Bomu chafu: Marekani yafanyia majaribio dawa mpya ya kuzuia mionzi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Marekani, wameanza kujaribu njia mpya ya kuondoa dutu hatari za mionzi kutoka kwa mwili wa binadamu. Inachukuliwa kuwa dawa ya HOPO 14-1 itaweza kugeuza baadhi ya dutu hatari ambayo hutumiwa katika uundaji wa kinachojulikana kama "mabomu machafu", ikiwa ni pamoja na urani yaani uranium.

Ikiwa dawa hiyo itapatikana kuwa salama na yenye ufanisi, inaweza kulinda dhidi ya madhara yanayoweza kutokea kutokana na ajali za nyuklia au mashambulizi ya kigaidi.

Karibu watu 40 wa kujitolea watakunywa dozi mbalimbali za dawa.

Madaktari watafuatilia madhara yatakayojitokeza na afya za watu wa kujitolea.

Matokeo ya awamu ya kwanza ya utafiti huo yanatarajiwa mwaka wa 2024, wanasema viongozi wa utafiti kutoka SRI International yenye makao yake California (iliyofadhiliwa na shirika la serikali la Taasisi za Kitaifa za Afya (NIH).

"Bomu chafu" ni nini?

"Bomu chafu" pia huitwa kilipuzi chenye mionzi. Wakati bomu kama hiyo inalipuka, uchafuzi wa mionzi katika eneo jirani hutokea.

Tume ya Kudhibiti Nyuklia ya Marekani haizingatii "bomu chafu" kama silaha ya nyuklia au silaha ya maangamizi makubwa.

Wingu la mionzi kutoka kwa bomu chafu linaweza kutoweka ndani ya vitalu vichache au kilomita kadhaa kutoka eneo la mlipuko, wakati eneo la uchafuzi baada ya mlipuko wa silaha ya nyuklia linaweza kuenea makumi ya maelfu ya kilomita za mraba.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, mionzi bado inaweza kuharibu vinasaba au DNA, tishu, na viungo vya mtu, na kusababisha magonjwa, ikiwa ni pamoja na saratani.

Kwa hiyo, wanasayansi wanatafuta dawa ambayo inaweza kukabiliana au angalau kupunguza athari za mionzi.

Dawa mbili za sindano sasa zimetengenezwa ili kuwasaidia watu wanapoathiriwa na dutu za kemikali ya mionzi aina ya plutonium, americium au curium.

Wanasayansi wamejua kwa miaka mingi kwamba tembe za iodini zinaweza kutumika kulinda dhidi ya athari za mionzi – zilizopewa watu mwaka wa 1986 baada ya ajali katika kiwanda cha nyuklia cha Chernobyl.

Dawa nyingine, Prussian blue (potasiamu hexacyanoferrate), inaweza kusaidia kuondoa mionzi ya cesium na thallium kutoka kwa mwili wa binadamu.

Ikiwa HOPO 14-1 itathibitika kuwa na ufanisi, madaktari wataweza kutoa ulinzi dhidi ya urani na neptunium pamoja na plutonium, americium na curium.

Bado hakuna shambulio moja la "bomu chafu" lililofanikiwa ulimwenguni, ingawa kumekuwa na majaribio kama hayo.

Kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Pamoja wa Ulinzi wa Kifalme wa Uingereza (RUSI), mnamo 1996, waasi wa Chechnya walitega bomu na baruti na mionzi ya caesium-137 katika Hifadhi ya Izmailovsky ya Moscow.

Aligunduliwa na huduma za usalama na hakukuwa na madhara.

Mnamo 1998, mashirika ya kijasusi ya Urusi yaligundua na kutegua bomu chafu lililotegwa karibu na njia ya reli huko Chechnya, shirika hilo lilisema katika ripoti.