Uchaguzi Kenya 2022: Mwanamke anayewakusanyia wanasiasa umati wa watu - lakini hatapiga kura

Na Dickens Olewe BBC News, Nairobi

Diana Mwazi ni mmoja wa vijana wengi wa Kenya ambao wanaona uchaguzi ujao wa nchi kama njia ya kupata pesa, badala ya fursa ya kuwapigia kura watu ambao wanaweza kuleta mabadiliko katika maisha yake.

Kijana huyo mdogo mwenye umri wa miaka 20 amejichonga sehemu ndogo ya ushawishi katika siasa za Kenya zinazotawaliwa na wanaume wengi, katika makazi yasiyo rasmi ya Kibra katika mji mkuu, Nairobi, anakoishi.

Kwa ada, anatafuta watu wasio na ajira kuhudhuria mikutano ya kampeni - na ana furaha kutoa huduma yake kwa chama chochote cha kisiasa.

"Nimefurahishwa na uchaguzi kwa sababu ninapata kazi kutoka kwa wanasiasa ambao wanataka kuonyesha kwamba wanaungwa mkono na wananchi," anasema.

Pilka pilka za uchaguzi zimetanda nchini kabla ya uchaguzi wa Agosti 9 - kauli mbiu za chama zimekuwa sehemu ya burudani za kawaida, mabango ya kisiasa yamebandikwa katika maeneo ya umma na hewani kumejaa muziki na nyimbo zinazotangazwa kutoka kwa spika kubwa zilizopandishwa kwenye magari ya kampeni.

Wanasiasa wakubwa na wakongwe hajasaza chochote kwa sababu kujenga hisia ya umaarufu ni muhimu - na hapo ndipo umati wa watu unapoingia.

"Kuhamasisha watu kuhudhuria mkutano sio kazi ngumu kwa sababu kupata vijana ambao hawana kazi ni rahisi sana," anasema Bi Mwazi, ambaye hana mpango wa kupiga kura mwenyewe.

"Wanasiasa wote ni waongo. Wakati wa uchaguzi wanamiminika hapa kama kondoo, wakiahidi: 'Nitafanya hivi, nitawapa vijana kazi.' Lakini unapowachagua hawafanyi lolote."

Uhamasishaji wa umati ni "hustle", anasema Bi Mwazi

Kwa kawaida yeye hununua viatu sokoni na kuviuza kupitia vikundi vya WhatsApp, na pesa hizo husaidia kukuza kipato kidogo cha mama yake kama mfanyakazi wa afya ya jamii.

Katika kipindi cha kampeni, Bi Mwazi anafanya kazi na wahamasishaji wengine wa umati na kulingana na idadi ya watu walioombwa, anaweza kukusanya kati ya watu 40 na 100.

"Ninapata shilingi 500 za Kenya ($5; £3) kwa kila tukio lakini baadhi ya wanasiasa ni wakarimu," Bi Mwazi anasema.

Wahudhuriaji hupata kiasi sawa

"Wanasiasa wanataka wapinzani wao waone kwamba wana uungwaji mkono zaidi, kwa hivyo wanapiga picha za umati na kutuma kwenye mitandao ya kijamii," Bi Mwazi asema.

Amepata mafanikio katika kuhamasisha wasichana, lakini vijana wa kiume wameonekana kuwa wagumu zaidi.

"Wanaume si wa kutegemewa, wanalalamika kuhusu fedha zinazotolewa," anasema, akiongeza kuwa wakati mwingine makundi yanayopingana ya vijana yanapigana kwa nguvu wanapokutana kwenye kampeni.

Katika nchi ambayo angalau 70% ya watu wana umri wa chini ya miaka 35, kuhakikisha wapigakura vijana wanajitokeza kwenye uchaguzi ni muhimu kwa wale wanaowania nyadhifa katika chaguzi sita zinazofanyika kwa wakati mmoja, ikiwa ni pamoja na urais, bunge na magavana wa kaunti.

Skip Uchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu wagombeaji wa Urais and continue readingUchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu wagombeaji wa Urais

End of Uchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu wagombeaji wa Urais

Wagombea hutumia mamilioni ya dola kununua nyenzo za kampeni, vifaa na mawasiliano, ikiwa ni pamoja na kuajiri washawishi wa mitandao ya kijamii ili kuchapisha machapisho yanayofaa.

Pia inabidi waendane na wapiga kura wanaozidi kuwadai wanaovamia wanasiasa hao kutaka kushinda - wanasiasa wa Kenya ni baadhi ya wanaolipwa vizuri zaidi duniani.

