Viongozi wanawake Kenya wamekuwa na mchango gani katika siasa za nchi hiyo?

Na Anne Ngugi

BBC Swahili,Nairobi

Kivumbi cha kisiasa nchini Kenya kinatifuka kila uchao ikiwa imesalia na chini ya miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu.

Ni mchakato ambao umejawa mengi lakini uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na kikubwa kwa wanawake kote nchini kwani kwa mara ya kwanza kuna uwezekano kwa mwanamke kushikilia nafasi ya ngazi ya juu serikalini baada ya moja ya mirengo mikubwa ya kisiasa katika uchaguzi wa mwaka huu -Azimio la Umoja kumteua Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa mgombeaji wake wa urais Raila Odinga.

Mrengo mwingine unaoongozwa na naibu wa rais William Ruto-Kenya Kwanza nao umeahidi kuwapa wanawake asilimia 50 ya nafasi za mawaziri endapo watashinda uchaguzi.

 Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya IEBC wagombea wanne wa urais wameidhinishwa kwa kuwania kiti hicho.

Kati ya wagombeaji hawa wakuu wa urais, watatu waliwateua wanawake kama wagombea wenza kwenye kinyang’anyiro hicho na kando na muunganon wa Raila Odinga tiketi nyingine mbili za wagombea urais zina wanawake kama wagombea wenza.

Chama cha Roots Party kinachoongozwa na George Wajackoyah kina mwanamke Justina Wamae kama mgombea mwenza na Ruth Mutua kutoka chama cha Agano.

Hatua hizo zinadhihirisha umuhimu mkubwa ambao uongozi wa wanawake umechukua katika siasa za Kenya na hasa katika uchaguzi huu unaokaribia .

Kuanzia wawaniaji wanawake katika nyadhifa mbalimbali , na pia uzito wa kura za wanawake nchini Kenya katika kusukuma au kutathmini atakayeshinda urais katika uchaguzi wa mwaka huu .

Uchaguzi Kenya 2022:Mengi zaidi kuwahusu wagombeaji wa Urais

Je ni wanawake wapi ambao ni nguzo kisiasa ?

Wanawake ni wengi mwaka huu ambao wamejitosa kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa nchini Kenya.

 Matumaini ya uongozi wa wanawake hayakuanza hivi karibuni na kumekuwa na majina mengi ya kutambulika katika jitihada hizi na wanawake wanaojipata kama nyuso za kampeni hii kwa sasa wanabeba matumaini ya wengi wa zamani na jinsia ya kike ya uongozi wa kizazi kijacho.

 Matumaini yao ni kwamba huu ndio mwanzo wa ngoma ya uongozi wa wanawake kupaa hata juu zaidi katika siku zijazo .

 Macho ya wengi katika hili yapo sasa kwa kundi la wanawake kadhaa ambao ndio wanasheheni matumaini haya iwapo watafaulu bila kujali wapo katika mirengo gani ya kisiasa .

Martha Karua

Huyu ni mwanamke ambaye anafahamika na wengi kwa kimombo kama “The iron Lady” tafsiri nyepesi ni chuma, jina hili amelipata kutokana na uweledi wake kama mwanasheria na vilevile ukakamavu wake wa kuzungumza wazi wazi kuhusiana na maoni na misimamo yake inapowadia maswala ya uongozi, utawala, haki za kibinadamu na pia hali ya ufisadi nchini Kenya .

Huyu ni mwanamke ambaye amekuwa mstari wa mbele kukosoa serikali zilizopita hata wakati amekuwa nje ya serikali hizo .Martha Karua ambaye sasa ni mgombea mwenza wake Raila Odinga ,alipozungumza na BBC alisema kuwa bado uwakilishi wa wanawake katika nyadhifa za uongozi uko chini ukilinganisha na idadi ya wapiga kura wanawake ambayo inakisiwa kuwa asilimia 51 nchini Kenya

“Uongozi wa wanawake sasa unakubalika katika nyanja zote , unapata kuwa kuna wanawake ambao wanawania nyadhifa tofauti kila mahali na bila shaka ni idadi ya juu kuliko ambavyo imekuwa hapo awali .Hatupo ambapo tunafaa kuwa kwani tunafaa kuwa tunawania nafasi kulingana na idadi ya wanawake nchini.”alisema Karua

Karua anasema kwamba imekuwa ni barabara yenye utelezi kwa wanawake viongozi na pia kwa wapiga kura wanawake kujitizama kwa nafasi halisi ya kwamba wanaweza kuwa uongozini na wafanye kazi kwa njia sawa kama sio bora kuliko wanaume .

Anaongeza kuwa changamoto imekuwa ni tetesi na semi zinazotumiwa kudhalilisha wanawake na hapo anasema kwamba hata yeye binafsi hajaepuka changamoto hiyo ila amekuwa na mikakati ya kufungia masikio wanaotumia jinsia kuwavuta chini wanawake walioko uongozini au ambao wanamezea mate nafasi za uongozi popote nchini Kenya .

“Mimi nimekuwa na mkakati wa kutotilia maanani baadhi ya wanaume wanapopanda kwenye jukwaa na kutumia lugha ya kisiasa ya kunidhalilisha , inakuwa ni kusudi yao kwamba waviuruge nia yangu kisiasa na kuniondoa kwenye mpango wangu kisasa ,kusudi ni wanipe uoga kwa njia hizo na kwa hio mimi husema ukisikiliza kila sauti mbele yako hautawahi kuafikia chochote” aliongezea Karua

Kuhusu kuzungumza waziwazi anachokifikiria kuhusu uongozi hapo awali amenukuliwa akitoa semi nzito bila uwoga

“Je, tunawachaguaje viongozi wetu, je tunasukumwa na maadili, takrima au shangwe? Tunahitaji kuwa na uongozi unaozingatia maadili.” Amenukuliwa akisema .

