Je, Vladimir Putin anaweza kukamatwa kwa uhalifu wa kivita?

Serikali ya Afrika Kusini inatathmini iwapo itamwalika Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhudhuria mkutano mwezi Agosti, baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa jinai (ICC) kutoa hati ya kukamatwa kwake.

Kuna maswali yameibuka kama kibali cha ICC kina nguvu yoyote, na kama kweli serikali ya nchi yoyote ingeweza kumkamata Bw Putin.

Rais Putin anatuhumiwa kwa nini?

ICC ilitoa hati za kukamatwa Machi 17 dhidi ya Rais Putin na kamishna wa haki za watoto wa Urusi, Maria Lvova-Belova.

Inadai kuwa wote wawili wanahusika kibinafsi kwa uhamishaji haramu wa watoto kutoka Ukraine hadi Urusi, kufuatia uvamizi wa Urusi mnamo Februari 2022.

Pia inamshutumu Bw Putin kwa kukosa kutumia mamlaka yake ya urais kukomesha watoto kufukuzwa nchini.

Kulingana na Ofisi ya Kitaifa ya Habari ya Ukraine, watoto 16,221 walipelekwa Urusi kwa nguvu.

ICC imeingilia kesi hii kwa sababu Ukraine iliipatia mamlaka ya kuchunguza uhalifu wa kivita uliofanywa katika eneo lake.

Hii ni mara ya kwanza kwa mahakama hiyo kutoa waranti dhidi ya kiongozi wa mmoja wa wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameitaja hatua ya ICC "uamuzi wa kihistoria, ambapo uwajibikaji wa kihistoria utaanza."

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ni nini?

Mahakama ya ICC ambayo makao yake makuu yako mjini The Hague nchini Uholanzi, inachunguza na kuwafungulia mashtaka watu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Ilianzishwa chini ya Mkataba wa Roma mnamo 1998 na ilianza kufanya kazi mwaka 2002.

Ina bajeti ya kila mwaka ya £130m kutumia katika uchunguzi, imeshughulikia kesi 40, na imewahukumu watu 10.

Kwa sasa ICC ina mataifa wanachama 123 kama watia saini, ambao wanakubali mamlaka yake.

Lakini, Urusi haijatia saini kukubali mamlaka ya ICC. Marekani na China pia hazijafanya hivyo.

Je, ICC inaweza kumkamata Putin?

Mahakama ya ICC haina mamlaka ya kuwakamata washukiwa.

Rais wa mahakama hiyo, Piotr Hofmanski, amesema ni jukumu la jumuiya ya kimataifa kumkamata Bw Putin.

Kwa kuwa mamlaka ya kisiasa ya Bw Putin nchini Urusi kwa sasa hayana pingamizi, na kwa kuwa Urusi haikuwahi kujiandikisha kuwa mwanachama wa ICC, hakuna uwezekano wa yeye kukamatwa nchini mwake.

Msemaji wa Kremlin Maria Zakharova amepuuzilia mbali hati za kukamatwa kwa Bw Putin na Bi Lvova-Belova kuwa "hazina maana" na anasema "ni batili na ni batili".

Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa ICC Khalid Khan aliiambia BBC kwamba wawili hao hawana kinga dhidi ya kufunguliwa mashitaka kwa madai ya uhalifu wa kivita kwa sababu tu Urusi haitambui ICC.

"Mataifa yote yana wajibu wa kutii sheria za kimataifa," alisema.

Mataifa yanaweza kumkamata?

Bw Putin anatazamiwa kuzuru Afrika Kusini mwezi Agosti kwa kongamano la mataifa ya Brics (Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini).

Afrika Kusini imetia saini mkataba wa kujiunga na ICC na serikali yake haina uhakika kama inapaswa kutekeleza agizo la kukamatwa kwa Bw Putin au kama inaweza kumchukulia kama mgeni anayekaribishwa.

"Afŕika Kusini itabidi iangalie vifungu vilivyopo vya sheŕia yetu,” waziŕi wake wa mambo ya nje, Naledi Pandor, alisema.

Hata hivyo, pia aliishutumu ICC kwa viwango viwili, akisema: "Kuna nchi nyingi na viongozi ambao wamefanya unyanyasaji mkubwa katika mazingira ya migogoro, lakini bado hawajachukuliwa hatua,"

Afrika Kusini na Urusi zina uhusiano wa kirafiki, na wanamaji wao walifanya mazoezi pamoja mnamo Februari.

Afrika Kusini imepuuza vibali vya kukamatwa kwa ICC hapo awali.

Mahakama ilitoa vibali vya kukamatwa kwa Omar al-Bashir, Rais wa Sudan, kwa uhalifu dhidi ya binadamu mwaka 2009 na 2010.

Yalihusiana na mzozo huko Darfur mwaka 2003 ambao ulisababisha vifo vya watu 300,000.

Hata hivyo, mamlaka za Afrika Kusini zilikataa kumkamata alipomzuru nchi hiyo mwaka wa 2015.

Bw Putin anatarajiwa kuzuru India kwa ajili ya mkutano wa kilele wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai mnamo Juni 2023 huko Varanasi, na mkutano wa kilele wa G20 mnamo Septemba.

Hata hivyo, India haijajiandikisha kuwa mwanachama wa ICC na haitarajiwi kufanyia kazi vibali vya kukamatwa.

Serikali ya Hungary, ambayo ina uhusiano wa kirafiki na Urusi, imesema haitamkamata Bw Putin katika eneo lake ingawa ometia saini saini wa mkataba wa ICC.

Inasema kufanya hivyo kungekinzana na katiba yake.

Bw Putin amesafiri katika nchi nane tangu kuanza kwa Vita vya Ukraine - jamhuri saba za zamani za Usovieti na Iran. Wote ni washirika wa karibu wa Urusi.

Haiwezekani kwamba angesafiri kwenda nchi yoyote ambayo anaweza kukamatwa.

Hata hivyo, tishio kwamba huenda akakamatwa nje ya nchi linaweza kupunguza uhuru wake wa kusafiri katika siku zijazo.

Je, ni kweli Putin anaweza kukabiliwa na mashtaka?

Hata kama Bw Putin angekamatwa, basi kungekuwa na vikwazo kadhaa vya kisheria kwake kushtakiwa katika mahakama ya ICC.

Mahakama hiyo iliundwa ili kusikiliza kesi kwa niaba ya nchi ambazo ni watia saini wa ICC na ambazo zinakubali mamlaka yake - na Urusi sio mojawapo wa mataifa hayo.

Na ingawa Ukraine iliitaka ICC kuchunguza madai haya ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Urusi, bado haijatia saini mkataba na ICC yenyewe (haijawahi kuridhia kutia saini kwake Mkataba wa Roma wa ICC).

Hata hivyo, mahakama ya ICC imetetea uamuzi wake wa kutoa hati za kukamatwa ikisema kuwa uhalifu wa kivita wa Urusi nchini Ukraine unaendelea na kwamba inajaribu kuzuia uhalifu zaidi kutokea.