Mfumo wa kisiasa nchini umeundwa ili kuhakikisha kuwa wale wanaotumia pesa nyingi zaidi wanachaguliwa, anasema mwanaharakati maarufu Boniface Mwangi, ambaye aligombea ubunge katika uchaguzi wa 2017 bila mafanikio.

"Mgombea mmoja alitumia takriban $2m (£1.5m) kuchaguliwa kuwa mbunge," asema. "Ni vigumu sana kwa mgombea maskini kuchaguliwa kwa sababu watu maskini hawachagui watu maskini - watu maskini wanahitaji kuhamasishwa kukuchagua."

Bw Mwangi, ambaye ana zaidi ya wafuasi milioni mbili kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, mara kwa mara hupokea maombi mengi kutoka kwa vijana wa Kenya, yakiwemo maombi ya kazi.

Anasema hii inaangazia kushindwa kwa wanasiasa kuunda nafasi za kazi, na anaongeza kuwa wapiga kura wamekuwa wabishi - wanapiga kura kwa yeyote anayewalipa. 

“Baadhi ya wanasiasa maarufu hapa nchini hawana umaarufu kwa kuwa ni viongozi wazuri, wanapendwa na watu kwa sababu wana ukarimu wa pesa zao, wapiga kura wameamua ‘kura zetu zinauzwa’ hivyo imekuwa ni shughuli,” Bw. Mwangi anasema.

"Katika demokrasia inayofanya kazi, watu unaowachagua wanafanya kazi kwa ajili yenu. Nchini Kenya wapiga kura wanafanya kazi kwa ajili ya wanasiasa," anaongeza.

Karibu na nyumba ya mawe ya chumba kimoja ya Bi Mwazi, anakoishi na mamake na wadogo zake wawili, kuna safu ya nyumba zilizojengwa kwa bati. Zimetenganishwa na njia nyembamba ya uchafu ambayo hukatizwa mara kwa mara na mabomba ya maji yenye rangi nyingi yanayopita katikati ya msongamano mkubwa wa makazi duni yanayotawanyika.

Huko, nakutana na James Mogaka au "Jimmy Mwanasheria".

Amevaa nadhifu na ana nywele fupi za kusokota(rasta)na amevaa glavu nyekundu za raba. Anafungua mtaro ulioziba, umejaa mifuko ya nailoni, chupa na taka nyinginezo.

Alipata jina lake, ambalo wakati mwingine lilitumiwa kama kejeli ya kikatili, kwa sababu alisomea sheria. Lakini kwa kuwa hawezi kupata kazi rasmi, anafanya kazi za mikono ili kujipa kipato, na pia kuigiza kama nyongeza kwenye vipindi vya televisheni vya ndani.

Tofauti na Bi Mwazi, kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 anapanga kumpigia kura mgombea ambaye anadhani ataleta mabadiliko.

Lakini anasema kuwa vijana wengi wanaona ugumu wa kusimama na imani zao, na wanalazimika kupitia uzoefu wa kudhalilisha wa kuuza kura zao ili kupata "fedha ya tumbo".

"Wapiga kura wanajua hata wasipochukua fedha kutoka kwa wanasiasa, mtu mwingine atachukua, na matatizo yao yatabaki," James Mogaka Mpiga kura nchini Kenya

Kenya ina tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, kulingana na Jacqueline Mugo, mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho la Waajiri nchini Kenya.

"Kijana aliyekatishwa tamaa, aliyekasirika na asiye na subira ni tatizo la kitaifa… Kama una vijana ambao hawawezi kujikimu na wazazi wao wanazidi kushindwa kuwahudumia, hilo ni tatizo linalongoja kulipuka," anasema.

"Ukiangalia kundi la umri kati ya miaka 16 hadi 35, basi kiwango cha ukosefu wa ajira kinaweza kuwa cha juu hadi 40%, kwa hivyo mambo ni mabaya sana lakini sidhani kama inaweza kuwa mbaya zaidi," Bi Mugo anasema na kuongeza kuwa vijana wanapaswa kuendelea kujihusisha na siasa ili kupata mabadiliko.

Bi Mwazi, ambaye anatarajia kusomea sanaa ya upishi siku moja, hajashawishika.

Katika wiki zijazo ataendelea kuruka kutoka mkutano mmoja hadi mwingine ili kujipatia riziki, bila kutarajia kusikia kutoka kwa wanasiasa mara tu uchaguzi utakapomalizika.

"Wengi wao hawaishi hapa hata hivyo," anasema kwa kuinua mabega.