Kuhusu swala la rushwa na ufisadi hapa napo hakukosa maoni

“Watu bado wanapora rasilimali za umma na hawawajibishwi. Tunahitaji mabadiliko ya mtazamo na utekelezaji wa sheria zetu, sio marekebisho ya katiba.

Hali kadhalika kuwa na shinikizo kubwa kwa watu kupenda nchi yao kwa hali zote

“Nchi unazofikiri unataka kutembelea zilijengwa na watu kama wewe na mimi. Vijana wametakiwa kufanya vyema zaidi kuijenga Kenya”

Itakuwa ni mara ya kwanza mwanamke anaingia kwenye tiketi ya kinyang’anyiro cha juu zaidi nchini Kenya na kinachosubiriwa ni kuona iwapo uwepo wa Martha Karua utakuwa mtikiso katika muelekeo wa siasa za Kenya .

Charity Ngilu

Siasa za Kenya na pia uongozi wa wanawake haziwezi kutajwa bila jina lake Charity Ngilu . Huyu ni gavana wa sasa wa Kaunti ya Kitui Mashariki mwa Kenya na tayari ametangaza kwamba hatokitetea kiti chake.Mchango wake katika siasa za mfumo wa vyama vingi na pia kupigania uongozi wa wanawake hauwezi kupuuzwa .

Mwaka 1997 aligombea urais na kuwa mwanamke wa kwanza nchini Kenya kuwania kiti hicho . Alijiunga na chama cha Social Democratics Party SDP na alimaliza katika nafasi ya tano.

Ni mwanasiasa ambaye hajakata tamaa ya kuendelea kupigania usawa wa kijinsia akitambuika sana wakati huo kwa jina la “masaa ni ya Ngilu” .Hakushinda kiti hicho lakini ujumbe ulikuwa umeshatoka-Wanawake walikuwa na nia ya kuzipigania nafasi za uongozi nchini Kenya katika nyanja zote.

Charity amekuwa mbunge kwa miaka mingi na pia amehudumu kama waziri .

Alipozungumza na BBC Swahili alisema ana imani kwamba bado kuna nafasi ya mwanamke kutwaa uongozi nchini Kenya na hasa inapotizamwa kwamba kwa sasa wanawake wana uakilishi katika nyadhifa muhimu serikalini na pia uongozi wa kisiasa . 

Anne Waiguru

Wanawake wengine waliojitosa katika upongozi wa kisiasa nchini Kenya ambao safari zao zinaweza kuangaliwa katika jitihada za kuendeleza uongozi wa wanawake ni Anne Waiguru , amekuwa kwenye ulingo wa uongozi katika nyadhifa serikalini na sasa ni Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga ,Kati mwa Kenya Anne Waiguru bado yuko kwenye kinyang’anyiro mwaka huu akilenga kutetea nafasi yake .

Alipozungumza na BBC ,Waiguru alisema kwamba ili wanawake wawe kwenye nafasi za juu uongozini , wanafaa kuwa tayari kuwapiga kura wenzao .

Dhana ya kwamba ‘Adui ya mwanamke ni mwanamke mwengine ’ mwanasiasa huyu anasema imekwaza jinsia hii hasa kwa sababu inatumiwa kisiasa visivyo.

“Idadi ya wanawake nchini Kenya ni kubwa , iwapo wanawake wenyewe wataamua kuwaweka wanawake wenzao madarakani basi hilo litawezekana .Ndio wanawake wapiga kura hapo awali wamepigia wanaume viongozi kura lakini sasa kuna fursa ya kufanya mambo kwa njia tofauti ”alisema Waiguru 

Kila Kaunti nchini Kenya ina majina ya wanawake tajika ambao wapo kwenye tiketi za kuwania nafasi mbali mbali katika uchaguzi ujao , kando na wadhifa wa urais pekee nafasi nyingine kama ubunge, useneta , madiwani na gavana yana uakilishi wa wanawake .

Wanawake kama Aisha Jumwa kutoka Pwani ya Kenya , Gladys Wanga Magharibi mwa Kenya , Peris Tobiko kutoka kaunti ya Kajiado ,Sabina Chege kutoka eneo la kati mwa Kenya , Miliie Odhiambo ,Magharibi mwa Kenya na Sophia Abdi Noor kutoka Kaskazini mwa Kenya ni miongoni mwa wengine wengi ambao wanazidi kupambana na wanaume kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa katika sehemu mbali mbali za Kenya . 

Huku kampeini zikishika kasi nchini humo wanawake wanajizatiti kujinadi kwa umma kwa njia zote kama tu wanavyofanya wenzao wa kiume .

Wadadisi wa kisiasa nchini wanakubali kwamba wakati huu tiketi iliyo na mwanamke haipuuzwi kama ilivyokuwa zamani .

 Taswira kamili kuhusu uwezekano wa mwanamke kuiongoza Kenya siku zijazo itategemea mengi-ikiwemo matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu .

Wengi hata hivyo wanaafiki kwamba iwapo kuliwahi kuwa na uchaguzi ambao utatoa njia kwa wanawake kupata ujasiri zaidi kupigania wanachostahili-usawab hatakatika uongozi,basi ni katika uchaguzi huu.

Mengi pia yatategemea utayari wa wapiga kura kutembea barabara ambayo wachache wamethubutu kuichukua

Mengi zaidi kuhusu Uchaguzi wa Kenya