zinazotumia sana huduma za kifedha kwa kutumia miamala ya simu, karibu robo tatu ya wananchi wa Kenya wenye kipato wanafanya malipo ya huduma na bidhaa kwa njia za simu.

Ukinunua bando, Kenya hautakata, kwa mfano bando la shilingi 99 ya Kenya wastani wa kama shilingi 1,800 za Tanzani kupitia Safaricom, haukatwi hata sumni. Nchini Tanzania ukinunua bando lolote utakatwa VAT.

Kutokuwepo kwa tozo, kodi na gharama kubwa za makato kumeifanya biashara ya Kenya kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi ulioimarika zaidi katika nchi za Afrika Mashariki.

Tanzania ipo Lipa namba kwenye kampuni za simu, lakini haijashika kasi sana, kama ilivyo Kenya. Kama ilivyonakiliwa na taarifa ya utafiti wa Twaweza, Serikali ilitarajia kukusanya shilingi trilioni 1.254 kutokana na tozo ya simu lakini hadi mwisho wa mwaka 2021 iliweza kukusanya shilingi bilioni 360 pekee. Makato mengi yanawakimbiza wengi kutumia huduma za kifedha kwenye simu.

Mbali na kubuni vyanzo vingine vingi vya mapato vinavyohusisha rasilimali za nchi kama ardhi, Serikali inapaswa kupunguza viwango vya tozo na kupunguza kodi ya Ongezeko la thamani (VAT), ili kufanya watu wengi kutokimbia huduma za kifedha za simu, kama tafiti inavoonesha.

Inawezekana kwa wakati tuliopo sasa na majukumu lukuki iliyo nayo serikali tozo hazikwepi, lakini fikra ni kuwa na tozo rafiki na zinazoweza kumfanya mtu kulipa bila manung’uniko.

Kwanini zisifutwe ama kuondolewa kabisa?

Wengi wanajiuliza haiwezekani kufutwa kwa tozo? Haiwezekani kufikiria vyanzo vingine?

Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba wakati anazungumzia malalamiko ya awali kuhusu tozo mbalimbali zilizopitishwa, alithibitishwa kwamba, tozo zilizowekwa zote zimefanyiwa utafiti wa kutosha.

Pamoja na kusema tozo hizo zitaangaliwa akafafanua kwamba uwepo wake ni sheria ya Bunge, ambayo yeye kama Waziri hawezi kuzifuta ama kuziondoa. Alichokisema wakati huo akizungumza na BBC ni kwamba kinachoweza kufanyika ni kupitiwa kwa kanuni kuangalia kama utekelezaji wake unafanyika kwa njia isiyofaa.

Pamoja na yote, elimu kwa mkatwa tozo ni zaidi ya elimu ya mwalimu kuingia darasani na kufundisha. Ni zaidi ya kumwambia mafanikio ya tozo. Kwa sasa kazi kubwa isiyo na kikomo iliyopo ni kumfanya mtanzania kutamani na kupenda kulipa tozo na kodi zingine kuliko jambo lingine lolote. Kama ni lazima sana kwa sasa kuwa na tozo zilizopo sasa kabla ya kufikiria kuongeza zingine, njia rahisi kubwa ni kumfanya mtanzania kuwajibika kwa kuwa na tozo zinazolipika bila kuathiri maisha ya mlipa kodi.